Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika Hadiyth:

“Kichwa cha mambo ni Uislamu, nguzo yake ni swalah na jihaad katika njia ya Allaah ndio nundu yake ya juu.”[1]

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) anachokusudia kwa Hadiyth hii ni kuonesha kuwa kila kitu kina kichwa cha mambo. Kichwa cha mambo alichokuja nacho Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Uislamu.

… nguzo yake ni swalah – Kwa sababu Uislamu hausimami isipokuwa kwayo. Kwa ajili hii maoni yenye nguvu ni kwamba yule mwenye kuacha swalah ni kafiri na hana Uislamu wowote.

Jihaad katika njia ya Allaah ndio nundu yake ya juu – Bi maana mambo yake ya juu na kamilifu zaidi ni kupambana jihaad katika njia ya Allaah. Hili ni kutokana na kwamba yule mwenye kuitengeneza nafsi yake ajaribu pia kuwatengeneza wengine kupitia jihaad katika njia ya Allaah. Hili hufanywa ili Uislamu uweze kusimamishwa na ili neno la Allaah liweze kuwa juu. Yule mwenye kupambana ili neno la Allaah liweze kuwa juu, basi huyo ndiye mwenye kupambana katika njia ya Allaah. Kwa hivyo ndio hufikiwa nundu hii ya juu kwa sababu ni kupitia yenyewe ndio Uislamu unakuwa juu ya dini nyinginezo.

[1] Ahmad (5/231-237), at-Tirmidhiy (5/13) na Ibn Maajah (2/1394).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 160
  • Imechapishwa: 05/06/2020