87. Usijaribu kuifahamu Qur-aan bila kuitegemea Sunnah

Miongoni mwa mambo yenye kushangaza sana hii leo na vurugu za kisomi ni kwamba utaona baadhi ya watu, mmoja wao ni yule aitwaye Is´aaf an-Nashaashiybiy katika kitabu “al-Islaam as-Swahiyh”, wanathubutu kupinga kuwasifu jamaa zake Mtume wakati wa kumsifu yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haya pamoja na kuwa kitendo hichi kimepokelewa ikiwa ni pamoja vilevile na al-Bukhaariy na Muslim kupitia Maswahabah wengi akiwemo Ka´b bin ´Ujrah, Abu Humayd as-Sa´diy, Abu Sa´iyd al-Khudriy, Abu Mas´uud al-Answaariy, Abu Hurayrah na Twalhah bin ´Ubaydillaah. Walipomuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni vipi watamsifu, ndipo akawafunza jumla hizi. Hoja yake ni kwamba Aayah inayosema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Enyi walioamini msifuni na msalimieni kwa mamkizi yaliyojaa amani.”[1]

Allaah hakumtaja mwingine zaidi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Matokeo yake akapinga kwa ukali kabisa kwamba eti Swahabah anaweza kuuliza swali kama hili kwa sababu namna ya kusifu kulikuwa kunatambulika maana yake, nako ni du´aa; ni vipi basi watauliza swali kama hili?

Huu ni upotevu wa wazi. Kwani wao hawakuuliza kuhusu maana ya kumsifu, isipokuwa walichouliza ni namna yake. Kwa ajili hiyo hakuna ajabu yoyote. Walichomuuliza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni namna ya kumsifu iliyowekwa katika Shari´ah ambayo inaweza kutambulika kupitia kwa Mwingi wa hekima na mjuzi wa kila jambo Mwekaji Shari´ah. Ni kama ambavo wangemuuliza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu namna ya utekelezaji wa swalah iliyowajibishwa wakati Allaah (Ta´ala) alipoamrisha:

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ

“Simamisheni swalah.”[2]

Kwa sababu tu ya kwamba wanajua maana ya swalah katika lugha haikuwafanya kutokuwa na haja ya kuuliza kuhusu namna ya utekelezaji wake. Hili ni jambo liko wazi.

Ama kuhusu hoja yake, haina kitu chochote. Ni jambo linalojulikana kwa waislamu kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mwenye kufasiri maneno ya Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ

“Tumekuteremshia Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amebainisha ni vipi atasifiwa na akawataja jamaa. Kwa ajili hiyo ni wajibu kuyakubali hayo kutokana na maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

“Kile alichokupeni Mtume basi kichukueni na kile alichokukatazeni basi acheni.”[4]

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh na yenye kujulikana:

“Hakika mimi nimepewa Qur-aan na mfano wake pamoja.”

Imetajwa katika “al-Mishkaah”[5].

Mimi najiuliza an-Nashaashiybiy na wale wote walioghurika na maneno yake yaliyopambwapambwa watasema nini kuhusu mtu ambaye anapinga Tashahhud ndani ya swalah au anapinga mwanamke mwenye hedhi kuacha kwake kuswali na kufunga. Kwani Allaah (Ta´ala) hakutaja Tashahhud ndani ya Qur-aan. Kitu pekee kilichotajwa humo ni kusimama, Rukuu´ na Sujuud. Vilevile Allaah (Ta´ala) hakutaja ndani ya Qur-aan kwamba mwanamke mwenye hedhi haimlazimu kwake kuswali wala kufunga. Hivyo ni lazima kwake kuswali na kufunga. Watakubaliana na mtu mwenye kuyapinga hayo au watamkemea? Ikiwa watakubaliana naye – jambo ambalo sitegemei – basi watakuwa wamepotea upotevu wa mbali kabisa na wametoka nje ya mkusanyiko wa waislamu. Na ikiwa watampinga, basi wamepatia. Vile watakavyokemea mtu mwenye kuyapinga hayo basi ndivo tunavyomkemea an-Nashaashiybiy.

Kwa hivyo tahadhari, ee muislamu, kujaribu kuielewa Qur-aan pasi na kuitegemea Sunnah. Hutoweza kufanya hivo japokuwa utakuwa ni Siybuuyah wa wakati wako. Hapa mbele yako uko na mfano. an-Nashaashiybiy alikuwa ni mmoja katika wanazuoni wakubwa wa lugha wa wakati wa sasa. Wewe mwenyewe unaona namna alivyopondoka pindi alipodanganyika na elimu yake ya lugha na hakutaka kutegemea msaada wa Sunnah katika kuifahamu Qur-aan. Bali hata hiyo Sunnah anaipinga. Nina mifano mingi kwa hili ninalolizungumzia, lakini hakuna nafasi ya kuitaja. Yanatosha yale niliyoyataja na Allaah ndiye Mwenye kuwafikisha.

[1] 33:56

[2] 02:43

[3] 16:44

[4] 59:07

[5] 163 na 4247.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 148-149
  • Imechapishwa: 03/01/2019