84. Kazi kubwa ya Mitume


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Kikubwa ambacho Mitume walilingania kwacho, kuanzia wa mwanzo wao Nuuh (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) mpaka wa mwisho wao Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ilikuwa ni Tawhiyd. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ

“Kwa hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah.” (an-Nahl 16 : 36)

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mungu wa haki isipokuwa Mimi – hivyo basi Niabuduni.” (al-Anbiyaa´ 21 : 25)

Wa mwanzo wao alikuwa ni Nuuh (´alayhis-Salaam) na wa mwisho wao alikuwa ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Dalili juu ya kwamba wa mwanzo wao alikuwa ni Nuuh (´alayhis-Salaam) ni
maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ

“Hakika Tumekufunulia Wahy kama tumevyomfunulia Wahy Nuuh na Manabii baada yake.” (an-Nisaa´ 04 : 163)

MAELEZO

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amebainisha kuwa Mtume wa kwanza alikuwa ni Nuuh (´alayhis-Swalaatu was-Salaam). Ametumia dalili juu ya hilo kwa maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ

“Hakika Tumekufunulia Wahy kama tumevyomfunulia Wahy Nuuh na Manabii baada yake.” (an-Nisaa´ 04 : 163)

Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kwenye Hadiyth ya uombezi:

“Watu watamwendea Nuuh na kumwambia: “Wewe ndite Mtume wa kwanza ambaye Allaah alikutuma katika ardhi.”[1]

Nuuh ndio Mtume wa kwanza. Kutokana na haya tunapata kujua kosa la baadhi ya wanahistoria ambao wamesema kuwa Idriys (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) alikuwa kabla ya Nuuh. Lililo la dhahiri ni kwamba Idriys alikuwa ni miongoni mwa Mitume wa wana wa israaiyl.

Mtume wa mwisho alikuwa ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا

“Hakuwa Muhammad baba wa mmoja yeyote miongoni mwa wanamme wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii. Na Allaah daima kwa kila jambo ni mjuzi.” (al-Ahzaab 33 : 40)

Hakuna Nabii mwingine baada yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yule mwenye kudai utume baada yake ni mwongo, kafiri na ni mwenye kuritadi kutoka nje ya Uislamu.

[1] al-Bukhaariy (7510) na Muslim (193).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 149-150
  • Imechapishwa: 04/06/2020