Unasema kwenye barua yako:

“Nyakati zote anasifiwa katika vikao na vitabu vyake vinasomwa.

Lakini tangu miaka saba ya nyuma ndugu wengi wamemshambulia na kumpokonya haki yake.”

Je, hii ni hoja kwa mimi kusifu mfumo wake? Je, hii ni hoja kwa mtu anayemsifu bila ya kujua makosa makubwa yanayopatikana katika mfumo wake? Hii sio hoja ya kwamba mfumo wake ni sahihi. Wewe mwenyewe unajua ndani ya nafsi yako kuwa hii sio hoja na kwamba wamemsifu pindi walipokuwa wamedanganyika na muonekano wa kijumla wa mfumo wake. Wakati walipojua yaliyomo, wakaukemea kwa haki zote.

Ee Allaah! Hakika wewe unajua kuwa sikusudii kumjeruhi wala kumtukana yeyote. Ninacholenga tu ni kubainisha haki na kuwatahadharisha vijana juu ya mifumo ilio na Bid´ah na upotevu. Tunawazindua tu juu ya makosa yaliyo kwenye mifumo ili wasije kudanganyika nayo na wakajiunga nao na matokeo yake wakaja kupotea wao na wakawapoteza wengine.

Kuhusu kwamba wamempokonya haki yake, sio sahihi kabisa. Wao wamesema tu yaliyopokelewa kutoka kwake kutoka katika vyanzo sahihi, majina ya vitabu vyake na namba za kurasa. Je, wamempokonya haki yake pindi waliponukuu maneno hayo ili kuwakinaisha vijana ya kwamba huo ni mfumo wa kimakosa kwa sababu uko na haki na batili? Wewe mwenyewe utapendelea kunywa nini lau uko na kinywaji kilichochanganyika na uchafu na kinywaji kingine ni kisafi na hakina uchafu? Hivyo watakuwa wamempokonya haki yake?

Lengo la kuumbwa mbingu, ardhi na kutumwa Mitume na kuteremshwa vitabu ni ili kuhakikisha haki na kuivunja batili. Hali kadhalika kuamrisha mema na kukataza maovu. Ikiwa juu ya ardhi hakuna yeyote mwenye kuamrisha mema na kukataza maovu, hakika itapelekea katika ghadhabu. Kukiwepo ghadhabu, basi adhabu ya Allaah ndio itashuka. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِذَا وَقَعَ الْقَوْلُ عَلَيْهِمْ أَخْرَجْنَا لَهُمْ دَابَّةً مِّنَ الْأَرْضِ تُكَلِّمُهُمْ أَنَّ النَّاسَ كَانُوا بِآيَاتِنَا لَا يُوقِنُونَ

“Na itakapowaangukia kauli [kwa uwazi wake] Tutawatolea mnyama atembeaye katika ardhi atakayewasemezesha [aseme] kwamba watu walikuwa hawana yakini na alama Zetu.”[1]

Qataadah amesema:

“Itapowaangukia kauli maana yake watapofikiwa na ghadhabu.”

Ibn ´Umar na Abu Sa´iyd al-Khudriy wamesema:

“Pale ambapo hawatoamrishana mema na kukatazana maovu, basi ghadhabu itawawajibikia.”

´Abdullaah bin Mas´uud amesema:

“Wataangukiwa na kauli kwa kufa kwa wanachuoni, elimu kupotea na Qur-aan kunyanyuliwa.”

Hili linapata kubainisha ya kwamba kuamrisha mema na kukataza maovu ni kinga dhidi ya kuteremka kwa adhabu na ghadhabu za Allaah (´Azza wa Jalla) juu ya waja Wake.

Miongoni mwa kuamrisha mema na kukataza maovu ni pamoja na kuraddi makosa ya ki-´Aqiydah pasi na kujali ni ya nani na mahali walipo. Je, wataka watu wa Haki wanyamazie hilo pasi na kulibainisha na kulichuja na uchafu na yasiyostahiki? Hili kamwe – Allaah akitaka – halitokuweko muda wa kuwa Hadiyth na haki ina wanaume wake.

[1] 27:82

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Radd-ul-Jawaab, uk. 23-27
  • Imechapishwa: 05/07/2020