83. ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kuhusu uombezi


Amesema mwandishi (Rahimahu Allaah):

Hakika Mtume wa Allaah ana uombezi juu ya watu wazi

Uombezi uliothibitishwa umegawanyika aina mbili:

Aina ya kwanza: Kuna uombezi ambao ni maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Uombezi wa kwanza  ni ule uombezi mkubwa. Atawaombea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) viumbe uombezi mkubwa pale ambapo watu watakuwa wamekusanyiwa na kusimamishwa kisimamo kirefu hali ya kuwa wamesimama kwa miguu yao, macho ya kukodoka, wakiwa miguu peku, wakiwa uchi, jua litateremshwa juu yao na watakuwa na majasho:

فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ أَلْفَ سَنَةٍ

“Katika siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu.” (32:05)

Watasogea mbele waombe mtu wa kuwaombea kwa Allaah ili awastareheshe kutokana na kisimamo hicho. Watamwendea Aadam (´alayhis-Salaam), kisha wamwendee Nuuh (´alayhis-Salaam), kisha wamwendee Ibraahiym (´alayhis-Salaam), kisha wamwendee Muusa (´alayhis-Salaam) na kisha wamwendee ´Iysaa (´alayhis-Salaam) ambapo wote watataka udhuru na waseme:

“Hakika Allaah amekasirika leo khasira ambayo hajapatapo kukasirika kabla yake na hatokasirika tena mfano wake baada yake.”

Wataomba udhuru kushufaia mbele ya Allaah kutokamana na kisimamo hichi. Hatimaye watamwendea Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo atasema:

“Mimi ndiye mwenye nayo.”

Atasogea mbele ya Mola Wake (Subhaanah), asujudu mbele Yake, amhimidi kwa himdi nyingi, amuombe na kunyenyekea Kwake mpaka aambiwe:

“Ee Muhammad! Inua kichwa chako! Omba utapewa! Shufaia utasikizwa!”

Awaombee waliosimamishwa na Allaah atakubali uombezi wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hatoombea isipokuwa baada ya kupewa idhini ilihali yeye ndiye kiongozi wa viumbe (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baada ya hapo ndio atashufaia uombezi huu mkubwa. Uombezi huu ndio kile  cheo kinachosifiwa alichokitaja Allaah pindi aliposema:

وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَّكَ عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا

“Katika usiku amka uswali, huenda Mola wako Akakuinua cheo kinachosifika.” (17:79)

Kwa sababu kwa uombezi huo atasifiwa na wa mwanzo na wa mwisho[1].

Uombezi wa pili ni pale atapowaombea watu wa Peponi waingie Peponi. Watapofika Peponi hawatofunguliwa mlango moja kwa moja. Watapitia kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili awaombee ufunguliwe mlango wa Peponi ambapo atafanya hivo. Amesema (Ta´ala):

وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا

“Waliomcha Mola wao watapelekwa kuelekea Peponi kwa makundi, mpaka watakapoifikia na ikafunguliwa milango yake.” (39:73)

Hakusema:

“… mpaka watakapoifikia ikafunguliwa milango yake.”

kama ilivyokuja kuhusu watu wa Motoni[2].

Bali amesema:

وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا

“… na ikafunguliwa milango yake.”

Kuja ni kitu na kufunguliwa milango ni kitu kingine. Hilo litafanyika kupitia Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Uombezi wa tatu ni pindi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atapowaombea watu wa Peponi zinanyanyuliwa manzilah zao Peponi.

