72. Sababu ya washirikina kukanusha Qiyaamah


Qiyaamah kikubwa kitakutana na kila mtu. Kuhusu mtu mmojammoja ni kwamba kila anayekufa basi amekutana na Qiyaamah na Saa. Ambaye anakufa na akaiaga dunia hii na akaingizwa ndani ya kaburi ambacho ni kituo baina ya dunia na Aakhirah. Imani ya kuamini Qiyaamah na yale yote yatayopitika ndani yake (kama vile Pepo, Moto, hesabu, adhabu, Mizani, madaftari ya matendo, watu kukabidhiwa madaftari yao ima kwa mkono wa kuume au wa kushoto na Njia ilioko juu ya Moto) yote haya ni lazima kuyaamini. Haijuzu kutilia shaka chochote katika hayo. Washirikina wamepinga kutokea Qiyaamah kwa sababu wamelinganisha uwezo wa Allaah na uwezo wao. Ni vipi mtu atakufa na kugeuka udongo kisha afufuliwe tena kwa mara nyingine? Hilo ni marejeo ya mbali:

أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ

“Je, hivi tukifa na tukawa udongo na mifupa, hivi sisi tutafufuliwa?”[1]

وَقَالُوا أَإِذَا كُنَّا عِظَامًا وَرُفَاتًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ خَلْقًا جَدِيدًا

“Wakasema: “Je, hivi sisi tukiwa mifupa na mapande yaliyosagikasagika, je, sisi hivyo tutafufuliwa kwa umbo jipya?”[2]

Hapa ndipo kikomo cha akili yao. Wamesahau uwezo wa Allaah na kwamba Allaah (Jalla wa ´Alaa) hashindwi na chochote. Allaah ameraddi madai yao kwa dalili ndani ya Qur-aan ikiwa ni pamoja na kuwathibitishia kwamba Yule aliyeweza kuwaumba basi ni muweza vilevile wa kuwarudisha upya kwa mara nyingine. Yeye ndiye amewaumba kutoka patupu na akawaumba baada ya kutokuweko. Basi Yeye ana haki zaidi ya kuwarudisha upya. Allaah (Jalla wa ´Alaa) anaihuisha ardhi baada ya kufa kwake – vivyo hivyo Kufufuliwa:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنَّكَ تَرَى الْأَرْضَ خَاشِعَةً فَإِذَا أَنزَلْنَا عَلَيْهَا الْمَاءَ اهْتَزَّتْ وَرَبَتْ ۚ إِنَّ الَّذِي أَحْيَاهَا لَمُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۚ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

”Miongoni mwa alama Zake ni kwamba utaona ardhi imetulia kame, kisha tunapoiteremshia maji inataharaki na kuotesha. Hakika Yule aliyeihuisha, bila shaka ni Mwenye kuhuisha wafu, hakika Yeye juu ya kila jambo ni Muweza.”[3]

Kama ambavyo mbegu inaota kutoka ardhini basi vivyo hivyo vitaota viwiliwili kutoka ardhini. Allaah atairudisha ardhi kuwa kama ilivyokuwa hapo kabla kwa umbile lake la asili:

قَدْ عَلِمْنَا مَا تَنقُصُ الْأَرْضُ مِنْهُمْ ۖ وَعِندَنَا كِتَابٌ حَفِيظٌ

“Hakika Sisi tunajua kinachopunguzwa na ardhi kutokana nao na tunacho Kitabu kinachohifadhi kwelikweli.”[4]

Hata kama watakuwa wameshaoza na kugeuka udongo, basi Allaah atairudisha katika umbile lake la asili kama ilivyokuwa hapo kabla hali ya kuwa ni wenye kutikisika, hai, wenye kusikia na wenye kuona. Hakuna chochote ambacho kinashindikana.

Allaah ndiye ambaye ameziumba mbingu na ardhi. Je, si muweza wa kumrudisha mtu?

لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ

”Bila shaka uumbaji wa mbingu na ardhi ni mkubwa zaidi kuliko uumbaji wa watu, lakini watu wengi hawajui.”[5]

Ambaye ameziumba mbingu na ardhi ni muweza wa kumrudisha mtu. Kwa dalili hizi za kukata kabisa zilizotajwa na Allaah ndani ya Qur-aan anawasambaratisha wale makafiri wanaopinga Kufufuliwa. Wamemfanya Allaah kutokuwa na uwezo juu yao – Allaah ametakasika kutokamana na yale wanayoyasema!

Waumini watambuzi wanaamini uwezo wa Allaah. Kwao jambo liko wazi kabisa. Wanaliamini kikamilifu kujengea juu ya maelezo ya Allaah na kwa sababu Allaah ni muweza juu ya kila jambo.

وَأَنَّ السَّاعَةَ آتِيَةٌ لَّا رَيْبَ فِيهَا وَأَنَّ اللَّـهَ يَبْعَثُ مَن فِي الْقُبُورِ

“…. na kwamba Saa itafika tu haina shaka ndani yake na kwamba Allaah atafufua waliyomo ndani ya makaburi.”[6]

Allaah atawafufua walioko ndani ya makaburi ijapo wameshakuwa udongo na kuoza. Allaah hakuna kitu kinachomshinda.

[1] 37:16

[2] 17:49

[3] 41:39

[4] 50:4

[5] 40:57

[6] 22:7

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 56
  • Imechapishwa: 12/08/2021