74. Hijrah itaendelea kuwepo mpaka siku ya Qiyaamah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ أَرْضِي وَاسِعَةٌ فَإِيَّايَ فَاعْبُدُونِ

“Enyi waja Wangu ambao mmeamini! Hakika ardhi Yangu ni pana, hivyo basi Mimi pekee niabuduni.” (al-´Ankabuut 29 : 56)

al-Baghawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Sababu ya kuteremka Aayah hii ni kwa baadhi ya waislamu Makkah ambao hawakufanya Hijrah. Hivyo Allaah amewazungumzisha kwa jina la imani.”

Dalili juu ya Hijrah kutoka katika Sunnah, ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hijrah haitosimama mpaka Tawbah isimamishwe. Na Tawbah haitosimamishwa mpaka jua lichomoze kutoka magharibi.”

MAELEZO

al-Baghawiy (Rahimahu Allaah) amesema… – Ikiwa Shaykh (Rahimahu Allaah) amenukuu maneno ya al-Baghawiy kutoka katika tafsiri yake ya Qur-aan, basi ni dhahiri kuwa amenukuu maneno ya al-Baghawiy kimaana na sio kimatamshi. Kwa sababu matamshi haya hayako katika tafsiri ya Qur-aan ya al-Baghawiy.

Hijrah haitosimama… – Hili litapitika pale ambapo matendo mema yatasimamishwa kukubaliwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَوْمَ يَأْتِي بَعْضُ آيَاتِ رَبِّكَ لَا يَنفَعُ نَفْسًا إِيمَانُهَا لَمْ تَكُنْ آمَنَتْ مِن قَبْلُ أَوْ كَسَبَتْ فِي إِيمَانِهَا خَيْرًا

“Siku zitakapokuja baadhi za alama za Mola wako haitoifaa nafsi imani yake, ikiwa haikuamini kabla au haikuchuma katika imani yake kheri yoyote.” (al-An´aam 06 : 158)

Makusudio ya “baadhi ya alama” ni jua kuchomoza kutoka magharibi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 131
  • Imechapishwa: 03/06/2020