87. Twawaaghiyt wakubwa watano


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Twawaaghiyt ni wengi. Wakubwa wao ni watano:

  1. Ibliys, Allaah amlaani.
  2. Yule mwenye kuabudiwa hali ya kuwa yuko radhi kwa hilo.
  3. Yule mwenye kuwaita watu katika kumwabudu.
  4. Yule mwenye kudai kujua kitu katika elimu ya ghaibu.
  5. Yule asiyehukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah.

MAELEZO

Twawaaghiyt – Ni wingi wa “Twaaghuut” na tafsiri yake imekwishatangulia.

Wakubwa wao ni watano – Bi maana viongozi wao ni watano.

Ibliys – Ibliys ni yule shaytwaan aliyewekwa mbali na rehema za Allaah na kulaaniwa ambaye Allaah amesema juu yake:

وَإِنَّ عَلَيْكَ لَعْنَتِي إِلَىٰ يَوْمِ الدِّينِ

“Na hakika laana Yangu iko juu yako mpaka siku ya malipo!” (Swaad 38 : 78)

Hapo kabla Ibliys alikuwa pamoja na Malaika na akifanya yale wanayoyafanya. Lakini pale ambapo alipoamrishwa kumsujudia Aadam, ndipo kulipodhihirika kutoka kwake uovu, kukataa na kiburi. Hivyo akawa amekataa, akafanya kiburi, na hivyo akawa ni miongoni mwa makafiri. Akafukuzwa mbali na rehema za Allaah (´Azza wa Jall). Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ وَاسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ

”Na pinid Tulipowaambia Malaika: “Msujudieni Aadam” wakasujudu isipokuwa Ibliys alikataa na akatakabari na akawa miongoni mwa makafiri.” (al-Baqarah 02 : 34)

Yule mwenye kuabudiwa hali ya kuwa yuko radhi kwa hilo – Bi maana akaabudiwa badala ya Allaah hali ya kuwa yuko radhi kwa hilo. Mtu kama huyu atakuwa ni katika viongozi wa Twawaaghiyt – na tunamuomba Allaah atulinde. Ni mamoja ikiwa mtu huyu ataabudiwa wakati wa uhai wake au baada ya kufa kwake na akiridhia hilo.

Yule mwenye kuwaita watu katika kumwabudu – Yule mwenye kuwaita watu katika kumwabudu yeye hata kama hawatomwabudu. Mtu huyu ni katika viongozi wa Twawaaghiyt. Ni mamoja ikiwa atakubaliwa au asiitikiwe wito wake.

Yule mwenye kudai kujua kitu katika elimu ya ghaibu – Ghaibu ni kile kitu kimefichikamana kwa mtu. Kuna aina mbili:

1- Ya sasa. Ya sasa inatofautiana kutoka kwa mtu na kwenda kwa mwingine. Baadhi ya watu wanaijua na wengine wakawa hawaijui.

2- Huko mbele. Aina hii hakuna yeyote anayeijua isipokuwa Allaah pekee au Mitume ambao amewajulisha nayo. Yule mwenye kudai kuijua ghaibu hii ni kafiri kwa sababu amemkadhibisha Allaah (´Azza wa Jall) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema:

قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّـهُ ۚ وَمَا يَشْعُرُونَ أَيَّانَ يُبْعَثُونَ

“Sema: “Hakuna katika mbingu na ardhi ajuaye yaliyofichikana isipokuwa Allaah na wala hawajui lini watafufuliwa.” (an-Naml 27 : 65)

Allaah (´Azza wa Jall) amemwamrisha Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwatangazia watu ya kwamba hakuna yeyote aliyeko mbinguni wala ardhini anayeijua ghaibu isipokuwa Allaah. Hii ina maana kwamba yule mwenye kudai kujua elimu ya ghaibu basi amemkadhibisha Allaah (´Azza wa Jall) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Vipi mtaweza kujua ghaibu hali ya kuwa Mtume mwenyewe (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hajui ghaibu? Je, nyinyi ni watukufu kuliko Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Wakisema kuwa wao ni watukufu kuliko Mtume, wamekufuru. Na wakisema kuwa yeye ndio mtukufu, tunawauliza:

“Kwa nini yeye hakuijua ghaibu na nyinyi mkawa mnaijua?”

