Ibn Baaz kuhusu gauni refu la biharusi, wanawake kuimba na kupiga dufu harusini

Swali: Umetaja kwamba kurefusha nguo kwa nisba ya mwanaume ni haramu na pia kwa nisba ya mwanamke ikiwa ni kwa njia ya majivuno ni haramu. Unasemaje kuhusu gauni la harusi analovaa biharusi na nyuma linakuwa refu takriban mita 3? Unasemaje pia kuhusu pesa wanazopewa waimbaji wa kike harusini?

Jibu: Kuhusu yaliyofungamana na mwanamke Sunnah ni yeye kuteremsha vazi lake kiasi cha kiganja kimoja. Asizidishe juu ya dhiraa kwa sababu ya sitara na kutoonyesha nyayo za miguu. Kuhusu kuzidisha juu ya dhiraa ni maovu kwa biharusi na mwenginewe. Ni kitendo kisichojuzu. Huku ni kuharibu mali pasi na haki juu ya mavazi ambayo yana bei kubwa. Kwa hiyo inatakiwa kufanya wastani katika mavazi. Hakuna haja ya kuiharibu juu ya mambo ambayo yanaiteketeza mali nyingi ambayo inaweza kuwanufaisha watu katika dini na dunia yao.

Kuhusu yale yaliyofungamana na waimbaji wa kike haijuzu kuwafanya wakaja kwa pesa nyingi. Lakini hata hivyo hakuna neno kama ni mwimbaji wa kike ambaye anaimba nyimbo ya kawaida, nyepesi na khafifu katika sehemu ya usiku kwa ajili ya kudhihirisha furaha na kudhihirisha harusi.

Kuimba na kupiga dufu harusini ni jambo linalojuzu[1]. Bali ni jambo lililopendekezwa ikiwa halipelekei katika shari. Lakini iwe kati ya wanawake tu na khaswa katika sehemu ya usiku. Jengine mambo yaishilie bila ya watu kukesha usiku mzima wala kuweka kipaza sauti. Bali iwe ni nyimbo ya kawaida ambayo ndani yake anasifiwa biharusi, bwanaharusi kwa haki, watu wa familia ya biharusi na mfano wa hayo katika maneno ambayo ndani yake hamna shari. Mambo hayo yafanyike kati ya wanawake peke yake na kusiwe mwanamume hata mmoja. Vilevile waimbe bila ya kipaza sauti. Katika hali hii hakuna neno. Ni kama ada yenye kufuatwa katika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakati wa Maswahabah.

Ama mambo ya kufakharishana kwa waimbaji wa kike na kwa mali nyingi kwa ajili ya waimbaji wa kike ni mambo ambayo hayajuzu. Vivyo hivyo inapokuja katika vipaza sauti. Kwa sababu mambo hayo yanapelekea kuwaudhi watu na kukesha usiku mpaka watu wanapitwa na swalah ya Fajr, mambo ambayo ni maovu ambayo ni lazima kuyawacha.

[1] Tazama https://firqatunnajia.com/39-kuimba-nyimbo-na-kupiga-dufu-harusini/

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/121)
  • Imechapishwa: 26/02/2020