63. Mlango kuhusu ahadi za Allaah na Mtume Wake

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَوْفُواْ بِعَهْدِ اللّهِ إِذَا عَاهَدتُّمْ وَلاَ تَنقُضُواْ الأَيْمَانَ بَعْدَ تَوْكِيدِهَا وَقَدْ جَعَلْتُمُ اللّهَ عَلَيْكُمْ كَفِيلاً إِنَّ اللّهَ يَعْلَمُ مَا تَفْعَلُونَ

“Timizeni ahadi ya Allaah mnapoahidi na wala msivunje viapo baada ya kuvifunga na mmekwishamfanya Allaah kuwa ni mdhamini wenu; hakika Allaah anajua yale mnayoyafanya.” (an-Nahl 16:91)

2- Buraydah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anateua kiongozi kwa jeshi au kikosi, basi humuusia kumcha Allaah na kuwafanyia wema wale waislamu aliyo pamoja nao. Alikuwa akisema:

“Anzeni kupigana kwa jina la Allaah mpigane katika njia ya Allaah. Piganeni na kila mwenye kumkufuru Allaah, piganeni, msichukue kitu katika ngawira pasi na idhini, msivunje mkataba na wala msikatekate viungo vya maiti na wala msimuue mtoto. Ukikutana na adui wako katika washirikina mlinganie katika mambo matatu. Ikiwa atakubali kwa lolote katika haya matatu basi mkubalie na jizuie kumpiga vita. Mlinganie katika Uislamu. Akikukubalia hilo muitikie. Kisha mlinganie katika kuhama kutoka katika miji yao na kwenda katika miji ya Muhaajiruun na uwaambie ya kwamba ikiwa watafanya hivyo basi wana haki zote kama walizonazo Muhaajiruun na watakuwa na kama yale walionayo Muhaajiruun. Wakikataa kuhama kutoka katika miji yao waambieni ya kwamba watakuwa na hadhi kama ya mabedui wa Kiislamu na watapitishiwa hukumu ya Allaah (Ta´ala); hawatokuwa na haki yoyote ya ngawira wala fai isipokuwa ikiwa watapigana Jihaad bega kwa bega wakiwa pamoja na waislamu. Ikiwa watakataa waombeni kodi. Wakikubali wakubalieni na jizuieni kupigana nao. Ikiwa watakataa muombeni Allaah msaada na piganeni nao. Utapowazingira watu waliomo ngomeni na wakakutaka ufunge nao mkataba wa Allaah na mkataba wa Mtume Wake, basi usifunge mkataba wa Allaah na mkataba wa Mtume Wake. Lakini badaba yake funga nao mkataba wako wewe na mkataba wa Maswahabah wako. Kwani hakika mtapotaka kuvunja mikataba yenu na mikataba ya Maswahabah wenu ni jambo jepesi kuliko kuvunja mkataba wa Allaah na mkataba Mtume Wake. Utapowazingira watu waliomo ngomeni na wakakutaka uwateremshe katika hukumu ya Allaah, usiwateremshe katika hukumu ya Allaah. Lakini badala yake wateremshe kwa hukumu yako. Kwani hakika hujui utapatia kwao hukumu ya Allaah au hapana.”[1]

Ameipokea Muslim.

MAELEZO

Mlango unahusu kuadhimisha ahadi ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Unatahadharisha vilevie kuitumia vibaya na kuifunga baina ya watu kwa sababu kufanya hivo kunaweza kupelekea ikatumiwa vibaya. Ni wajibu kwa watawala wasivunge ahadi ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kati ya watu. Badala yake wafunge kwa jina la maraisi, wafalme au watu wao. Huku ni kwa sababu ya kuadhimisha ahadi ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni katika kukamilisha Tawhiyd na imani. Kuvunja ahadi kama hii ni jambo linaipunguza Tawhiyd na ni njia inayopelekea ikachezewa.

