Ambaye amezigawanya Bid´ah kati ya Bid´ah nzuri na Bid´ah mbaya amekosea na amekhalifu maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika kila Bid´ah ni upotevu.”

Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amehukumu kwamba Bid´ah zote ni upotevu ilihali mtu huyu anasema:

“Si kila Bid´ah ni upotevu na kwamba zipo Bid´ah nzuri.”

Ibn Rajab amesema katika “Sharh-ul-Arba´iyn”:

“Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kila Bid´ah ni upotevu.”

ni miongoni mwa maneno yake machache yenye maana pana. Ndani yake hakutoki kitu. Ni msingi mkubwa katika misingi ya dini. Ni yenye kufanana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”[1]

Kila ambaye atazua kitu akakinasibisha katika dini na kisiwe na msingi wowote wa dini unaorejelewa, basi ni upotevu. Dini iko mbali kabisa na mtu huyo. Ni mamoja amefanya hivo katika mambo ya kiimani, matendo au maneno ya dhahiri au yaliyojificha.”[2]

Watu hawa hawana hoja yoyote juu ya kwamba kuna Bid´ah nzuri isipokuwa tu maneno ya ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) kuhusu swalah ya Tarawiyh:

“Neema ya Bid´ah iliyoje hii!”[3]

Vilevile wamesema kuwa kumezuliwa mambo ambayo Salaf hawakuyakemea. Kwa mfano Qur-aan ilikusanywa kwenye kitabu kimoja na kuandikwa kwa Hadiyth.

Majibu juu ya hayo ni kwamba mambo haya yana msingi katika Shari´ah. Kwa hivyo sio mambo yaliyozuliwa. Kuhusu maneno ya ´Umar:

“Neema ya Bid´ah iliyoje hii!”

anakusudia uzushi wa kilugha na si wa kidini. Kunaposemwa kuwa kitu fulani ni uzushi na wakati huohuo kikawa na msingi katika Shari´ah ambao unarejelewa, basi ni uzushi wa kilugha na si wa kidini. Kwa sababu uzushi wa kidini ni ule usiokuwa na msingi katika Shari´ah. Kuikusanya Qur-aan katika kitabu kimoja ni jambo lina msingi katika Shari´ah. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiamrisha iandikwe Qur-aan. Lakini ilikuwa imeandikwa sehemu mbalimbali. Ndipo Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wakaikusanya katika msahafu mmoja kwa ajili ya kuihifadhi.

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaswalisha Tarawiyh Maswahabah zake nyusiku kadhaa na mwishoni akawakwepa kwa kuchelea isije kufaradhishwa juu yao. Baadaye Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wakaendelea kuiswali makundimakundi mbalimbali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa hai na baada ya kufa kwake. Hali iliendelea hivo mpaka ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alipowakusanya nyuma ya imamu mmoja kama walivyokuwa nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hivyo huku sio uzushi katika dini.

Kuandikwa Hadiyth ni jambo lina msingi katika Shari´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliamrisha ziandikwe baadhi ya Hadiyth waandikiwe baadhi ya Maswahabah zake walipomuomba jambo hilo. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa akiandika Hadiyth katika kipindi cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kilichomzuia kuziandika kwa mtindo wa ujmla ni kuchelea Qur-aan isije kuchanganyika na yale yasiyokuwa Qur-aan. Wakati alipofariki (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kikaondoka kile alichokuwa anachelea. Kwa sababu Qur-aan imeshakamilika na imedhibitiwa kabla ya kufa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndipo waislamu wakazikusanya Hadiyth baada ya kufa kwake kwa ajili ya kuzihifadhi zisipotee. Allaah awalipe kheri nyingi kwa ajili ya Uislamu na waislamu kwa vile wamehifadhi Kitabu cha Mola wao na Sunnah za Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokamana na kupotea na mchezo wa wachezaji.

[1] al-Bukhaariy (2550) na Muslim (1718).

[2] Jaamiy´-ul-´Uluum wal-Hikam, uk. 233.

[3] Swahiyh-ul-Bukhaariy (2010).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 182-183
  • Imechapishwa: 02/07/2020