70. Safari ya Mtume (صلى الله عليه وسلم) kupandishwa mbinguni

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Miaka kumi alilingania katika Tawhiyd. Baada ya miaka kumi alipandishwa mbinguni na akafaradhishiwa swalah tano kwa siku.

MAELEZO

Miaka kumi alilingania katika Tawhiyd – Bi maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alibaki miaka kumi akiwalingania watu kumpwekesha Allaah (´Azza wa Jall) na kumpwekesha kwa ´ibaadah (Subhaanah).

Baada ya miaka kumi alipandishwa mbinguni… – Bi maana alinyanyuliwa juu:

تَعْرُجُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ إِلَيْهِ

“Malaika na roho wanapanda Kwake.” (al-Ma´aarij 70 : 04)

Hili ni katika mambo makubwa ambayo ni maalum kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah alimfadhilisha kwa tukio hili kabla ya kuhama kutoka Makkah.

Wakati alipokuwa amelala katika chumba karibu na Ka´bah, alikuja mwenye kuja ambaye alifungua mwili wake kutoka sehemu ya chini ya shingo mpaka sehemu ya chini ya tumbo. Halafu moyo wake ukatolewa nje na kujazwa hekima na imani, kwa kumwandaa kwa yale atakayotekeleza. Kisha akaletewa kipando cha mnyama. Alikuwa ni mdogo kuliko nyumbu na mkubwa kuliko punda na alikuwa akiitwa “al-Buraaq”. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akapanda juu yake huku akisuhubiana na mwaminifu Jibriyl. Wakasafiri mpaka walipofika Yerusalemu. Akashuka na akaswali na Mitume. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaswalisha Mitume na Manabii wote, ili ipate kubainika fadhilah na utukufu wake na kwamba yeye ndiye kiongozi anayetakiwa kufuatwa.

Kisha Jibriyl akampandisha katika mbingu ya chini ya dunia. Wakati walipofika, akaomba ifunguliwe. Kukasemwa: “Ni nani?” Akasema: “Ni Jibriyl.” Akaambiwa: “Ni nani yuko pamoja nawe?” Akasema: “Ni Muhammad.” Kukasemwa: “Ameitwa?” Akasema: “Ndio.” Hivyo kukasemwa: “Karibu! Mfikaji bora aliyoje amefika!” Hivyo akawa amefunguliwa na huko akamuona Aadam. Jibriyl akasema: “Huyu ni baba yako Aadam. Msalimie.” Akamsalimia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yeye akamuitikia salamu na kusema: “Karibu mtoto mwema na Mtume mwema.” Kuliani mwa Aadam kulikuwa roho zenye furaha kutoka katika kizazi chake na kushotoni mwake kulikuwa roho zilizokula hasara kutoka katika kizazi chake. Pindi anapotazama kuliani mwake, hufurahi na kucheka, na pindi anapotazama kushotoni mwake hulia.

