79. Ndio maana Maswahabah hawakukufuru walipoomba Dhaat Anwaatw

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Na katika dalili ya hayo pia ni yale aliyosema Allaah (Ta´ala) kuhusu wana wa israaiyl – mbali na Uislamu wao, elimu yao na wema wao – walimwambia Muusa:

اجْعَل لَّنَا إِلَـٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ

”Tufanyie nasi mungu kama walivokuwa hawa wana miungu!”

Hali kadhalika walisema baadhi ya Maswahabah: “Tujaalie Dhaat Anwaatw!”. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaapa ya kwamba hii inakumbushia maneno ya wana wa israaiyl: “Tufanyie mungu”.

MAELEZO

Dalili nyingine juu ya kwamba mtu anaweza kusema au kutenda kitu cha kufuru pasi na kujua, ni yale yaliyosemwa na wana wa israaiyl. Walifanya haya pamoja na Uislamu, elimu na wema waliokuwa nao. Walimwambia Muusa (´alayhis-Swalaatu was-Salaam):

اجْعَل لَّنَا إِلَـٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ

”Tufanyie nasi mungu kama walivokuwa hawa wana miungu!”

Kadhalika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walisema:

“Tujaalie Dhaat Anwaatw kama wao walivyo na Dhaat Anwaatw!”

Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Allaah ni mkubwa! Ninaapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake! Mmesema kama walivyosema wana wa israaiyl kumwambia Muusa: “Tufanyie mungu kama wao walivyo na mungu.” Mtakuja kufuata nyayo za wale waliokuwa kabla yenu.”[1]

Hii inafahamisha ya kuwa Muusa na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhimaa was-Salaam) waliyakemea hayo kwa ukali, kama inavyotakikana. Mitume hawa wawili watukufu hawakuwakubalia watu wao maombi haya. Uhakika wa mambo ni kwamba waliwakemea kwa hilo.

Baadhi ya washirikina wamefanya dalili hii kuwa ni utata na wakasema kuwa si Maswahabah wala wana wa israaiyl hawakukufuru. Jibu ya hili ni kwamba si Maswahabah wala wana wa israaiyl hawakufanya kitu baada ya kukaripiwa na Mitume wawili watukufu.

[1] Ahmad (5/218) na at-Tirmidhiy (1771) ambaye amesema: ”Hadiyth ni Swahiyh na ni nzuri.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 89-90
  • Imechapishwa: 25/11/2023