Uombezi wa nne ni kwa ami yake Abu Twaalib pamoja na kuwa [asli ni kuwa] uombezi hauwafai makafiri. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema kuhusu makafiri:

فَمَا تَنفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ

“Basi hautowafaa uombezi wowote wa waombezi.” (74:48)

Abu Twaalib alikufa juu ya ukafiri. Lakini kwa mtazamo wa kwamba Abu Twaalib alimhami Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akamtetea, akasubiri pamoja naye juu ya dhiki na akamtendea wema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini pamoja na haya yote hakuwafikishwa kuingia katika Uislamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuonyesha Uislamu na alikuwa na pupa aingie katika Uislamu, lakini hata hivyo akakataa. Alikuwa anaona kuwa kuingia katika Uislamu kuna kuitukana dini ya mababa zake. Mori wa kipindi cha kikafiri ndio uliomfanya kukataa. Vinginevyo alikuwa anatambua kuwa Muhammad yuko katika haki na kwamba dini yake ndio ya haki. Lakini kilichomzuia ni mori. Alikuwa anaonelea kuwa lau atasilimu hilo – kwa madai yake – lingehesabika kuwa ni kuwatukana watu wake.

Alichochelea ni lawama na akaogopa kuwatukana watu wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimjia pindi alipokuwa katika hali ya kukata roho akamwabia:

“Ee ami yangu! Sema “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” ni tamko nitalokutetea nalo mbele ya Allaah.””

Abu Jahl na ´Abdullaah bin Abiy Umayyah walikuwepo hapo. Wakamwambia: “Hivi kweli unataka kuipa mgongo mila ya ´Abdul-Muttwalib?” Mwishoni akasema: “Yeye yuko katika mila ya ´Abdul-Muttwalib.””

Hatimaye akafa juu ya hali hiyo na akakataa kusema “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Nitakuombea msamaha midhali sijakatazwa.”[3]

Ndipo Allaah (Ta´ala) akateremsha:

مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَن يَسْتَغْفِرُوا لِلْمُشْرِكِينَ وَلَوْ كَانُوا أُولِي قُرْبَىٰ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُمْ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ

“Haimpasi Nabii na wale walioamini kuwaombea maghfirah washirikina japokuwa ni jamaa zao wa karibu baada ya kuwabainikia kwamba wao ni watu wa [Moto wa] al-Jahiym.” (09:113)

Akateremsha kuhusu Abu Twaalib:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ ۚ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ

“Hakika wewe huwezi kumhidi umpendaye lakini Allaah humhidi amtakaye – Naye anawajua zaidi waongokao.” (28:56)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumuombea atolewe Motoni. Kwa sababu atadumishwa Motoni kama watavyodumishwa milele makafiri wengine wote. Alichomuombea ni Amkhafifishie adhabu peke yake. Atawekwa katika ule moto mwepesi ambapo chini ya miguu yake kuna makaa mawili yanayounguza mpaka kwenye ubongo wake. Haoni kama kuna ambaye yuko na adhabu kali kumshinda[4] pamoja na kuwa yeye ndiye mtu wa Motoni aliye na adhabu nyepesi kabisa.

Hizi ndio nyombezi maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Aina ya pili: Uombezi anaoshirikiana yeye pamoja na Malaika, wapenzi wa Allaah, waja wema na watoto waliokufa kabla ya kubaleghe[5]. Inahusu ule uombezi kwa watenda madhambi makubwa ili watolewe ndani ya Moto au wasiingie kabisa. Ni uombezi ulioenea kwa Malaika, Manabii, Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wapenzi wa Allaah wataowaombea ndugu zao na watoto waliokufa kabla ya kubaleghe ambao watawaombea wazazi wao. Huu ni uombezi ulioenea. Unamuhusu yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wengine pia.

Huu ndio ufupisho unaoweza kusemwa kuhusu uombezi.

Sema kuhusu adhabu ya kaburi… – Haya yameshatangulia kubainishwa katika masuala yanayohusiana na adhabu ya kaburi.

[1] al-Bukhaariy (4718)

[2] Tazama Suurah “az-Zumar” (39) Aayah ya 71

[3] al-Bukhaariy (1360) na Muslim (39) na (24)

[4] al-Bukhaariy (3885) na Muslim (210) na (360)

[5] al-Bukhaariy (334) na (4712) na Muslim (327) na (194)