73. Mikono inainuliwa katika ile Takbiyr ya kwanza peke yake


75- Imesuniwa kwake kunyanyua mikono yake katika Takbiyr ya kwanza. Kumepokelewa Hadiyth mbili juu ya hilo:

Ya kwanza: Abu Hurayrah amesimulia:

“Kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimswalia maiti na akapiga Takbiyr juu ya maiti ambapo akanyanyua mikono katika Takbiyr ya kwanza, akaweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto.”

Ameipokea at-Tirmidhiy (02/165), ad-Daaraqutwniy (192), al-Bayhaqiy (284), Abush-Shaykh katika “Twabaqaat-ul-Aswbahaaniy”, uk. 262 kwa cheni ya wapokezi ambayo ni dhaifu. Lakini hata hivyo inatolewa ushahidi na Hadiyth inayofuata:

Ya pili: ´Abdullaah bin ´Abbaas ameeleza:

“Kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akinyanyua mikono juu ya jeneza katika Takbiyr ya kwanza. Halafu harudi.”

Ameipokea ad-Daaraqutwniy kwa cheni ya wapokezi ambayo wapokezi wake ni waaminifu isipokuwa al-Fadhwl bin as-Sakan ambaye ni mtu asiyejulikana. Ibn-ut-Turkumaaniy amemkalia kimya katika “al-Jawhar-un-Naqiyy” (04/44).

Kisha at-Tirmidhiy akasema mara tu baada ya Hadiyth ya kwanza:

“Hadiyth hii ni geni. Wanachuoni wametofautiana juu ya hili. Wanachuoni wengi katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wengineo wameonelea mtu anyanyue mikono yake katika kila Takbiyr. Haya pia ndio maoni ya Ibn-ul-Mubaarak, ash-Shaafi´iy, Ahmad na Ishaaq. Wanachuoni wengine wakasema: “Asinyanyue mikono yake isipokuwa katika ile Takbiyr ya kwanza. Haya ndio maoni ya ath-Thawriy na wanachuoni wa Kuufah. Imetajwa kutoka kwa Ibn-ul-Mubaarak kwamba amesema kuhusu kuswalia jeneza: “Asiweke mkono wake wa kulia juu ya mkono wake wa kushoto.” Baadhi ya wanachuoni wameonelea kwamba akamate mkono wake wa kushoto kama anavofanya katika swalah.”

Katika “al-Majmuu´” (05/232) ya an-Nawawiy imekuja:

“Ibn-ul-Mundhir amesema katika vitabu vyake viwili “al-Ishraaf” na “al-Ijmaa´”:

“Wameafikiana juu ya kwamba anyanyue mikono katika ile Takbiyr ya kwanza na wakatofautiana katika zile zengine zilizobakia.”

Hatujapata katika Sunnah yanayofahamisha juu ya usuniwaji wa kunyanyua mikono mbali na ile Takbiyr ya kwanza. Kwa hiyo hatuoni kuwa imesuniwa kufanya jambo hilo. Haya ndio madhehebu ya Hanafiyyah na wengineo. Pia yamechaguliwa na ash-Shawkaaniy na wengineo katika wakaguzi. Ibn Hazm ameenda katika hayo na akasema (05/128):

“Kuhusu kunyanyua mikono ni jambo halikupokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alinyanyua sehemu yoyote katika Takbiyr ya jeneza isipokuwa katika Takbiyr ya kwanza peke yake. Kwa hiyo haijuzu kufanya hivo. Kwa sababu ni kitendo ndani ya swalah ambacho hakukupokelewa andiko juu yake. Shani ya mambo kilichopokelewa kutoka kwake ni kwamba alipiga Takbiyr na akanyanyua mikono yake katika sehemu zote za kuinama na kuinuka. Lakini katika swalah ya jeneza hakuna kuinuka wala kuinama. Ajabu ni maneno ya Abu Haniyfah kunyanyua mikono katika kila Takbiyr katika swalah ya jeneza, jambo ambalo halikuja kabisa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kukataza kwake kunyanyua mikono katika sehemu zote za kuinama na kuinuka kwenye swalah zilozobaki, jambo ambalo limesihi kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Yale aliyoyaegemeza kwa Abu Haniyfah yaliyopokelewa katika baadhi ya vitabu vya maelezo kutoka kwa Hanafiyyah usidanganyike na yale yaliyotajwa katika maelezo ya chini ya “Naswb-ur-Raayah” (02/285) juu ya uegemezwaji huu, hilo ndio chaguo la maimamu wengi wa Balkh ambapo miongoni mwao ni kama ilivo katika “al-Mabsuutw” cha as-Sarakhsiy (02/64). Lakini kinachofanyiwa kazi na Hanafiyyah ni kinyume na hivo na ndio kilichopitishwa na as-Sarakhsiy. Lakini hata hivyo wanaona kufaa kunyanyua mikono katika zile Takbiyr zilizozidi katika swalah za ´iyd mbili licha ya kuwa ni jambo pia lisilokuwa na msingi wowote kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ni kweli kwamba al-Bayhaqiy (04/44) amepokea kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kutoka kwa Ibn ´Umar kwamba alikuwa akiinua mikono yake katika kila Takbiyr miongoni mwa Takbiyr za jeneza. Ambaye alikuwa anafikiria kuwa alikuwa hafanyi hivo isipokuwa kwa kuliegemeza kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi na yeye anyanyue. as-Sarakhsiy ametaja kutoka kwa Ibn ´Umar kinyume na hayo. Hayo ni miongoni mwa mambo ambayo hatujui msingi wowote wa kufaa katika vitabu vya Hadiyth.

Kuhusu usahihisha kutoka kwa baadhi ya wanachuoni waheshimiwa upokezi  wa kuinua mikono katika taaliki yake juu ya “Fath-ul-Baariy” (03/190) ni kosa la wazi, kama ambavo hilo liko wazi kwa ambaye ni mtambuzi wa fani hii.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 146-148
  • Imechapishwa: 01/02/2022