Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Siku ya Qiyaamah watu watapewa madaftari yao ndani kukiwa na matendo yao.

MAELEZO

Miongoni mwa mambo yatayokuweko siku ya Qiyaamah ni watu kukabidhiwa madaftari yao ya matendo. Kwani Malaika huandika matendo yetu. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ

“Pale wanapopokea wapokeaji wawili wanaokaa kuliani na kushotoni. Hatamki maneno yoyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha [kurekodi].”[1]

Wanaandika kila tunachokifanya au kukisema ndani ya madaftari ambayo tutakabidhiwa nayo siku ya Qiyaamah. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَكُلَّ إِنسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَائِرَهُ فِي عُنُقِهِ ۖ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنشُورًا اقْرَأْ كِتَابَكَ كَفَىٰ بِنَفْسِكَ الْيَوْمَ عَلَيْكَ حَسِيبًا

“Kila mtu Tumemfungia matendo yake shingoni mwake na tutamtolea Siku ya Qiyaamah kitabu akutane nacho hali ya kuwa kimekunjuliwa. [Ataambiwa]: “Soma kitabu chako nafsi yako inakutosheleza leo kukuhesabu.””[2]

Kila mmoja, ni mamoja alikuwa anajua kusoma au hajui kusoma duniani, atasoma daftari lake ili apate kujua matendo na malipo yake. Miongoni mwao wako ambao watakirimiwa na kufurahishwa kwa kupewa madaftari yao kwa mkono wa kuume. Wengine watakabidhiwa vitabu vyao kwa mkono wa kushoto na wahuzunike. Amesema (Ta´ala):

فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَيَقُولُ هَاؤُمُ اقْرَءُوا كِتَابِيَهْ إِنِّي ظَنَنتُ أَنِّي مُلَاقٍ حِسَابِيَهْ فَهُوَ فِي عِيشَةٍ رَّاضِيَةٍ فِي جَنَّةٍ عَالِيَةٍ قُطُوفُهَا دَانِيَةٌ كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا أَسْلَفْتُمْ فِي الْأَيَّامِ الْخَالِيَةِ

“Basi ama yule atakayepewa kitabu chake kuliani mwake, atasema: “Hebu chukueni someni kitabu changu. Hakika mimi niliyakinisha kwamba ni mwenye kukutana na hesabu yangu!” Hivyo basi, yeye atakuwa katika maisha ya kuridhisha, kwenye Jannah ya juu, matunda yake ya kuchumwa ni karibu. [Wataambiwa]: “Kuleni na kunyweni hali ya kufurahi kwa yale mliyoyatanguliza katika siku nyingi zilopita.””[3]

Atafurahi kwelikweli, kwa sababu alikuwa na yakini kwamba atakutana na hesabu yake na hivyo akafanya matendo mema. Kuhusu ambaye atapewa kitabu chake kwa mkono wa kushoto, Allaah (Ta´ala) anasema:

وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِشِمَالِهِ فَيَقُولُ يَا لَيْتَنِي لَمْ أُوتَ كِتَابِيَهْ وَلَمْ أَدْرِ مَا حِسَابِيَهْ يَا لَيْتَهَا كَانَتِ الْقَاضِيَةَ مَا أَغْنَىٰ عَنِّي مَالِيَهْ ۜ هَلَكَ عَنِّي سُلْطَانِيَهْ

“Ama yule atakayepewa kitabu chake kushotoni mwake, atasema: “Ee! Laiti nisingepewa kitabu changu na wala nisingelijua hesabu yangu! Ee! Laiti kingelikuwa kifo ndio kumalizika kwangu. Haikunifaa chochote mali yangu. Madaraka yangu yameniondoka.”[4]

Atatamani laiti asingelipewa daftari lake kwa sababu linamfedhehesha na limebeba mambo maovu. Atatamani laiti asingekuwa amefufuliwa na angekufa na kutokomea moja kwa moja kabisa. Atahuzunika na huku Allaah (Jalla wa ´Alaa) awaambie Malaika Wake:

خُذُوهُ فَغُلُّوهُ ثُمَّ الْجَحِيمَ صَلُّوهُ

“Mchukueni, na mfungeni pingu, kisha kwenye moto uwakao vikali mno mwingizeni achomeke.”[5]

Hali za siku ya Qiyaamah ni ngumu na za kutisha, lakini waumini watakuwa katika amani:

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي ظِلَالٍ وَعُيُونٍ وَفَوَاكِهَ مِمَّا يَشْتَهُونَ كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

“Hakika wale wenye kumcha Allaah wamo katika vivuli na chemchemu na matunda katika yale wanayoyatamani. [Wataambiwa]: “Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyatenda.””[6]

[1] 50:17-18

[2] 17:13-14

[3] 69:19-24

[4] 69:25-29

[5] 69:30-31

[6] 77:41-43

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 67-68
  • Imechapishwa: 23/08/2021