73. Uhalisia wa hali ndani ya kaburi


Mambo yanayompitikia maiti ndani ya kaburi ambayo ni wajibu kwa mtu kuyaamini ni yafuatayo:

La kwanza: Kujiwa na Munkar na Nakiyr. Malaika hawa wawili wanamjia maiti. Ikiwa mtu atauliza ni vipi wanamjia ndani ya kaburi ilihali sisi hatuwaoni? Jibu ni kuwa Allaah juu ya kila kitu ni muweza. Hakika umefichikiwa vitu vingi. Malaika wawili hawa wanamjia ilihali wewe huwaoni. Hivi wewe unaiona roho yako inayoingia kwenye mwili wako? Wewe unaona kila kitu? Kuna vitu vingi usivyoviona. Je, wewe unaiona akili yako inayokupambanua wewe na vyengine? Sio kila usichokiona si sahihi. Haya ni maneno ya watu wa mazingira. Kuhusu watu wa imani; imani yao inawawezesha kuamini yale yote yaliyopokelewa kwa mapokezi sahihi na hawayaingizii ndani yake akili zao. Malaika hao wawili wanamjia na kumkaza na kumtamkisha: “Ni nani Mola Wako? Ni ipi dini yako? Ni nani Mtume Wako?” Muumini atajibu: “Mola Wangu ni Allaah, dini yangu ni Uislamu na Mtume wangu ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Anadi mwenye kunadi: “Amesema kweli mja Wangu, muandalieni makazi Peponi, mpanulieni kaburi lake upeo wa macho yake na mfungulieni mlango Peponi.” Baada ya hapo ajiwe na harufu na manukato yake na aone makazi yake Peponi. Aseme: “Ee Mola! Lete Qiyaamah ili niweze kurejea kwa familia na mali yangu.”[1]

Pepo yake igeuke kuwa ni bustani miongoni mwa mabustani ya Peponi. [Tunayaamini] hata kama hatuyaoni. Kuna baadhi ambao wanaweza kuyaona ambao Allaah amependa kuwaonyesha nayo. Lakini hata hivyo sio jambo la lazima.

Kuhusu mnafiki na mwenye mashaka – ambaye aliishi juu ya shirki duniani – atakufa juu ya shaka. Atapoulizwa: “Ni nani Mola Wako?” Atasema: “Sijui.” Atapoulizwa: “Ni ipi dini yako?” Atasema: “Sijui. Niliwasikia watu wanasema kitu na mimi nikakisema.” Atapoulizwa: “Ni nani Mtume wako?” Atasema: “Sijui.” Huyu ni kwa sababu duniani hakuamini kwa moyo wake isipokuwa alitamka tu kwa ulimi wake. Yeye aliwasikia watu wanasema kitu na yeye akakisema kwa ajili ya kuwapaka mafuta. Huyu ndiye mnafiki. Ni yule anayesema yale yanayosemwa na wenye kuswali na anaswali na kufunga, lakini pamoja na hivyo moyoni mwake hakuna imani. Anafanya haya kwa ajili tu ya kutaka kuwapaka watu mafuta na unafiki. Anafanya hivi ili tu aweze kueshi pamoja na waislamu na wakati huo huo haamini ndani ya moyo wake. Hata kama alikuwa ni mfaswaha, amehifadhi vitabu na vitabu na milolongo ya wapokezi, ndani ya kaburi lake hatoweza kuzungumza na jibu litampotea na kusema kwamba hajui. Lakini hata hivyo niliwasikia watu wakisema kitu na mimi nikakisema pasi na kukijua kitu hicho na kukiamini. Anadi mwenye kunadi: “Amesema uongo mja wangu. Muandalieni makazi Motoni, mfungulieni mlango Motoni na ajiwe na moto na vuke lake na kaburi lake limbane mpaka mbavu zake zikutane – tunaomba Allaah atukinge – na kaburi lake ligeuke kuwa ni shimo miongoni mwa mashimo ya Motoni.” Aseme: “Ee Mola! Usilete Qiyaamah.” Kwa kuwa anajua kuwa Qiyaamah kikisimama, basi hali  inayokuja baadaye ni mbaya zaidi kuliko aliyomo hivi sasa. Haya yanaashiriwa na maneno Yake (Ta´ala):

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ

“Allaah huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na Aakhirah… “

Allaah atawathibitisha ndani ya kaburi na wakati wa kuhojiwa kama ambavyo waliishi juu ya kauli thabiti duniani na imani ya kweli.

وَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ

“… na Allaah huwaacha wakapotea madhalimu.” (14:27)

Hawatoweza kujibu.

Hadiyth kuhusu haya zimepokelewa kwa mapokezi mengi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ahl-us-Sunnah wameafikiana juu yake. Hakuna walioyapinga isipokuwa Mu´tazilah ambao wanategemea akili yao. Hali kadhalika watu wa mantiki hii leo, ambao ni vifaranga vya Mu´tazilah, nao pia wanafuata madhehebu haya.

[1] Abu Daawuud (4753), Ahmad (04/287) na at-Twayaalisiy (01/102) na wengineo