´Abdur-Rahmaan bin ´Awf


´Abdur-Rahmaan bin ´Awf bin ´Abd bin al-Haarith bin Zuhrah bin Kullaab bin Murrah bin Ka´b bin Lu’ayy al-Qurashiy az-Zuhriy. Abu Muhammad.

Ni mmoja katika wale kumi. Ni pia ni mmoja katika wale watu wa mashauriano. Ni mmoja katika wale waislamu wa mwanzo waliopigana vita vya Badr. Ni mmoja katika wale nane ambao walikimbilia kuingia katika Uislamu.

Amepokea Hadiyth nyingi. Baadhi ya waliopokea kutoka kwake ni Ibn ´Abbaas, Ibn ´Umar na Anas bin Maalik.

Katika kipindi cha kikafiri alikuwa akiitwa ´Abd ´Amr. Imesemekana vilevile kwamba alikuwa akiitwa ´Abdul-Ka´bah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akalibadilisha jina lake kwenda ´Abdur-Rahmaan.

al-Madaa-iniy amesema:

”´Abdur-Rahmaan alizaliwa miaka kumi baada ya mwaka wa ndovu.”

Jamaa´ah wamesema kuwa mama yake alikuwa anaitwa ash-Shifaa´ bint ´Awf bin ´Abd bin al-Haarith bin Zuhrah.

´Abdur-Rahmaan bin ´Awf amesema:

”Jina langu lilikuwa ´Abd ´Amr. Pindi niliposilimu, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanibadilisha jina ´Abdur-Rahmaan.”[1]

Sahlah bint ´Aaswim amesema:

”´Abdur-Rahmaan alikuwa mweupe. Alikuwa na macho mapana na kope ndefu. Alikuwa mwenye kuinama. Alikuwa na meno mawili ya kwenye kono marefu ambayo wakati mwingine yanamfanya midomo yake kutokwa na damu. Nywele zake zilikuwa zinateremka mpaka kwenye masikio yake. Alikuwa na shingo refu na mabega makubwa.

Ibn Ishaaq amesema:

”Amevunjwa meno ya mbele. Alikuwa mwenye kutumia mkono wa kushoto na ni mlemavu wa mguu. Alipoteza meno yake ya mbele katika vita vya Uhud. Alijeruhiwa majeraha ishirini ambapo baadhi yalikuwa mguuni mwake. Hivyo akawa kiguru.”[2]

Miongoni mwa fadhilah zake ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimshuhudia Peponi. Aidha ni miongoni mwa wale walioshiriki vita vya Badr ambao waliambiwa:

”Fanyeni mtakavyo.”[3]

Ni miongoni mwa wale waliotajwa katika Aayah:

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ

“Hakika Allaah amewawia radhi waumini waliokupa kiapo cha usikivu na utiifu chini ya mti.”[4]

Vilevile Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwahi kuswali nyuma yake. ´Amr bin Wahb ath-Thaqafiy amesema:

”Tulikuwa pamoja na al-Mughiyrah bin Shu´bah wakati alipoulizwa: ”Je, kuna mtu mwingine mbali na Abu Bakr ambaye alimswalisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?” Akajibu: ”Ndio.” Kisha akataja namna ambavyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitawadha na akafuta juu ya soksi na kilemba chake na jinsi yeye pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakaswali Rak´ah moja ya swalah ya Fajr nyuma ya ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf. Baadaye wakalipa Rak´ah iliyokuwa imewapita.”[5]

Qataadah amesema kuhusu Aayah:

الَّذِينَ يَلْمِزُونَ الْمُطَّوِّعِينَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ فِي الصَّدَقَاتِ

”Wale wanaowabeua waumini wanaotoa swadaqah nyingi.”[6]

”´Abdur-Rahmaan bin ´Awf alitoa swadaqah nusu ya mali yake, vipande vya dhahabu elfunne. Ndipo wanafiki wakasema: ”´Abdur-Rahmaan ni mtu mkubwa mwenye kujionyesha.”[7]

´Abdur-Rahmaan bin ´Awf amesema:

”Nimeiona Pepo na jinsi ninavyoingia kwa kutambaa. Nimeona kwamba hawatoingia ndani yake isipokuwa mafukara peke yake.”

Cheni ya wapokezi wake ni nzuri. Hii, na nyinginezo, ni ndoto na ndoto zina tafsiri zake. Ibn ´Awf (Radhiya Allaahu ´anh) amenufaika kwa yale aliyoyaota na yale yaliyomfikia. Jambo hilo lilimfanya kutoa pesa nyingi. Hivyo miguu yake ikafunguliwa na akawa ni miongoni mwa wenye kurithi firdaws. Kwa hivyo haitomdhuru.”

Sa´iyd bin Zayd amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´aalyhi wa sallam) alikuwa juu ya Hiraa´ akiwa pamoja na Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan, ´Aliy, Twalhah, az-Zubayr, Sa´d na ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf na akasema: ”Tulizana, ee Hiraa´! Hakika juu yako yuko Nabii, mkweli au shahidi.”[8]

Abu Hurayrah ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´aalyhi wa sallam) amesema:

”Mbora wenu ni yule ambaye ni mbora kwa familia yake.”

