87. Ndio maana mafusaki wanayapenda madhehebu ya Murji-ah


Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

35- Usiwe Murjiy anayecheza na dini yake

     hakika Murjiy kweli anacheza na dini yake

36- Sema kuwa imani ni maneno na nia

     na kitendo kutokana na [ushahidi wa] maneno ya Mtume yaliyo wazi

37- Inapungua kwa maasi wakati fulani, na wakati mwingine

     inaongezeka kwa utiifu na inakuwa na uzito kwenye mizani

MAELEZO

Murji-ah ndio kundi la pili linalokabiliana na Khawaarij. Wameitwa “Murji-ah” kutokamana na neno “Irjaa´” ambalo maana yake ni kuchelewesha. Kwa kuwa wao wamechelewesha matendo katika imani na wakasema kuwa matendo hayaingii katika imani. Wao wanaonelea kuwa iwapo mtu ataamini kwa moyo wake lakini asifanye kitu; asiswali, asitoe zakaah, asifanye maamrisho na kujiepusha na mambo ya haramu ni muumini mwenye imani kamilifu. Haya ni madhehebu batili yanayokana matendo kabisa.

Usiwe Murjiy anayecheza na dini yake – Kwa sababu madhehebu ya Murji-ah ni kucheza na dini. Wanaona kuwa mja anakuwa muumini hata kama hakufanya kitu; hata kama ataacha swalah, ataacha kufunga, ataacha kutoa zakaah, kuhiji hata kama hatofanya kitu katika maisha yake yote. Sivyo tu bali hata kama atafanya ya haramu yote. Haya ni madhehebu batili. Kwa ajili hii watenda madhambi na maasi wanafurahi kwa madhehebu haya na kuyasapoti. Kwa sababu yanaendana nao kwa njia ya kwamba wanapata kufanya wanachokitaka na wakati huo huo bado wako na imani zao kwa mujibu wa Murji-ah. Wanaofuata hawaa, matamanio na maasi wanafurahi kwa madhehebu haya. Ni madhehebu yamejengwa juu ya kucheza na dini.

hakika Murjiy kweli anacheza na dini yakeBi maana Murji-ah wanacheza na dini na wanayaharibu maamrisho na makatazo. Kujengea juu ya madhehebu yao wanaonelea kuwa hakuna haja ya maamrisho na makatazo. Huku ni kucheza na dini ya Allaah (´Azza wa Jall).