Swali: Je, ni halali kwa waislamu kusherehekea msikitini ili wakumbuke historia ya Mtume katika usiku wa tarehe 12 Rabiy´ al-Awwaal katika mnasaba wa mazazi ya Mtume mtukufu bila ya kuuharibu mchana wao kama idi? Tumetofautiana; wako waliosema kuwa ni Bid´ah nzuri na wengine wakasema kuwa sio Bid´ah nzuri.

Jibu: Haifai kwa waislamu kusherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika usiku wa tarehe 12 Rabiy´ al-Awwaal wala wakati mwingine. Kama ambavyo haifai kwa wao kusherehekea sherehe yoyote kwa kuzaliwa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu kusherehekea maulidi ni miongoni mwa Bid´ah zilizozuliwa katika dini. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakusherehekea kuzaliwa kwake katika maisha yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilihali yeye ndiye mfikishaji wa dini na muwekaji Shari´ah kutoka kwa Mola Wake (Subhaanah), hakuamrisha jambo hilo, hayakufanywa na makhaliyfah wake waongofu, Maswahabah zake wote wala wale waliowafuata kwa wema katika zile karne bora. Kwa hivyo imetambulika kuwa ni katika Bid´ah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayezusha katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo ndani yake atarudishiwa mwenyewe.”

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Mwenye kufanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”

Kusherehekea maulidi si jambo lenye kuafikiana na amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bali ni miongoni mwa mambo yaliyozuliwa na watu katika karne za mwisho. Kwa hivyo yanakuwa ni yenye kurudishwa. Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema katika Khutbah zake za ijumaa:

“Amma ba´d: Hakika maneno bora ni Kitabu cha Allaah, uongofu bora ni wa uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa na kila Bid´ah ni upotevu.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake. an-Nasaa´iy kwa cheni ya wapokezi nzuri na akazidisha:

“Kila upotevu ni Motoni.”

Kusoma khabari zinazohusiana na mazazi ndani ya masomo yanayozungumza historia yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maisha yake kabla ya kuja Uislamu na baada ya kuja Uislamu yanayosomwa masomoni, misikitini na kwenginepo kunatosheleza kutokamana na kusherehekea maulidi. Hakuna haja ya kuzusha sherehe ambazo hazikuwekwa na Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hazikusimama juu ya dalili ya Kishari´ah. Tunamuomba Allaah awaongoze waislamu wote na watosheke na Sunnah na watahadhari kutokamana na Bid´ah.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/884/%D9%87%D9%84-%D9%8A%D8%AD%D9%84-%D9%84%D9%84%D9%85%D8%B3%D9%84%D9%85%D9%8A%D9%86-%D8%A7%D9%86-%D9%8A%D8%AD%D8%AA%D9%81%D9%84%D9%88%D8%A7-%D8%A8%D8%A7%D9%84%D9%85%D9%88%D9%84%D8%AF-%D8%A7%D9%84%D9%86%D8%A8%D9%88%D9%8A
  • Imechapishwa: 15/11/2019