Ndipo ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf akaacha usia wa bustani ambalo lilikuwa na thamani ya dinari 400.000.”[9]

Umm Bakr bint al-Miswar ameeleza kwamba ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf alimuuzia ardhi yake ´Uthmaan kwa dinari 40.000. Akazigawanya pesa hizo kwa mafukara wa kabila la Zuhrah, Muhaajiruun na mama wa waumini.”

Miongoni mwa fadhilah bora kabisa ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf ni kwamba alijichomoa miongoni mwa wale watu wa mashauriano na kujitahidi kuchagulia Ummah ambaye ni mbora kabisa ambaye aliashiriwa na watu wasimamizi. Laiti angelikuwa anataka utawala, basi angeliuchukua mwenyewe au angempa binamu yake a mbaye ni Sa´d bin Abiy Waqqaas.”

Niyaar al-Aslamiy amesema:

”´Abdur-Rahmaan bin ´Awnf alikuwa ni mmoja katika watu wanaojibu maswali zama za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Abu Bakr na ´Umar kutokana na yale aliyosikia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Mujaahid amesimulia kutoka kwa ash-Sha´biy ambaye amesema kuwa ´Abdur-Rahmaann bin ´Awf ndiye ambaye aliongoza hijjah ya mwaka wa 13.

Sa´iyd bin al-Musayyab ameeleza kwamba Sa´d bin Abiy Waqqaas alimtuma mjumbe kwenda kwa ´Abdur-Rahmaan wakati alipokuwa amesimama na huku anatoa Khutbah akasema: ”Waite watu kwa nafsi yako mwenyewe!” Ndipo ´Abdur-Rahmaan akasema: ”Hakuna yeyote aliyechukua uongozi baada ya ´Umar isipokuwa alilaumiwa na watu.”

Twalhah bin ´Abdir-Rahmaan bin ´Awf amesema:

”Watu wa al-Madiynah walikuwa wakimtegemea ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf: theluthi ya mali yake anawaazima, theluthi nyingine anawalipia madeni yao na akiweka theluthi nyingine kwa ajili ya jamaa zake.”

Ibn-ul-Musayyab amesema:

”Kulikuwa na mtengano fulani kati ya Twalhah na Ibn ´Awf. Twalhah akagonjweka, ´Abdur-Rahmaan akaja kumtembelea. Ndipo Twalhah akasema: ”Naapa kwa Allaah ndugu yangu kwamba wewe ni bora kuliko mimi.” Akasema: ”Usisemi hivo ndugu yangu.” Ndipo Twalhah akasema: ”Ndio. Kwa sababu endapo wewe ndiye umegonjweka basi mimi nisingekutembelea.”

Sa´d bin al-Hasan amesema:

”Ilikuwa huwezi kuona tofauti yoyote kati ya ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf na watumwa wake.”

Anas amesema:

”Niliona namna ambavo ´Abdur-Rahmaan anaacha anausia 100.000 kwa kila mmoja katika wake zake.”

Wakati alipohama kwenda al-Madiynah, alikuwa fakiri na hana chochote. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akajenga udugu kati yake yeye na Sa´d bin ar-Rabiy´. Sa´d akataka kumpa nusu ya mali yake na kumtaliki mrembo kabisa katika wakeze ili ampe yeye. Ndipo akamwambia: ”Allaah akubarikie familia na mali yako. Nioneshe soko liko wapi.” Akaenda kufanya biashara na akapata faida. Hakukupita muda mrefu mpaka akamiliki dirhamu. Akamuoa mwanamke na akampa dhahabu inayolingana na kokwa ya tende. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomuona na athari ya zafarani akamwambia: ”Umefanya karamu ya ndoa?” Akasema: ”Hapana.” Ndipo Mtume akamwambia: ”Fanya karamu ya ndoa japo kondoo mmoja tu.” Ndipo jambo lake la biashara likaishilia kama lilivyoishilia[10].

al-Madaa-iniy, al-Haytham bin ´Adiyy na wengineo wamesema kuwa alifariki mwaka wa 32. al-Madaa-iniy amesema:

”Alizikwa Baqiy´.”

Ya´quub bin al-Mughiyrah amesema:

“Aliishi miaka 75.”

Ibn ´Abdil-Barr amesema:

“Alikuwa amefanikiwa katika biashara. Aliacha ngamia elfu, kondoo elfutatu na farasi mia.”

Hali ndio hii ya tajiri mwenye kushukuru. Uways alikuwa fakiri mwenye kusubiri. Abu Dharr na Abu ´Ubaydah walikuwa ni wafanya ´ibaadah, wenye kuipa nyongo dunia na wenye kuchunga heshima zao.

[1] al-Haakim (3/306) ambaye ameisahihish na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[2] al-Haakim (3/308).

[3] al-Bukhaariy (3007) na Muslim (2494).

[4] 48:18

[5] Ahmad (4/249).

[6] 9:79

[7] at-Twabariy (10/195).

[8] Ahmad (1/188).

[9] al-Haakim (3/311) ambaye amesema: ”Ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim.” adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[10] al-Bukhaariy (2048).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa' (1/68-92)
  • Imechapishwa: 20/01/2021