Ni haramu kwa mwanamke kupeana mikono na mwanaume ambaye sio Mahram yake. Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin Baaz (Hafidhwahu Allaah), raisi mkuu wa baraza la kufutu, Da´wah na maelekezo, amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa” iliyochapishwa na Mua´ssasat-ud-Da´wah al-Islaamiyyah as-Swahafiyyah:

“Haijuzu kabisa kupeana mikono na wanawake ambao sio Mahram. Ni mamoja mwanamke huyo ni msichana au mzee. Ni mamoja huyo anayepewa mkono ni kijana au mtumzima mzee. Hayo ni kutokana na ile khatari ya fitina kwa wote wawili. Imesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakupatapo kamwe kugusa mkono wa mwanamke. Hakuwa anawapa bay´ah isipokuwa kwa maneno tu.”

Hakuna tofauti eti anapeana mkono kwa kizuizi katikati au bila kizuizi kutokana na kuenea kwa dalili na kwa ajili ya kuzuia njia zinazopelekea katika fitina.”[1]

Shaykh Muhammad al-Aamiyn ash-Shanqiytwiy (Rahimahu Allaah) amesema katika “Adhwaa´-ul-Bayaan”:

“Tambua kwamba haijuzu kwa mwanamume wa kando kupeana mkono na mwanamke ambaye ni kando naye. Wala haijuzu kwa mwanaume kugusa kitu chochote katika mwili wake. Dalili juu ya hayo ni mambo yafuatayo:

1 – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) imethibiti kutoka kwake kwamba amesema:

“Mimi sipeani mikono na wanawake… “

Na Allaah anasema:

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ

“Hakika mna kigezo chema kwa Mtume wa Allaah.”[2]

Hivyo itatulazimu na sisi kutopeana mikono na wanawake kwa ajili ya kumuigiliza yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hadiyth iliyotajwa tumeitanguliza katika Suurah “al-Hajj” hali ya kuweka wazi katika kuelekezea makatazo ya kuvaa nguo inayomili kwenye rangi ya njano kibichi kwa wanaume katika Ihraam na kwenginepo na katika Suurah “al-Ahzaab” katika Aayah ya Hijaab hii hapa. Kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutopeana mikono na wanawake katika wakati wa kuwapa bay´ah ni dalili ya wazi kabisa inayoonyesha kwamba mwanamume hapeani mkono na mwanamke na wala hagusi kitu katika mwili wake. Kwa sababu jambo jepesi zaidi katika mambo ya kugusa ni kupeana mikono. Hivyo, akikataa kufanya hivo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika wakati ambapo kuna haja – nao ni ule wakati wa kupeana bay´ah – ni dalili inayoonyesha kuwa haijuzu. Haifai kwa yeyote kwenda kinyume naye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu yeye ndiye mwenye kuwawekea Ummah wake Shari´ah kwa matendo yake, maneno yake na yale anayoyakubali.

2 – Ni yale tuliyoyatanguliza kwamba mwanamke yeye wote ni uchi. Hivyo ni lazima kwake kujifunika. Ameamrishwa kuteremsha macho yake ili asije kutumbukia katika fitina. Hapana shaka kwamba mwili kugusana na mwili mwingine ni jambo lina nguvu zaidi katika kuamsha matamanio na ni jambo lina nguvu zaidi kuita katika fitina kuliko kutazama kwa macho. Kila mwadilifu anayajua hayo.

3 – Hiyo ni njia inayopelekea kupata ladha kutoka kwa mwanamke wa kando kutokana na uchache wa kumcha Allaah katika zama hizi, kupoteza amana na kutojichunga na mambo yenye kutia mashaka. Mara nyingi tumeeleza kwamba baadhi ya waume wa watu wajinga wanakubali dada ya mke wake kuweka mdomo juu ya mdomo wake na wanaita kitendo hicho cha kusalimiana kuwa ni ´kubusu` kulikoharamishwa kwa maafikiano au wanasema: “Msalimie mwanamke huyo!” na huku wanamaanisha kumbusu. Haki isiyokuwa na mashaka yoyote ndani yake ni kwamba mtu anatakiwa kujiepusha na fitina, mashaka yote na sababu zake. Miongoni mwa sababu zake kubwa ni mwanamume kugusa kitu kutoka kwa mwanamke wa kando. Ni lazima kufunga njia zinazopelekea katika haramu.”[3]

[1] (01/185).

[2] 33:21

[3] (06/602-603).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 127-130
  • Imechapishwa: 12/12/2019