Allaah (´Azza wa Jalla) amesema:

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا لَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِن رَّسُولٍ فَإِنَّهُ يَسْلُكُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ رَصَدًا

“Mjuzi wa ghaibu na wala hamdhihirishii ghaibu Yake yeyote, isipokuwa yule aliyemridhia miongoni mwa Mitume, basi hakika Yeye anamwekea mlinzi mbele yake na nyuma yake.” (al-Jinn 72 : 26-27)

Hii ni Aayah ya pili inayojulisha kuwa mwenye kusema kuwa anajua elimu ya ghaibu ni kafiri. Allaah (Ta´ala) amemwamrisha Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kusema kuwaambia watu:

قُل لَّا أَقُولُ لَكُمْ عِندِي خَزَائِنُ اللَّـهِ وَلَا أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلَا أَقُولُ لَكُمْ إِنِّي مَلَكٌ ۖ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ

“Sema: “Sikuambieni kuwa mimi nina hazina ya Allaah; na kwamba najua ghaibu na wala sikuambieni kuwa mimi ni Malaika. Si vyenginevyo sifuati isipokuwa yale niloletewa Wahy.”” (al-An´aam 06 : 50)

Yule asiyehukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah – Kuhukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah (Ta´ala) ni katika Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Kwa sababu inahusiana na kuitekeleza hukumu ya Allaah, jambo ambalo linapelekea katika uola Wake na ukamilifu wa ufalme Wake na uendeshaji Wake. Kwa ajili hii Allaah (Ta´ala) amewaita wale wenye kufuatwa katika mambo mengine yasiyokuwa yale aliyoteremsha Allaah “miungu” ya wale wenye kuwafuata. Amesema (Ta´ala):

اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَـٰهًا وَاحِدًاۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ

“Wamewafanya marabi na watawa  wao kuwa ni miungu badala ya Allaah na al-Masiyh mwana wa Maryam, na hali hawakuamrishwa isipokuwa kumwabudu Mungu Mmoja pekee – hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye; utakasifu ni Wake kutokamana na yale yote wanayomshirkisha nayo!” (at-Tawbah 09 : 31)

Allaah amewaita wale wenye kufuatwa “miungu” kwa sababu wamewafanya wao ni wenye kuweka Shari´ah pamoja na Allaah (Ta´ala). Vilevile amewaita wenye kufuata “waja” kwa sababu wamewanyenyekea na wakawatii katika yale yanayoenda kinyume na hukumu ya Allaah (Subhanaahu wa Ta´ala). ´Adiyy bin Haatim alisema kumwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hawakuwaabudu.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ndio. Waliwaharamishia ya halali na kuwahalalishia ya haramu. Wakawafuata. Hivyo ndivyo walivyowaabudu.”[1]

Utakapofahamu hayo, basi jua ya kwamba kuna Aayah zinazokanusha imani ya yule asiyehukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah na badala yake anataka mtu mwengine asiyekuwa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wahukumu. Vilevile kuna Aayah zinazohukumu  juu ya ukafiri, dhuluma na ufuska wa mtu huyu.

Kigawanyo cha kwanza: Amesema (Ta´ala):

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يَزْعُمُونَ أَنَّهُمْ آمَنُوا بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ يُرِيدُونَ أَن يَتَحَاكَمُوا إِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُوا أَن يَكْفُرُوا بِهِ وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُضِلَّهُمْ ضَلَالًا بَعِيدًا وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا إِلَىٰ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ وَإِلَى الرَّسُولِ رَأَيْتَ الْمُنَافِقِينَ يَصُدُّونَ عَنكَ صُدُودًا فَكَيْفَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ ثُمَّ جَاءُوكَ يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ إِنْ أَرَدْنَا إِلَّا إِحْسَانًا وَتَوْفِيقًا أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَعْلَمُ اللَّـهُ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ وَعِظْهُمْ وَقُل لَّهُمْ فِي أَنفُسِهِمْ قَوْلًا بَلِيغًا وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذ ظَّلَمُوا أَنفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّـهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّـهَ تَوَّابًا رَّحِيمًا فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Je, huoni wale ambao wanadai kwamba wao wameamini yaliyoteremshwa kwako na yale yaliyoteremshwa kabla yako, wanataka wahukumiane kwa Twaaghuut na hali wameamrishwa wakanushe hiyo, na shaytwaan anataka awapoteze upotofu wa mbali kabisa. Na wanapoambiwa: “Njooni katika yale aliyoyateremsha Allaah na kwa Mtume, basi utawaona wanafiki wanakugeuka kukugeukia. Basi itakuwaje utakapowafika msiba kwa sababu ya yale iliyotanguliza mikono yao kisha wakakujia wakiapa: “Hatukutaka jengine isipokuwa wema na mapatano.” Hao ndio ambao Allaah anayajua yaliyomo ndani ya nyoyo zao. Hivyo basi jitenge nao mbali na wape mawaidha na uwaambie maneno yatakayowaathiri na kuingia katika nafsi zao. Na hatukutuma Mtume yeyote isipokuwa atiiwe kwa idhini ya Allaah. Na lau wao pale walipojidhulumu nafsi zao wangelikujia wakamwomba Allaah msamaha na Mtume akawaombea msamaha, basi wangelimkuta Allaah Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. Naapa kwa Mola wako! Hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni hakimu katika yale wanayozozana kati yao kisha wasipate katika nyoyo zao uzito katika yale uliyohukumu na wajisalimishe kwa kujisalimisha.” (an-Nisaa´ 04 : 60-65)

