”Burudika na acha kujizeekesha kwa kuvaa Hijaab”

Swali: Mimi ni muislamu wa kike na hufanya kila kinachomridhisha Allaah. Ni mwenye kujisitiri kwa Hijaab ya ki-Shari´ah. Lakini mama yangu – Allaah amsamehe – hataki nilazimiane na Hijaab na ananiamrisha kutazama sinema, video na kadhalika na kwamba eti nisipostarehe na kujitanafasi basi nitakuwa mzee na nywele zangu zitakuwa mvi.

Jibu: Ni lazima kwako kumfanyia upole mama yako, umtendee wema na uzungumze naye kwa njia nzuri. Kwa sababu haki ya mama ni kubwa. Lakini haifai kumtii katika yasiyokuwa mema. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakika si venginevyo utiifu ni katika yaliyo mema.”

”Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba.”

Vivyo hivyo inapokuja kwa baba, mume na wasiokuwa wao. Haifai kuwatii katika mambo yanayohusiana na kumwasi Allaah kutokana na Hadiyth zilizotajwa. Lakini hata hivyo inatakiwa mke, mtoto na wengine watumie upole na njia nzuri katika kuyatatua matatizo mbalimbali. Wafanye hivo kwa kubainisha dalili za kidini na ulazima wa kumtii Allaah na Mtume Wake na matahadharisho ya kumwasi Allaah na Mtume Wake. Sambamba na hilo mtu awe imara juu ya haki na kutomtii yule mwenye kuamrisha kwenda kinyume nao. Ni mamoja awe mume, baba, mama au wengineo.

Hakuna makatazo ya wewe kutazama yale yasiyokuwa na maovu kwenye runinga, video, kusikiliza nad-wah za kielimu na darsa zenye manufaa. Sambamba na hilo mtu atahadhari kutazama yale maovu yanayoonyeshwa ndani yake. Vivyo hivyo haijuzu kutazama sinema kutokana na ile batili inayokuwa ndani yake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (05/355)
  • Imechapishwa: 11/02/2021