94. Ngazi ya pili ya imani na sehemu zake


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ngazi ya pili ni Imani. Imegawanyika sehemu sabini na kitu. Ya juu yake ni neno “hapana mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah” na ya chini yake ni kuondosha kitu chenye kudhuru katika njia. Hayaa ni sehemu katika imani.

MAELEZO

Imani ni kitu kilichoenea zaidi kuliko Uislamu. Kila muislamu ni muumini na si kila muislamu ni muumini. Imani ni kitu maalum upande wa dhati yake na ni kitu maalum kwa upande wa watu wake.

Maana ya imani katika lugha ni kusadikisha. Amesema (Ta´ala) kupitia ndimi za nduguze Yuusuf:

وَمَا أَنتَ بِمُؤْمِنٍ لِّنَا وَلَوْ كُنَّا صَادِقِينَ

“Nawe hutotuamini japo tukiwa ni wakweli.”[1]

Ni mwenye kutusadikisha.

Kuhusu maana ya imani katika Shari´ah ni kama walivofasiri Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah: ni kutamka kwa mdomo, kuamini ndani ya moyo na matendo ya viungo vya mwili. Inazidi kwa utiifu na inapungua kwa maasi. Kwa tafsiri hii inakuwa ni uhakika wa Kishari´ah. Kwa sababu kuna uhakika aina tatu:

1- Uhakika wa kilugha.

2- Uhakika wa Kishari´ah.

3- Uhakika wa kidesturi.

Tafsiri ya imani kwa tafsiri hii ni uhakika wa Kishari´ah. Imani hutolewa katika maana ya kilugha na kupelekwa katika maana ya Kishari´ah.

Imani ni kutamka kwa mdomo – Ni lazima kutamka na kutambua kwa mdomo na kuamini moyoni. Ni lazima yale anayotamka kwa mdomo wake awe ni mwenye kuyaamini moyoni mwake. Vinginevyo atakuwa kama imani ya wanafiki ambao:

يَقُولُونَ بِأَلْسِنَتِهِم مَّا لَيْسَ فِي قُلُوبِهِمْ

“Wanasema kwa ndimi zao yasiyokuweko nyoyoni mwao.”[2]

Pia haitoshi kutamka kwa mdomo na kuamini ndani ya moyo. Ni lazima pia kufanya matendo ya viungo. Ni lazima kutekeleza faradhi na kujiepusha na mambo ya haramu. Mtu afanye matendo mema na ajiepushe na mambo ya haramu. Yote haya ni katika imani. Kwa maana hii kumeikusanya dini nzima. Lakini matendo yote haya na Shari´ah nyingi katika hayo yako ambayo ni sehemu katika uhakika wa imani na mengine ni yenye kuikamilisha imani.

Imani ina nguzo na tanzu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameyabainisha katika Hadiyth mbili. Amebainisha nguzo za imani katika Hadiyth ya Jibriyl na amebainisha tanzu za imani katika Hadiyth isemayo:

“Imani imegawanyika sehemu sabini na kitu.”

Itakuja huko mbele – Allaah akitaka.

Imani na Uislamu vikitajwa kwa pamoja kila kimoja kinakuwa na maana yake. Kukitajwa kimoja katika viwili hivyo basi kimoja kinaingia ndani ya kingine. Yakitajwa yote mawili basi Uislamu unafasiriwa kuwa ni yale matendo ya nje ambazo ni zile nguzo tano za Uislamu ilihali imani inafasiriwa kuwa ni yale matendo yenye kujificha ambazo ni zile nguzo sita za imani ambazo zimehusiana na moyo. Ni lazima yakusanyike kwa muislamu. Ni lazima awe muislamu na muumini kwa njia ya kwamba anasimamisha nguzo za Uislamu na anasimamisha nguzo za imani. Ni lazima ayakusanye yote mawili. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Imani ni sehemu sabini na kitu au ni sehemu sitini na kitu.”

Kumepokelewa mapokezi mawili[3].

Sehemu – Ni namba kati ya tatu mpaka tisa. Kunaposemwa “kumi na kitu” ni yaliyo kati ya kumi na tatu mpaka kumi na tisa. Kunaposemwa “sehemu” ni yaliyo kati ya tatu mpaka tisa.

Ya juu yake – Ya juu zaidi katika tanzu hizi ni kusema “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”. Ndio kichwa cha Uislamu, kichwa cha imani, nguzo ya kwanza na ndio inayomwingiza mtu katika dini.

Ya chini yake – Ya mwisho yake na ndogo yake.

Kuondosha chenye kudhuru… – Kuondosha kitu chenye kudhuru katika njia inayopitwa na watu. Inahusiana na kila chenye kuwadhuru watu kama mfano wa miba, mawe, uchafu na mambo yaliyo kinyume. Inahusiana na kila chenye kuwaudhi watu katika njia zao. Pia kuweka vyenye kudhuru katika njia ni kitendo cha haramu. Njia ni kwa ajili ya wenye kupita. Vyenye kudhuru vinawazuia wapitaji au vinawaweka khatarini. Kwa mfano mtu kupaki gari yake njiani. Haya ni katika madhara. Kuyafungulia maji kutoka nyumbani kwenda katika njia za watu. Haya pia ni katika madhara. Kuweka takataka katika njia za watu. Haya ni katika madhara. Ni mamoja njia hiyo iko mjini au kijijini. Mifano mingine ni kuweka mawe, kuni, kuweka vyuma katika njia za watu na kuchimba mashimo katika njia za watu. Yote haya ni katika madhara. Akija muislamu na kuondosha kitu hichi chenye kudhuru na akawafungulia njia kutokamana na kitu hichi ni dalili juu ya imani yake. Kuweka vyenye kudhuru njiani ni katika tanzu za ukafiri kama ambavo kuondosha vyenye kudhuru njiani ni katika tanzu za imani.

Hayaa ni sehemu… – Hayaa ni umbile ambalo Allaah huliweka kwa mtu linalomfanya kufanya yenye kumpamba na kuonekana mzuri na wakati huohuo linamzuia na yale yanayomchafua na kuonekana mbaya. Hayaa inayomfanya mwenye nayo kufanya mambo ya kheri na kujiepusha mbali na maovu ni yenye kusemwa vizuri. Ama hayaa inayomzuia mtu kufanya mambo ya kheri, kujifunza elimu na kuuliza mambo yanayomtatiza ni hayaa yenye kusemwa vibaya. Kwa sababu ni woga.

[1] 12:17

[2] 48:11

[3] al-Bukhaariy (09) kwa tamko:

”… na sitini.”

Pia Muslim (35) kwa upokezi wake kupiti kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 197-201
  • Imechapishwa: 20/01/2021