Swali: Miongoni mwa makosa vilevile ni kwamba wanawake wanaenda kwa wingi masokoni na khaswakhaswa mwishoni mwa mwezi wa Ramadhaan.

Jibu: Hili ni kosa jengine. Kwanza mwanamke nyumbani kwake ni bora kwake. Hata kuhusu Tarawiyh lau atabaki nyumbani ni bora kwake. Lakini baadhi ya wanawake wanasema kuwa eti wanasikia uvivu iwapo watabaki nyumbani na wala hawawezi kuswali Tarawiyh, tunasema: hakuna neno. Haya ni manufaa na hivyo nenda msikitini. Ama kuzurura katika masoko pamoja na uwepo wa wapumbavu wengi ni kosa. Ni lazima kwa wasimamizi wa wanawake wawazuie kutokamana na hili.

Swali: Vipi kuhusu kufuatilia musalsal na chaneli zinazoshindana katika mwezi huu?

Jibu: Kufuatilia musalsal na filamu chafu katika mwezi huu ni haramu. Ni haramu katika miezi mingine vilevile. Lakini katika mwezi huu uharamu unakuwa mkubwa zaidi. Kwa sababu huu ni mwezi wa ´ibaadah, mwezi wa kumcha Allaah na mwezi wa kujitenga mbali na mambo ya haramu. Ni wajibu kwa wasimamizi wa wanawake wawazuie wale ambao Allaah amewatawalisha juu yao kutokamana na kutazama musalsal hizi.

Swali: Vijana kujishughulisha na michezo usiku.

Jibu: Michezo imegawanyika sehemu mbili:

1- Michezo iliyoruhusiwa: Mashindano ya mbio za miguu, mchezo wa mpira ikiwa hawatoonyesha vile viungo visivyotakiwa kuonekana, ugomvi na mivutano. Michezo kama hii haina neno. Lakini sioni kuwa wakeshe usiku mzima katika mambo haya. Kwani ni kupoteza muda. Kusanyikeni nyumbani mkisomeshana Qur-aan au laleni ili mpate nguvu za kufanya ´ibaadah mchana. Kwa sababu watu wengi wanakesha usiku mzima na wanashinda mchana mzima wamelala. Baya zaidi ni kwamba baadhi ya watu wanalala baada ya kuswali Fajr na hawaamki isipokuwa baada ya jua kuzama. Hivyo wanaacha swalah. Hili ni kosa kubwa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (70) http://binothaimeen.net/content/1563
  • Imechapishwa: 29/02/2020