Swali: Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) makatazo ya kuukebeshi uso na kwamba Allaah (Subhaanah) amemuumba Aadam kwa sura Yake. Ni ipi imani sahihi ya muislamu juu ya mfano wa Hadiyth kama hii?

Jibu: Hadiyth imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Atapopiga mmoja wenu basi ajiepushe na uso. Kwani hakika Allaah amemuumba Aadam kwa sura Yake.”

Katika matamshi mengine imekuja:

“Atapopiga mmoja wenu basi ajiepushe na uso. Kwani hakika Allaah amemuumba Aadam kwa sura ya Mwingi wa huruma.”

Haya hayapelekei katika mashabihisho wala kumpigia Allaah mfano.

Maana yake kwa mujibu wa wanachuoni ni kwamba Allaah amemuumba Aadam akiwa ni mwenye kusikia, mwenye kuona na mwenye kuzungumza anapotaka. Hizi vilevile ndio sifa za Allaah; ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona na Mwenye kuzugumza anapotaka. Vilevile ana uso (Jalla wa ´Alaa). Haina maana ya kushabihisha na kumfananisha. Sura alionayo Allaah sio sura walionayo viumbe. Maana yake ni kwamba ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona na ni Mwenye kuzungumza pale anapotaka. Vivyo hivyo ndivyo Allaah alivyomuumba Aadam hali ya kusikia, mwenye kuona, akiwa na uso na unyanyo. Lakini kusikia kwa Allaah Allaah hakufanani kusikia kwa Aadam, kuona kwa Allaah hakufanani na kuona kwa Aadam, kuzungumza kwa Allaah hakufanani na kuzungumza kwa Aadam. Bali Allaah ana sifa zinazolingana na utukufu na ukubwa Wake na mja vilevile ana sifa zinazoingiliwa na ukomo na upungufu. Upande mwingine sifa za Allaah (Subhaanah) ni kamilifu na haziingiliwi na upungufu, kutoweka na ukomo. Kwa ajili hii ndio maana akasema (Subhaanah):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“Wala hakuna yeyote anayefanana na kulingana Naye.”[2]

Kwa hivyo haijuzu kuupiga wala kuukebehi uso.

[1] 42:11

[2] 112:04

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/226)
  • Imechapishwa: 02/07/2017