69. Mtume (صلى الله عليه وسلم) Ametumwa ili kutahadharisha shirki na kulingania katika Tawhiyd

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah amemtuma ili kutahadharisha shirki na kulingania katika Tawhiyd. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ قُمْ فَأَنذِرْ وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ وَالرُّجْزَ فَاهْجُرْ وَلَا تَمْنُن تَسْتَكْثِرُ وَلِرَبِّكَ فَاصْبِرْ

”Ee uliyejigubika! Simama na uonye! Na Mola wako mtukuze! Na nguo zako zitwaharishe! Na masanamu epukana nayo! Na wala usifanye wema kwa ajili ya kutaraji kukithirishiwa! Na kwa ajili ya Mola wako subiri!” (al-Muddaththir 74 : 01-07)

“Simama na uonye” maana yake ni kutahadharisha shirki na kulingania katika Tawhiyd.

“Na Mola Wako mtukuze” maana yake amtukuze kwa Tawhiyd.

“Na nguo zako zitwaharishe” maana yake twaharisha matendo yako kutokamana na shirki.

“Na Masanamu epukana nayo” Kuyakata na kuyaacha, ina maana ya kuyaepuka na kujitenga nayo na watu wake.

MAELEZO

Allaah amemtuma ili kutahadharisha shirki na kulingania katika Tawhiyd – Bi maana akiwatahadharisha watu shirki na akiwalingania katika kumpwekesha Allaah (´Azza wa Jall) katika uola Wake, ´ibaadah Yake na majina na sifa Zake.

Ee uliyejigubika – Hapa anaambiwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Simama na uonye – Allaah (´Azza wa Jall) anamwamrisha Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asimame kidete na kwa uchangamfu kuwatahadharisha watu na shirki. Shaykh ameshazifasiri Aayah hizi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 123
  • Imechapishwa: 03/06/2020