77. Mtazamo wa Mu´tazilah juu ya mizani siku ya Qiyaamah


Mu´tazilah wanasema kuwa sio mizani ya kihakika. Wanasema kuwa maana yake ni kusimamisha uadilifu. Wanaona kuwa ni mizani ya kimaana na kwamba maana yake ni kusimamisha uadilifu kati ya waja. Wao hawana mashiko mengine zaidi ya akili zao. Wao wanaipinga kwa sababu hawajaiona. Wao ni watu wasioamini mambo yaliyofichikana. Haya ndio maradhi ya kuitegemea akili. Kwa sababu muumini haitegemei akili yake. Akili ni dalili, lakini sio katika mambo yote. Kuna mambo yasiyodhibitiwa na akili. Mambo yaliyofichikana akili haiwezi kuyadhibiti. Hivyo usiihukumu akili yako kwa mambo hayo. Mambo hayo yanategemea dalili peke yake. Hili ndilo lililowafanya kuipinga. Madhehebu yao yamejengwa juu ya kupinga kile wasichokiona au wanakipindisha maana kinyume na maana yake. Hawawezi kupinga mizani kwa kuwa ni kitu kilichothibiti katika Qur-aan. Amesema (Ta´ala):

وَالْوَزْنُ يَوْمَئِذٍ الْحَقُّ ۚ فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُم بِمَا كَانُوا بِآيَاتِنَا يَظْلِمُونَ

“Na mizani siku hiyo itakuwa ni haki. Basi ambao mizani yao itakuwa nzito – hao ndio watakaofaulu, na ambao mizani yao itakuwa khafifu – basi hao ni wale waliokhasirika nafsi zao kwa yale waliyokuwa wakizifanyia dhulma Aayaat Zetu.” (07:08-09)

فَأَمَّا مَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ  فَهُوَ فِي عِيشَةٍ رَّاضِيَةٍ  وَأَمَّا مَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ  فَأُمُّهُ هَاوِيَةٌ

“Basi yule itakayekuwa mizani yake nzito, basi huyo atakuwa katika maisha ya kuridhisha, na yule itakayekuwa mizani yake khafifu, basi makazi yake [itakuwa] ni Haawiyah.” (101:06-09)

Hawapingi tamko la mizani. Lakini hata hivyo wanaifasiri na kuipotosha kinyume na maana yake. Hivi ndivyo ilivyo hali yao katika maandiko mengine yote ambapo wanaikengeusha kinyume na maana yake sahihi.

Kuhusu Ahl-ul-Haqq wao wanaiamini  juu ya uhakika wake. Kuhusu namna yake hakuna anayeijua isipokuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa).