1 – Hukumu ya kumposa

a) Ni haramu kumposa mwenye kukaa eda ya kurejelewa kwa uwazi au kwa kumwashiria. Kwa sababu yuko ndani ya hukumu ya wake. Kwa hiyo haijuzu kwa yeyote kumposa. Kwa sababu bado yuko katika ulinzi wa mume wake.

b) Ni haramu kumposa kwa uwazi ambaye anakaa eda isiyorejelewa na si haramu kumposa kwa kumwashiria. Amesema (Ta´ala):

وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا عَرَّضْتُم بِهِ مِنْ خِطْبَةِ النِّسَاءِ

“Wala si dhambi juu yenu katika ambayo mmedokezea ya kuposa wanawake hao.”[1]

Kwa uwazi ni kumuonyesha waziwazi kwamba unataka kumuoa. Kwa mfano kusema “Nataka kukuoa”. Pupa ya kutaka kuolewa inaweza kumfanya akasema kwamba eda yake imekwisha kabla kumalizika kikweli. Tofauti na kumwashiria ambaye hambainishii uwazi kwamba anataka kumuoa. Kwa hiyo ni jambo lisilopelekea katika madhara kutokana na vile inavyofahamisha Aayah tukufu.

Mfano wa kumwashiria ni kama kusema “Mimi namtaka mwanamke mfano wako”.

Inafaa kwa mwenye kukaa eda ambayo sio ya kurejelewa kujibu maashirio haya kwa njia ya yeye pia kuashiria. Si halali kwake kujibu kwa uwazi. Haijuzu kwa mwenye kukaa eda ya kurejelewa kumjibu mwenye kumposa; si kwa njia ya uwazi wala njia ya kuashiria.

2 – Ni haramu kwa mwanamke mwenye kukaa eda kufunga ndoa na mume mwengine. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تَعْزِمُوا عُقْدَةَ النِّكَاحِ حَتَّىٰ يَبْلُغَ الْكِتَابُ أَجَلَهُ

“Na wala msiazimie kufunga ndoa mpaka muda ulioandikwa Kishari´ah [katika eda] ufike mwisho wake.”[2]

Ibn Kathiyr amesema katika “Tafsiyr” yake:

“Bi maana haifai kufunga ndoa ndani ya eda mpaka imalizike. Wanachuoni wameafikiana juu ya kwamba ndoa haisihi ndani ya muda wa eda.”[3]

[1] 02:235

[2] 02:235

[3] (01/509).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 112-113
  • Imechapishwa: 27/11/2019