80. Dalili ya kufa kwa Mtume (صلى الله عليه وسلم)

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّكَ مَيِّتٌ وَإِنَّهُم مَّيِّتُونَ ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عِندَ رَبِّكُمْ تَخْتَصِمُونَ

“Hakika wewe utakufa na wao pia watakufa. Kisha hakika nyinyi siku ya Qiyaamah mbele ya Mola wenu mtagombana.” (az-Zumar 39 : 30-31)

Baada ya watu kufa, watafufuliwa. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ

“Kutoka humo Tumekuumbeni na katika hiyo tutakurudisheni na kutoka humo tutakutoeni mara nyingine.” (Twaa Haa 20 : 55)

وَاللَّـهُ أَنبَتَكُم مِّنَ الْأَرْضِ نَبَاتًا ثُمَّ يُعِيدُكُمْ فِيهَا وَيُخْرِجُكُمْ إِخْرَاجًا

”Allaah amekuotesheni katika ardhi muotesho. Kisha atakurudisheni humo na atakutoeni tena mtoke.” (Nuuh 71 : 17-18)

MAELEZO

“Hakika wewe utakufa… – Aayah hii inathibitisha kuwa Mtume (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) na wale aliotumilizwa kwao watakufa. Baada ya hapo wataenda kugombana mbele ya Allaah siku ya Qiyaamah. Hapo ndipo Allaah atahukumu kati yao kwa haki na Allaah hakuwa ni mwenye kuwapa makafiri ushindi juu ya waumini.

Baada ya watu kufa, watafufuliwa – Katika sentesi hii amebainisha (Rahimahu Allaah) ya kwamba watu baada ya kufa watafufuliwa. Baada ya kufa, Allaah (´Azza wa Jall) atawafufua ili awafanyie hesabu. Hii ndio natija ya kutumilizwa Mitume, ili mtu aweze kuifanyia kazi siku hii, siku ya kufufuliwa na kukusanywa. Hali na khofu ya siku hiyo yake imesifiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa njia ya kwamba inaufanya moyo urejee kwa Allaah (´Azza wa Jall) na kuigopa siku hii. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَكَيْفَ تَتَّقُونَ إِن كَفَرْتُمْ يَوْمًا يَجْعَلُ الْوِلْدَانَ شِيبًا السَّمَاءُ مُنفَطِرٌ بِهِ ۚ كَانَ وَعْدُهُ مَفْعُولًا

“Basi nyinyi mkikufuru, mtawezaje kujikinga na siku itakayowafanya watoto wadogo kuwa wenye kutoka mvi? Hapo mbingu zitapasuka, ahadi Yake itakuwa itatimizwa?” (al-Muzzammil 73 : 17-18)

Katika maneno haya kuna ishara ya kuamini kufufuliwa na Shaykh ametumia dalili juu ya hilo kwa Aayah mbili.

“Kutoka humo Tumekuumbeni… – Bi maana kutokamana na ardhi hii ndio Tumewaumba pindi Aadam (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) alivyoumbwa kutokamana na udongo.

… na katika hiyo tutakurudisheni… – Bi maana wakati mlipozikwa baada ya kufa.

… na kutoka humo tutakutoeni mara nyingine… – Bi maana kwa kufufuliwa siku ya Qiyaamah.

“Na Allaah amekuotesheni katika ardhi muotesho… – Aayah hii ni yenye kuafikiana na maneno Yake (Ta´ala):

مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ

Kutoka humo Tumekuumbeni na katika hiyo tutakurudisheni na kutoka humo tutakutoeni mara nyingine.”

Aayah zilizo na maana kama hii ni nyingi sana. Allaah (´Azza wa Jall) amefanya vitu kuishi na kufa ili baada ya hapo kuvifufua ili kuthibitisha ufufuliwaji. Amefanya hivi ili watu waamini hilo, imani iweze kuzidi na kufanyia kazi siku hiyo kubwa. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) atujaalie kuweza kuifanyia kazi siku hiyo na kuwa ni miongoni mwa wale wenye furaha kwayo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 143-144
  • Imechapishwa: 04/06/2020