86. Tahadhari na maoni ya Khawaarij yatakuangamiza


Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

34- Usiitakidi maoni ya Khawaarij kwani hakika

    ni maoni ya mwenye kupenda yanayomwangamiza na kumfedhehi

MAELEZO

Khawaarij ni pote miongoni mwa mapote potevu. Wameitwa Khawaarij kwa sababu walijivua kutoka katika utiifu wa watawala. Wa kwanza ambaye walimfanyia uasi ni ´Aliy bin Abiy Twaalib (Raadhiya Allaahu ´anh) katia kipindi cha uongozi wake na wakasema ni kwa nini amewafanya wanaume kuhukumu ilihali Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّـهِ

“Hakuna hukumu isipokuwa ya Allaah.”? (12:40)

Kwa ajili hiyo pindi ´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alipojadiliana nao wakamletea utata huu ya kwamba amewatumia wanaume katika hukumu. Akawajibu kwa kuwaambia kwamba Allaah si Yeye ndiye ambaye amehukumu kwa kutumia wanaume pindi muhrim atapomuua mnyama pale aliposema:

يَحْكُمُ بِهِ ذَوَا عَدْلٍ مِّنكُمْ هَدْيًا بَالِغَ الْكَعْبَةِ

“Ahukumu kwacho watu wawili walio waadilifu miongoni mwenu. Mnyama huyo afikishwe Ka’bah [kuchinjwa]? (05:95)

Kadhalika amehukumu kwa kutumia wanaume katika masuala yanayohusiana na uasi pale aliposema (Ta´ala):

وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُوا حَكَمًا مِّنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِّنْ أَهْلِهَا إِن يُرِيدَا إِصْلَاحًا يُوَفِّقِ اللَّـهُ بَيْنَهُمَا

“Mkikhofu kutengana baina yao [mke na mume], basi pelekeni mwamuzi kutoka watu wake mume na mwamuzi kutoka watu wake mke. Wakitaka sulhu, basi Allaah atawawafikisha baina yao.”? (04:35)

Amehukumu kwa kutumia wanaume. ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) kuhukumu kwa kutumia wanaume inahusiana na sura kama hii.

ni maoni ya mwenye kupendaBi maana anayapenda na kuyafuata.

… yanayomwangamiza – Yanamwangamiza yule mwenye kushikamana nayo. Kwa sababu ni maoni ya khatari yanayowakufurisha waislamu, kuhalalisha damu na mali zao na kuwafanyia uasi watawala.

Madhehebu ya Khawaarij ni yenye kutoa matawi mabaya. Kwa hivyo usiyaitakidi au ukamili kwayo. Unachotakiwa ni wewe kuyazingatia kuwa ni madhehebu batili. Hili linahusiana na yule ambaye anaonelea maoni yao hata kama hakufanya matendo wanayofanya wao. Vipi kuhusu yule ambaye anaonelea maoni yao na kuyatendea kazi?