1Wakati Abramu alipokuwa na umri wa miaka tisini na tisa, Mwenyezi Mungu alimtokea, akamwambia: “Mimi ni Mungu mwenye nguvu. Fuata mwongozo wangu na kuishi bila lawama. 2Nami nitafanya agano nawe na kuwazidisha wazawa wako.” 3Hapo Abramu akasujudu. Naye Mungu akamwambia, 4“Ninafanya agano hili nawe: Utakuwa baba wa mataifa mengi. 5Tangu sasa, hutaitwa tena Abramu, bali utaitwa Abrahamu, maana nimekufanya kuwa baba wa mataifa mengi. 6Nitakufanya uwe na wazawa wengi sana; kwako nitazusha mataifa mengi na wafalme. 7Nitalithibitisha agano langu nawe, wazawa wako na vizazi vyao vyote milele; tena nitakuwa Mungu wako na Mungu wa wazawa wako milele. 8Nitakupa wewe na wazawa wako nchi hii ambamo unaishi kama mgeni; yaani nchi yote ya Kanaani iwe mali yenu milele; nami nitakuwa Mungu wao.”

  • Marejeo: Mwanzo 17:1-08 https://www.bible.com/sw/bible/74/GEN.17.BHN
  • Imechapishwa: 12/02/2020