Swali 08: Baadhi ya wafanya kazi wa hospitalini katika madaktari, wauguzi wa kike au wenye kufanya kazi ya usafi wanavaa mavazi ya kubana na wanaacha wazi sehemu ya juu ya kifua, mikono yao na miundi yao. Ni ipi hukumu ya Shari´ah katika hayo?

Jibu: Ni wajibu wa madaktari wa kike, wauguzi wa kike na wafanya kazi wa kike kumcha Allaah (Ta´ala) na wavae mavazi ya heshima yasiyoonyesha muundo wa viungo vyao vya mwili au vile viungo visivyotakiwa kuonekana. Bali inatakiwa iwe vazi pana – lisiwe la wasaa sana wala lenye kubana – lenye kuwasitri sitara ya Kishari´ah. Mavazi hayo ni yenye kuwazuia kutokamana na sababu ya fitina. Hayo ni kutokana na zile Aayah mbili zilizotangulia katika jibu la swali la saba[1]. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke ni ´Awrah.”

 “Kuna watu aina mbili wa Motoni sijawaona; wanaume walio na bakora kama mkia wa ng´ombe ambazo wanawapiga kwazo watu, na wanawake waliovaa vibaya, uchi, Maaylaat na Mumiylaat. Vichwa vyao ni kama nundu ya ngamia. Hawatoingia Peponi na wala hawatonusa harufu yake. Harufu yake inapatikana umbali wa kadhaa na kadhaa.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake. Haya ni matishio makali.

Wanaume waliyoko mikononi mwao na bakora ni wale wenye kuyasimamia mambo ya watu na matokeo yake wanawapiga pasi na haki katika mapolisi, wanajeshi au wengineo. Lililo la wajibu kwao wasiwapige watu isipokuwa kwa haki.

Kuhusu wanawake waliovaa vibaya ni wale waliovaa wakiwa uchi mavazi yasiyositiri ima kwa sababu mavazi hayo ni mafupi au kwa sababu ni yenye kubana. Wao wamevaa kwa uinje lakini ukweli wa mambo wako uchi. Kwa mfano wameacha wazi vichwa vyao, vifua vyao, miundi yao au viungo vyenginevyo katika miili yao. Yote haya ni aina ya kuwa uchi.

Lililo la wajibu ni kumcha Allaah katika hilo na kutahadhari kutokamana na kitendo hichi kiovu. Mwanamke anapaswa awe ni mwenye kujisitiri na awe mbali na sababu zinazopelekea kuwafitinisha wanaume. Wanawake wanatakiwa kuyatendea kazi hayo na wawe ni wenye kuvaa nguo za heshima ili waije kuigizwa. Ni wajibu kwa daktari, tabibu, mgonjwa na muuguzi kumcha Allaah. Kadhalika muuguzi wa kiume na wa kike wote hawa wanatakiwa kumcha Allaah. Kama ambavo madaktari wa kiume na wauguzi wa kiume pia wanatakiwa kumcha Allaah katika hayo na awe wenye kujiheshimu na wenye kujisitiri hali ya kujiweka mbali na sababu za fitina.

[1] Tazama https://firqatunnajia.com/7-wanaume-kupeana-mikono-na-wanawake-mahospitalini/

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Mariydhw, uk. 27-30
  • Imechapishwa: 16/05/2019