[13] Niliandika kwa upambanuzi suala hili katika “Swalaat-ut-Taraawiyh”, uk. 101-115, na kwa hivyo napendelea kulitaja hilo hapa kwa ufupi kama kumsahilishia na kumkumbusha msomaji:

Njia ya kwanza: Rak´ah kumi na tatu. Inafunguliwa kwa Rak´ah mbili fupi na kwa mujibu wa maoni yaliyo na nguvu ndio zile Rak´ah mbili za Sunnah baada ya ´Ishaa au Rak´ah mbili maalum ambazo inafunguliwa swalah ya usiku kwazo kama tulivyotangulia kusema. Halafu anaswali Rak´ah mbili ndefu kabisa. Kisha anaswali Rak´ah mbili fupi kuliko zilizotangulia. Kisha anaswali Rak´ah mbili fupi kuliko zile mbili zilizo kabla yake. Halafu anaswali Rak´ah mbili fupi kuliko zile mbili zilizo kabla yake. Kisha anaswali Rak´ah mbili fupi kuliko zile mbili zilizotangulia na kisha anaswali Witr kwa Rak´ah moja.

Njia ya pili: Rak´ah kumi na tatu. Kunaswaliwa Rak´ah nane na kutolewa Tasliym kila baada ya Rak´ah mbili. Halafu aswali Witr kwa Rak´ah tano na asikae na wala asitoe Tasliym isipokuwa katika ile ya tano.

Njia ya tatu: Rak´ah kumi na moja. Atoe Tasliym kila baada ya Rak´ah mbili na mwishowe aswali Witr kwa Rak´ah moja.

Njia ya nne: Rak´ah kumi na moja. Mtu anaswali nne kwa Tasliym moja kisha afanye hali kadhalika katika zile zengine nne zinazofuata na mwishowe mtu aswali tatu.

Je, alikuwa akikaa baina ya kila Rak´ah mbili wakati anaposwali nne na tatu? Hatukupata jibu lenye kutosheleza katika hilo, lakini haikuwekwa katika Shari´ah pindi mtu anaposwali tatu.

Njia ya tano: Rak´ah kumi na moja. Hapa hakai isipokuwa tu katika ile ya nane na anafanya Tashahhud, anamswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kisha anasimama bila kutoa Tasliym. Halafu anaswali Witr kwa Rak´ah moja kisha anatoa Tasliym. Zinakuwa tisa. Kisha anaswali Rak´ah mbili hali ya kukaa.

Njia ya sita: Aswali Rak´ah tisa na wala asikae isipokuwa katika ile Rak´ah ya sita. Halafu afanye Tashahhud, amswalie Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) n.k.

Hizi ndio namna zilizothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuna uwezekano vilevile wa kuongeza namna moja ambayo ni kupunguza idadi ya Rak´ah mpaka kubaki Rak´ah moja peke yake. Hili ni kujengea maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule anayetaka aswali Witr kwa tano, anayetaka aswali Witr kwa tatu na anayetaka aswali Witr kwa moja.”[1]

Hizi Rak´ah tano na tatu zinaweza kuswaliwa kwa kukaa mara moja na kutoa Tasliym mara moja kama ilivyo katika njia ya pili. Vilevile yule anayetaka anaweza kutoa Tasliym kila baada ya Rak´ah mbili kama ilivyo katika njia ya tatu, jambo ambalo ndio bora[2].

Ama kuhusu kuswali tano na tatu na kukaa baina ya kila Rak´ah mbili bila ya kutoa Tasliym, ni kitu sikupata kuwa kimethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Asili ni kuwa inajuzu, lakini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuwitiri kwa Rak´ah tatu na akatoa sababu ya hilo kwa kusema:

“Isifananishwe na Swalah ya Maghrib.”[3]

Kwa hiyo ni wajibu kwa yule anayetaka kuswali Witr Rak´ah tatu aepuke mfanano huu. Hili linakuwa kwa njia mbili:

Ya kwanza: Tasliym kati ya ile isiyokuwa Witr na Witr na hii ndio yenye nguvu na bora zaidi.

Ya pili: Mtu asikae kati ya ile isiyokuwa Witr na Witr na Allaah (Ta´ala) ndiye mjuzi zaidi.

 [1] Ameipokea at-Twahaawiy, al-Haakim na wengineo. Hadiyth ina mlolongo wa wapokezi Swahiyh kama walivyosema maimamu wengi. Ina Hadiyth nyingine mfano wake ilio na nyongeza ambayo ni munkari, kama nilivyobainisha katika “Swalaat-ut-Taraawiyh”, uk. 99-100

[2] Faida muhimu! Ibn Khuzaymah amesema katika “as-Swahiyh” yake (02/194) baada ya kutaja Hadiyth ya ´Aaishah na nyenginezo juu ya hizo namna zilizotajwa: “Inajuzu kwa mtu kuswali idadi yoyote ya swalah anayotaka katika yale yaliyopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Haya yanaafikiana na maoni yetu ya kwamba mtu ashikamane na ile idadi iliyosihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mtu asizidishe juu yake. Himdi zote zinamstahikia Allaah kwa mafanikio Yake na ninamuomba ziada katika fadhila Zake.

[3] at-Twahaawiy, ad-Daaraqutwniy na wengineo. Tazama “at-Taraawiyh”, uk. 99-100.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qiyaam Ramadhwaan, uk. 27-30
  • Imechapishwa: 07/05/2019