Halafu akachukuliwa na Jibriyl na kumpeleka katika mbingu ya pili. Walipofika, akaomba ifunguliwe na kadhalika. Huko akakutana na mabinamu Yahyaa na ´Iysaa (´alayhimaas-Swalaatu was-Salaam). Jibriyl akasema: “Huyu ni Yahyaa na ´Iysaa. Wasalimie.” Akawasalimia na wao wakamrudishia salamu na kusema: “Karibu ndugu mwema na Mtume mwema.” Halafu akachukuliwa na Jibriyl na kumpeleka katika mbingu ya tatu. Walipofika, akaomba ifunguliwe na kadhalika. Huko akakutana na Yuusuf (´alayhis-Swalaatu was-Salaam). Jibriyl akasema: “Huyu ni Yuusuf. Msalimie.” Akamsalimia na yeye akamrudishia salamu na kusema: “Karibu ndugu mwema na Mtume mwema.” Kisha akachukuliwa na Jibriyl na kumpeleka katika mbingu ya nne. Wakati walipofika, akaomba ifunguliwe na kadhalika. Huko akakutana na Idriys (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Jibriyl akasema: “Huyu ni Idriys. Msalimie.” Akamsalimia na yeye akamrudishia salamu na kusema: “Karibu ndugu mwema na Mtume mwema.” Halafu akachukuliwa na Jibriyl na kumpeleka katika mbingu ya tano. Wakati walipofika, akaomba ifunguliwe na kadhalika. Huko akakutana na Haaruun bin ´Imraan (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ndugu yake na Muusa. Jibriyl akasema: “Huyu ni Haaruun. Msalimie.” Akamsalimia na yeye akamrudishia salamu na kusema: “Karibu ndugu mwema na Mtume mwema.” Kisha akachukuliwa na Jibriyl na kwenda katika mbingu ya sita. Wakati walipofika, akaomba ifunguliwe na kadhalika. Huko akakutana  na Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Jibriyl akasema: “Huyu ni Muusa. Msalimie.” Akamsalimia na yeye akamrudishia salamu na kusema: “Karibu ndugu mwema na Mtume mwema.” Baada ya kumpita, Muusa akaanza kulia. Akaambiwa: “Ni kipi kinachokuliza?” Akasema: “Nalia juu ya kijana aliyetumilizwa baada yangu ambaye Ummah wake utakuwa na watu wengi wataoingia Peponi kuliko Ummah wangu.”

Sababu ya Muusa kulia ilikuwa ni huzuni kwa fadhilah ambazo Ummah wake umezikosa, na si kwa sababu ya uhasidi juu ya Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kisha akachukuliwa na Jibriyl kumpeleka katika mbingu ya saba. Wakati walipofika, akaomba ifunguliwe na kadhalika. Huko akakutana na Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kipenzi wa hali ya juu wa Mwingi wa rehema. Jibriyl akasema: “Huyu ni Ibraahiym. Msalimie.” Akamsalimia na yeye akamrudishia salamu na kusema: “Karibu mtoto mwema na Mtume mwema.”

Jibriyl alimzungusha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa Mitume hawa ili kumuheshimisha na kuonyesha utukufu na ubora wake. Ibraahiym alikuwa ameegemeza mgongo wake katika Nyumba yenye kuamiriwa kwenye mbingu ya saba. Humo kila siku huingia Malaika elfu sabini kuswali na kufanya ´ibaadah. Pindi wanapotoka, hawarudi tena na siku ya kufuata huja Malaika wengine. Hakuna anayejua ni wangapi isipokuwa Allaah pekee.

Kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akapandishwa mkunazi wa mwisho. Ilikuwa imelemewa na uzuri na pambo la Allaah kwa kiasi cha kwamba hakuna yeyote awezae kusifia uzuri na pambo lake. Halafu Allaah akamfaradhishia swalah khamsini kwa siku, akaridhia na akajisalimisha nalo. Alipokuwa njiani yuwarudi akakutana na Muusa na akamwambia: “Mola Wako amewafaradhishia nini Ummah Wako?” Akasema: “Swalah khamsini kila siku.” Akasema: “Ummah wako hawatoweza hilo. Niliwajaribu watu kabla yako na nilitangamana na wana wa israaiyl kwa ukali nilivyoweza. Rudi kwa Mola Wako na umuombe awapunguzie Ummah wako. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Nikarudi na nikapunguziwa kumi.” Akaendelea kwenda kwa Mola Wake mpaka swalah za faradhi mwishowe zikabaki kuwa tano. Akanadi mwenye kunadi: “Nimeweka faradhi Yangu na nimewawepesishia waja Wangu.”

Katika usiku huu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia Peponi. Huko alikutana na kuba ya lulu na udongo wake ilikuwa miski. Hatimaye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akashuka mpaka alipofika Makkah karibu na wakati wa alfajiri na huko akaswali swalah ya Subh.[1]

[1] al-Bukhaariy (3207) na Muslim (162).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 126
  • Imechapishwa: 03/06/2020