Bora kuliko ´ibaadah ya miaka 83

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ

“Usiku wa Qadr ni bora kuliko miezi elfu.”[1]

Amebainisha fadhilah na ubora wake. Ubora wa wakati unatokana na zile fadhilah nyingi zinazopitika ndani yake. Katika usiku huo hugawanywa kheri nyingi ambazo hazipatikana kunako miezi mingine – na Allaah ndiye mjuzi zaidi. Wafasiri wengi wa Qur-aan wamesema kutenda matendo ndani yake ni bora kuliko miezi elfu tukiondosha usiku huo. Abul-´Aaliyah amesema:

“Usiku wa Qadr ni bora kuliko miezi elfu usiyokuwa na usiku wa Qadr.”

Kuna maoni mengine yanayosema miezi elfu kunamaanishwa maisha mazima. Kwa sababu waarabu wana mazowea ya kutumia elfu katika matukio mengi. Kama alivosema Allaah (Ta´ala):

يَوَدُّ أَحَدُهُمْ لَوْ يُعَمَّرُ أَلْفَ سَنَةٍ

”Anatamani wao lau angelipewa umri mrefu wa miaka elfu.”[2]

Maoni mengine yanasema kuwa hapo kale mtu alikuwa hahesabiki ni mwenye kumwabudu Allaah mpaka pale atakapomwabudu Allaah miezi elfu, kwa msemo mwingine miaka thamanini na tatu na miezi minne. Ndipo Allaah (Ta´ala) akaupa Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ´ibaadah ya usiku ambayo inashinda miezi elfu ya kufanya ´ibaadah. Abu Bakr al-Warraaq amesema:

“Ufalme wa Sulaymaan (´alayhis-Salaam) ulikuwa kwa miezi mia tano na ufalme wa Dhul-Qarnayn (´alayhis-Salaam) ulikuwa kwa miezi mia tano. Ukijumuisha ufalme wao inakuwa miezi elfu. Allaah akajaalia kitendo katika usiku huo kwa yule ambaye atakumbana nao ni bora kuliko ufalme wao.”

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anawatajia mwana wa israaiyl mmoja ambaye alikuwa amevaa silaha miezi elfu katika njia ya Allaah, Maswahabah wakashangazwa kutokana na jambo hilo na ndipo Allaah akateremsha:

لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ

“Usiku wa Qadr ni bora kuliko miezi elfu.”

Bi maana ni bora kuliko kipindi chote ambacho mtu yule alivaa silaha katika njia ya Allaah.”

Yamepokelewa mfano wa hayo pia kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

[1] 97:03

[2] 02:96

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Jaami’ li Ahkaam-il-Qur-aan (22/393)
  • Imechapishwa: 14/05/2020