´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya adhabu ya kaburi

Swali: Ni ipi ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kuhusu adhabu ya ndani ya kaburi? Kunaadhibiwa roho peke yake au ni roho na kiwiliwili?

Jibu: ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuamini adhabu na neema za ndani ya kaburi. Maiti ima akastareheshwa na ima akaadhibiwa. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanayaamini haya. Yameelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kaburi ima ni bustani miongoni mwa mabustani ya Peponi au ni shimo miongoni mwa mashimo ya Motoni.

Ni lazima kwa muislamu kuyaamini haya. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapitia watu wawili ambao wanaadhibiwa. Mmoja wao kazi yake ilikuwa kueneza umbea na mwengine alikuwa hajichungi na cheche za mkojo.

Ahl-us-Sunnah wanaamini adhabu na neema za ndani ya kaburi na kwamba ni haki. Ni juu ya roho na kiwiliwili vyote viwili. Lakini kinachokuwa na hisia zaidi ni roho. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema kuhusu watu wa Fir´awn:

النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا

“Wanaonyeshwa moto asubuhi na jioni.”[1]

Vivyo hivyo maiti. Mtu mwema anastareheshwa ndani ya kaburi lake na asiyekuwa mwema anaadhibiwa ndani ya kaburi lake. Siku ya Qiyaamah adhabu inakuwa kubwa zaidi na neema zinakuwa kubwa zaidi. Hapa ni baada ya watu wameshafufuliwa na kukusanywa.

[1] 40:46

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa ad-Duruus https://binbaz.org.sa/fatwas/3105/%D9%85%D8%A7-%D8%B9%D9%82%D9%8A%D8%AF%D8%A9-%D8%A7%D9%87%D9%84-%D8%A7%D9%84%D8%B3%D9%86%D8%A9-%D9%88%D8%A7%D9%84%D8%AC%D9%85%D8%A7%D8%B9%D8%A9-%D9%81%D9%8A-%D8%B9%D8%B0%D8%A7%D8%A8-%D8%A7%D9%84%D9%82%D8%A8%D8%B1
  • Imechapishwa: 08/02/2020