Hapa itakuwa ni haramu kuingiza king´amuzi/dishi nyumbani

Swali: Unajua kuwa kumetokea fitina kubwa kwa kutazama hizi king´amuzi/dishi. Baadhi ya watu – na ulinzi unaombwa kwa Allaah – huenda wakaiingiza majumbani mwao na kati ya watoto wake. Ni ipi taaliki yako?

Jibu: Taaliki yangu juu ya haya ni kwamba mtu anapaswa kumcha Allaah juu ya nafsi yake na familia yake na asiingize king´amuzi/dishi hizi kwenye majumba. Kwa sababu mtu anaingiza kwa hoja kwamba anataka kutazama taarifa ya khabari peke yake au zile elimu zinazorushwa ndani yake. Lakini inamvuta mpaka anatumbukia kwenye udongo wake.

Nimesikia kuhusu watu wenye msimamo wenye viwango vya juu katika elimu ambao wameingiza king´amuzi/dishi hizi kwa lengo la kutaka kutazama taarifa ya khabari na baadhi ya mambo ya kielimu, tahamaki wakapinduliwa. Khatari yake ni kubwa.

Kuhusu wale wenye kuziingiza majumbani mwao na wao wanaziona familia zao wanatazama maovu haya makubwa, mimi nawauliza: watu hawa wanazingatiwa wanazitakia kheri familia zao au wamewafanyia ghushi? Hapana shaka kwamba wamewafanyia ghushi. Kwa sababu wana uwezo wa kuwakataza kwa kuitoa na kuivunja. Akishakuwa ni mwenye kufanya ghushi anaingia ndani ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna mja Allaah atamchungisha raia na akafa siku atayokufa ilihali ni mwenye kuwafanyia ghushi isipokuwa Allaah atamuharamishia Pepo.”

Ndugu! Jambo ni la khatari. Kwa ajili hiyo naona kuwa ni haramu kwa mtu kuingiza king´amuzi/dishi hizi ikiwa anajua kuwa familia yake itatazama yale ambayo hayafai kutazamwa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (72) http://binothaimeen.net/content/1662
  • Imechapishwa: 10/04/2020