Allaah (Ta´ala) amewasifu watu hawa wanaodai kuwa wanaamini, hali ya kuwa ni wanafiki, kwa sifa zifuatazo:

1- Wanataka Twaaghuut ndio ihukumu na Twaaghuut ni kila kile kinachoenda kinyume na hukumu ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kila kinachoenda kinyume na hukumu ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kupindukia na mashambulizi juu ya Yule mwenye hukumu na ambaye mambo yote yanarejea Kwake, Naye ni Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Zindukeni! Ni Vyake pekee uumbaji na amri. Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu.” (al-A´raaf 07 : 54)

2- Wanapoitwa katika yale aliyoteremsha Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi hugeuka na kupinga kikamilifu.

3- Wanapopatwa na msiba kutokana na yale yaliyochumwa na mikono yao, basi huapa kwamba hawakukusudia isipokuwa wema na upatanishi. Mfano wa hao ni kama wale wanaopinga leo hukumu za Kiislamu na badala yake wanahukumiana kwa sheria zilizotungwa na watu. Wanadai kuwa hawakukusudia jengine isipokuwa wema na kwamba ni jambo ambalo linaendana na hali ya sasa.

Kisha akatahadharisha (Subhanaah) watu hawa ambao wanadai kuwa ni waumini hali ya kuwa wanasifika kwa sifa kama hizi. Yeye (Subhaanah) anajua yale yaliyomo mioyoni mwao na yale wanayoyaficha, mambo yanayoenda kinyume na yale wanayoyasema. Akamwamrisha Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awape mawaidha na awaambie maneno yatakayowaathiri na kuingia katika nafsi zao. Halafu akabainisha hekima ya kutumwa Mtume, nayo ni kwamba yeye – na si mtu mwengine – ndiye anatakiwa kutiiwa na kufuatwa, pasi na kujali ni nadharia yenye nguvu iliyoje walionayo na ufahamu wao mpana walionao. Kisha akaapa (Ta´ala) kwa uola Wake juu ya Mtume Wake, jambo ambalo ni katika aina maalum ya uola na inayoashiria ukweli wa ujumbe wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ameapa kuwa imani ya mtu haisihi isipokuwa kwa kutimia sharti tatu:

1- Kurejea kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kila ugomvi wa kitu.

2- Mtu akunjue kifua chake juu ya hukumu yake na baada ya hapo kusipatikane pingamizi yoyote dhidi yake.

3- Mtu akubali hukumu hii na ajisalimishe kwayo kikamilifu na kuitekeleza bila ya kuirudisha.

Kigawanyo cha pili: Amesema (Ta´ala):

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ

“Na yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio makafiri.” (al-Maaidah 05 : 44)

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ

“Na yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio madhalimu.” (al-Maaidah 05 : 45)

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ

“Na yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio mafasiki.” (al-Maaidah 05 : 47)

Je, sifa zote hizi tatu zinamuhusu mtu mmoja? Kila asiyehukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah ni kafiri, dhalimu na fasiki? Hakika ya (Ta´ala) amesema:

وَالْكَافِرُونَ هُمُ الظَّالِمُونَ

“Makafiri wao ndio madhalimu.” (al-Baqarah 02 : 254)

إِنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَمَاتُوا وَهُمْ فَاسِقُو

“Hakika wao wamemkanusha Allaah na Mtume Wake na wakafa hali wao ni mafasiki.” (at-Tawbah 09 : 84)

Kila kafiri ni dhalimu na ni fasiki.

