Elimu ya Allaah inajua yasiyokuwepo

Hakika Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) aliwajua viumbe Wake kabla ya kuwaumba na anawajua baada ya kuwaumba. Mwandishi – Imaam at-Twahaawiy – anawaraddi Mu´tazilah ambao wanasema kuwa Allaah hawajui viumbe isipokuwa baada ya kuwaumba. Hii ni batili ya batili.

Elimu ya Allaah imeenea kujua mambo ya kale, ya sasa na yaliyoko mbele. Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) anajua yaliyokuwa hapo kale, yatayokuwa huko mbeleni na vilevile Anajua yasiyokuwepo lau yangelikuwepo yangelikuwa namna gani. Kama ilivo katika Kauli Yake (Subhaanahu) kuhusu makafiri ambao waliomba kurudishwa duniani [ili kutenda matendo mema]. Amesema (Ta´ala):

وَلَوْ رُدُّوا لَعَادُوا لِمَا نُهُوا عَنْهُ وَإِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ

“Na lau wangelirudishwa kwa yakini wangeyarudia yale waliyokatazwa. Hakika wao ni waongo.” (06:28)

Anajua hali yao lau watarudishwa itavokuwa. Vilevile Kauli Yake (´Azza wa Jall):

وَلَوْ عَلِمَ اللَّـهُ فِيهِمْ خَيْرًا لَّأَسْمَعَهُمْ ۖ وَلَوْ أَسْمَعَهُمْ لَتَوَلَّوا وَّهُم مُّعْرِضُونَ

“Na kama Allaah Angelijua kuwa wana kheri yoyote ile, basi Angeliwasikilizisha na kama Angeliwasikilizisha, wangeligeuka nao huku wakipuuza.” (08:23)

Mfano pia wa Kauli Yake (Subhaanahu wa Ta´ala) juu ya wanafiki ambao walikwepa vita vya Tabuuk:

وَلَوْ أَرَادُوا الْخُرُوجَ لَأَعَدُّوا لَهُ عُدَّةً وَلَـٰكِن كَرِهَ اللَّـهُ انبِعَاثَهُمْ فَثَبَّطَهُمْ وَقِيلَ اقْعُدُوا مَعَ الْقَاعِدِينَ لَوْ خَرَجُوا فِيكُم مَّا زَادُوكُمْ إِلَّا خَبَالًا وَلَأَوْضَعُوا خِلَالَكُمْ يَبْغُونَكُمُ الْفِتْنَةَ وَفِيكُمْ سَمَّاعُونَ لَهُمْ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِالظَّالِمِينَ

“Na lau wangelitaka kutoka [kwenda vitani], wangeliandaa maandalizi yake, lakini Allaah Amekirihika kutoka kwao, basi Akawazuia na ikasemwa: “Kaeni [mbakie majumbani] pamoja na wanaokaa. Lau wangelitoka nanyi, wasingelikuzidishieni isipokuwa machafuko na wangeliharakia huku na huku baina yenu kukutakieni fitnah – na miongoni mwenu wako wanaowasikiliza kwa makini [kwa ujasusi]. Na Allaah ni Mjuzi kwa madhalimu.” (09:46-47)

Hakika (Subhaanahu wa Ta´ala) Anajua kungelitokea nini endapo wangelitoka.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/96-97)
  • Imechapishwa: 31/05/2020