84. al-´Ayyaashiy upotoshaji wa tatu wa an-Nisaa´

al-´Ayyaash amesema kuhusu Aayah:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa Amtakae; yeyote atakayemshirikisha Allaah, basi hakika amezua dhambi kuu.”[1]

“Bi maana hawasamehi wale wenye kupinga uongozi wa ´Aliy. Ama kuhusu maana ya:

وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“… na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa Amtakae.”

inamaanisha wale waliosimama upande wa ´Aliy.”[2]

Shirki ni kumuabudu mungu mwengine asiyekuwa Allaah kama katika du´aa, kichinjwa, Rukuu´, Sujuud, matarajio, kuogopa na kutegemea. Mwenye kufanya kitu katika ´ibaadah za Allaah kumfanyia mwengine asiyekuwa Allaah basi amemshirikisha Allaah. Haya ndio makusudio ya Aayah. Huu ndio ujumbe uliofikishwa na Mitume wote ambao ni kupambana na shirki. Hii ndio shirki inayomsababishia mwenye nayo kudumishwa Motoni milele na kutosamehewa. Aayah haina uhusiano wowote kabisa na uongozi.

Mazanadiki na Baatwiniyyah wanakuja kupotosha Aayah na makusudio yake ili waweze kuwapotosha wafuasi wao. Upotoshaji huu mchafu unapelekea kuporomosha haki kubwa ya Allaah (Tawhiyd ya kweli). Ni makengeusho mangapi ya jinai walionayo ambayo yanaangusha haki kubwa za Allaah, Mitume wake na waumini!  Malengo yao kwa hayo ni ule mtazamo wao mbaya walionao juu ya familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 04:48

[2] Tafsiyr al-´Ayyaashiy (1/245).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Intiswaar li Kitaab-il-´Aziyz al-Jabbaar, uk. 126-127
  • Imechapishwa: 07/11/2017