Au sifa hizi zinamuhusu mwenye kusifika nazo kutegemea ni kwa sababu gani iliyompelekea yeye kuhukumu kinyume na aliyoteremsha Allaah? Haya ndio ninayoonelea mimi kuwa yako karibu na haki – na Allaah ndiye anajua zaidi.

Yule asiyehukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah kwa sababu anayadharau au kwa sababu anaonelea hukumu zingine ni bora zaidi na zinaendana na viumbe au zinalingana nayo, basi ni kafiri na ameritadi. Miongoni mwa watu hawa kunaingia pia wale wenye kuwatungia watu kanuni na katiba zinazoenda kinyume na Shari´ah ya Kiislamu. Wamefanya hivi ili iwe ni mfumo utakaofuatwa na watu. Hawakufanya hivyo isipokuwa ni kwa sababu wanaitakidi kuwa sheria zao ndio bora zaidi na zinazoendana na viumbe. Ni jambo linalojulikana kilazima kwa akili na kimaumbile ya kwamba mtu haachi mfumo na kwenda katika mwingine isipokuwa ni kwa sababu anaonelea kuwa ule aliyobadilisha ndio bora zaidi.

Yule asiyehukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah, pasi na kuyadharau na kuonelea kuwa hukumu zingine ndio bora zaidi kuliko yenyewe au mfano wa hayo, huyu ni dhalimu na sio kafiri. Dhuluma zake zinatofautiana kihukumu na njia zake. Dhuluma yake inatofautiana kutokana na hukumu yenyewe na njia zake.

Yule asiyehukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah, pasi na kuyadharau, kuyapunguza, kuonelea kuwa hukumu zingine ndio bora na zenye manufaa zaidi juu ya viumbe na zinalingana nayo na kadhalika, lakini amefanya hivo kwa sababu ya kumpendelea yule anayemuhukumu, rushwa au mengineyo katika mambo ya kidunia, basi huyu ni fasiki na sio kafiri. Dhambi yake inatofautiana kutokana na hukumu yenyewe na njia zake.

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema kuwa wale waliowafanya wanachuoni wao na watawala badala ya Allaah wamegawanyika katika makundi mawili:

1- Wanajua kuwa wameibadilisha dini ya Allaah. Pamoja na hivyo wakawafuata katika mabadilisho haya na kuonelea ya haramu kuwa halali na ya halali kuwa haramu. Wanawafuata viongozi wao pamoja na kwamba wanajua kuwa wanaenda kinyume na dini ya Mtume. Hii ni kufuru na inazingatiwa amemshirikisha Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

2- Wanaonelea ya haramu kuwa halali na ya halali kuwa haramu – namna hii ndivyo maelezo yalivyonakiliwa kutoka kwake – lakini wakawatii katika maasi. Hili ni kama wale waislamu ambao wanafanya maasi na huku wanaonelea kuwa ni maasi. Watu hawa na watu mfano wao wanazingatiwa kuwa ni watenda madhambi.

Hata hivyo kuna tofauti kati ya hukumu iliyoenea na kutohukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah katika suala fulani. Kwa sababu hukumu ya iliyoenea inaingia tu katika kile kigawanyo cha kwanza. Kwani aina ya hukumu hii inayoenda kinyume na Uislamu imetungwa kwa sababu tu ameonelea kuwa ni bora na inawafaa watu zaidi kuliko Uislamu.

Suala hili kuhusu kuhukumu kinyume na aliyoteremsha Allaah ni katika mambo makubwa. Viongozi wengi wa leo wamepewa mtihani kwa jambo hilo. Hivyo basi, mtu asiwe na haraka ya kuwahukumu kwa kitu wasichostahiki mpaka pale watakapobainishiwa haki. Suala hili ni khatari. Tunamuomba Allaah (Ta´ala) azintengeneze hali za waislamu, watawala wao na nchi zao.

Vilevile ni wajibu kwa wale watu ambao Allaah amewapa elimu kuwabainishia watawala hawa haki ili wasiwe na udhuru wowote. Yule atayekufa, basi awe amekufa juu ya dalili, na yule atakayeishi, basi awe ameishi juu ya dalili. Mtu asijidogeshe na kumuogopa yeyote. Kwani hakika ya utukufu ni wa Allaah, Mtume Wake na waumini.

[1] at-Tirmidhiy (5/262).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 152-159
  • Imechapishwa: 04/06/2020