71. Hijrah ya Mtume (صلى الله عليه وسلم) kutoka Makkah na kwenda al-Madiynah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Aliswali Makkah kwa miaka mitatu. Baada yake akaamrishwa kufanya Hijrah kwenda al-Madiynah.

Aliswali Makkah kwa miaka mitatu – Swalah ambazo ni Rak´ah nne alikuwa akiziswali Rak´ah mbili mpaka alipohamia al-Madiynah. Baadaye wasafiri wakaendelea kuswali kama mwanzoni na wakazi wakaanza kuswali nne.

MAELEZO

Baada yake akaamrishwa kufanya Hijrah kwenda al-Madiynah – Allaah (´Azza wa Jall) alimwamrisha Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhajiri kwenda al-Madiynah kwa sababu watu wa Makkah walimkataza kusimamisha Da´wah yake. Katika Rabiy´ al-Awwal miaka kumi na tatu baada ya kupewa utume Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifika al-Madiynah baada ya kuhajiri kutoka Makkah.

Makkah ndio ulikuwa mji wa kwanza ulioteremshiwa Wahy na mji ambao unapendwa zaidi na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuhajiri kulikuwa baada ya kupewa idhini na Mola Wake. Kabla ya hapo aliishi Makkah kwa miaka kumi na tatu na anafikisha ujumbe wa Mola Wake na akilingania katika dini Yake kwa elimu. Mabwanyenye wengi wa Quraysh waliikabili Da´wah yake kwa kuikataa, kuipa mgongo na kumshambulia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wale waliomuamini. Mpaka mwishowe ikafikia kiasi cha kwamba wakakusanyika ili kumuua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakashauriana juu ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na nini watachomfanya baada ya kuwaona Maswahabah zake wanahajiri kwenda al-Madiynah. Hii ina maana bila ya shaka ya kwamba ni lazima ataenda kujiunga nao na baada ya hapo atapata ushindi na msaada kutoka kwa Answaar ambao walimpa ahadi ya kuamini na utiifu juu ya kumzuia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yale wanayowazuia kwayo watoto wao na wake zao. Hili litapelekea yeye kuweza kupata utawala wake dhidi ya Quraysh. Adui wa Allaah Abu Jahl akasema:

“Rai bora ni sisi tuchague kutoka katika kila kabila kijana mwenye nguvu. Halafu tumpe kila mmoja upanga wenye makali na waende kwa Muhammad wampige kwa pamoja na kummaliza. Baada ya hapo tutastarehe naye. Damu yake itaenea kwa makabila mbalimbali na hapo kabila la ´Abd Manaaf – yaani nduguze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – hawatoweza kupigana na makabila yote. Badala yake wataridhika kupewa diyaa, na hapo tutawapa.”

Allaah akamjuza Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) makusudio na njama za washirikina na hivyo akawa amempa idhini ya kuhama.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) tokea hapo mbele alikuwa ameshajiandaa kuhajiri kwenda al-Madiynah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia:

“Tulia. Nataraji nitapewa idhini.”

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) akachelewesha Hijrah ili aweze kutangamana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Siku moja pindi tulipokuwa nyumbani kwa Abu Bakr katikati ya mchana, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaja mlangoni. Uso wake ulikuwa umefunikwa. Abu Bakr akasema: “Ninawatoa fidia wazazi wangu juu yake! Ninaapa kwa Allaah hakuja kwa saa kama hii isipokuwa kwa kitu muhimu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaingia na kumwambia: “Watoe nje walioko kwako.” Akasema: “Ni familia yako tu.” Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Nimepewa idhini ya kuhajiri.” Abu Bakr akasema: “Nakuomba nisuhubiane na wewe, ewe Mtume wa Allaah.” Akasema: “Ndio.” Abu Bakr akasema: “Ee Mtume wa Allaah, chukua mmoja katika wanyama wangu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Kwa thamani.”

Kisha wakatoka na wakakaa katika pango kwenye mlima Thawr siku tatu. Katika masiku haya ´Abdullaah bin Abiy Bakr pia alikuwa akilala nao. Alikuwa ni kijana, mwenye akili na makini. Usiku unapokaribia kumalizika, anarudi Makkah na anakuwa na Quraysh asubuhi. Hakukusemwa khabari yoyote juu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na rafiki yake, isipokuwa anaielewa na kuihifadhi. Baada ya hapo wakati giza linapoanza kuingia, anarudi na kuwaeleza kilichosemwa. Quraysh wakaanza kumtafuta Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kila mahali na wakitumia kila njia ili waweze kumpata Mtume. Ilifikia kiasi cha kwamba, wakamuahidi kumpa ngamia mia, yule mwenye kuja nao, au mmoja katika wao. Lakini Allaah alikuwa na wao na akiwahifadhi kwa hifadhi Yake na akiwatunza kwa ulinzi Wake. Quraysh walisimama nje ya mlango wa pango bila ya kuwaona. Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Nilimwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati tulipokuwa ndani ya pango: “Lau mmoja wao angelitazama kwenye miguu yake, wangelituona.” Akasema: “Usihuzunike. Hakika Allaah yupamoja basi. Ee Abu Bakr, wafikiriaje watu wawili wakati Allaah ndio watatu wao?””[1]

Kule kuwatafuta kulipotulia kidogo, ndio wakatoka ndani ya pango lile baada ya masiku matatu na kuanza safari yao kuelekea al-Madiynah kwa njia ya pwani.

Pindi watu wa al-Madiynah miongoni mwa Muhaajiruun na Answaar waliposikia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yuko njiani kwenda kwao, walikuwa wakitoka kila asubuhi nje ya mji wakingojea kufika kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na rafiki yake. Wanasimama na kungojea mpaka ukali wa jua unawalazimisha kurudi. Siku ambayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa afike, wakafanya vilevile na wakarudi majumbani mwao pindi jua lilipokuwa likali. Wakati huo kulikuwa myahudi mmoja alokuwa juu ya jengo limoja lirefu al-Madiynah na akitafuta haja yake. Pindi alipomuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na rafiki yake, hakuweza kustahamili kuacha kunadi kwa sauti: “Enyi kongamano la waarabu! Imefika zamu yenu.” Bi maana furaha na utukufu wenu mnaosubiri. Waislamu wakaondoka kwenda kumpokea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na walikuwa na silaha ili kumuadhimisha na kumtukuza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lengo lingine ilikuwa kuonyesha kuwa wako tayari kupigana jihaad na kumlinda – Radhi za Allaah ziwe juu yao. Wakampokea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika uwanja wa mwamba. Akaendelea upande wa mashariki na akashukia kwenye kabila la ´Amr bin ´Awf Qubaa´. Huko alikaa siku kadhaa na akajenga msikiti. Kisha akaenda al-Madiynah na wakati huo akikutana na watu njiani. Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) akasema:

“Wakati tulipofika al-Madiynah, watu walitoka kwenye njia. Watoto na wafanya kazi walisimama juu ya majengo huku wakisema: “Allaah ni mkubwa, Mtume wa Allaah amekuja! Allaah ni mkubwa, Muhammad amekuja!”

[1] al-Bukhaariy (3653) na Muslim (2381).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 126-129
  • Imechapishwa: 03/06/2020