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَوْفُواْ بِعَهْدِ اللّهِ إِذَا عَاهَدتُّمْ وَلاَ تَنقُضُواْ الأَيْمَانَ بَعْدَ تَوْكِيدِهَا وَقَدْ جَعَلْتُمُ اللّهَ عَلَيْكُمْ كَفِيلاً إِنَّ اللّهَ يَعْلَمُ مَا تَفْعَلُونَ

“Timizeni ahadi ya Allaah mnapoahidi na wala msivunje viapo baada ya kuvifunga na mmekwishamfanya Allaah kuwa ni mdhamini wenu; hakika Allaah anajua yale mnayoyafanya.”

Yule mwenye kufunga mkataba kwa jina la Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi ni lazima atekeleze. Japokuwa atakuwa amekosea kufunga mkataba kwa jina la Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lakini pamoja na hivyo ni lazima atekeleze. Haifai kwake akaivunja:

وَأَوْفُواْ بِعَهْدِ اللّهِ إِذَا عَاهَدتُّمْ وَلاَ تَنقُضُواْ الأَيْمَانَ بَعْدَ تَوْكِيدِهَا وَقَدْ جَعَلْتُمُ اللّهَ عَلَيْكُمْ كَفِيلاً إِنَّ اللّهَ يَعْلَمُ مَا تَفْعَلُونَ

“Timizeni ahadi ya Allaah mnapoahidi na wala msivunje viapo baada ya kuvifunga na mmekwishamfanya Allaah kuwa ni mdhamini wenu; hakika Allaah anajua yale mnayoyafanya.”

Msivunje ahadi baada ya kuwa mmeshaifunga kwa viapo vikali. Timizeni kama alivyosema (Subhaanah):

وَأَوْفُوا بِالْعَهْدِ ۖ إِنَّ الْعَهْدَ كَانَ مَسْئُولًا

“Timizeni ahadi; hakika ahadi itakuwa ni yenye kuulizwa.” (al-Israa´ 17:34)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila mdanganyifu atakuwa na bendera siku ya Qiyaamah na itasemwa: “Huu ni udanganyifu wa fulani mwana wa fulani.”[2]

Haya ni matishio makali ambayo yanafahamisha kwamba ni lazima kutekeleza ahadi.

2- Buraydah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anateua kiongozi kwa jeshi au kikosi, basi humuusia kumcha Allaah na kuwafanyia wema wale waislamu aliyo pamoja nao. Alikuwa akisema:

“Anzeni kupigana kwa jina la Allaah mpigane katika njia ya Allaah. Piganeni na kila mwenye kumkufuru Allaah, piganeni, msichukue kitu katika ngawira pasi na idhini, msivunje mkataba na wala msikatekate viungo vya maiti na wala msimuue mtoto. Ukikutana na adui wako katika washirikina mlinganie katika mambo matatu. Ikiwa atakubali kwa lolote katika haya matatu basi mkubalie na jizuie kumpiga vita. Mlinganie katika Uislamu. Akikukubalia hilo muitikie. Kisha mlinganie katika kuhama kutoka katika miji yao na kwenda katika miji ya Muhaajiruun na uwaambie ya kwamba ikiwa watafanya hivyo basi wana haki zote kama walizonazo Muhaajiruun na watakuwa na kama yale walionayo Muhaajiruun. Wakikataa kuhama kutoka katika miji yao waambieni ya kwamba watakuwa na hadhi kama ya mabedui wa Kiislamu na watapitishiwa hukumu ya Allaah (Ta´ala); hawatokuwa na haki yoyote ya ngawira wala fai isipokuwa ikiwa watapigana Jihaad bega kwa bega wakiwa pamoja na waislamu. Ikiwa watakataa waombeni kodi. Wakikubali wakubalieni na jizuieni kupigana nao. Ikiwa watakataa muombeni Allaah msaada na piganeni nao. Utapowazingira watu waliomo ngomeni na wakakutaka ufunge nao mkataba wa Allaah na mkataba wa Mtume Wake, basi usifunge mkataba wa Allaah na mkataba wa Mtume Wake. Lakini badaba yake funga nao mkataba wako wewe na mkataba wa Maswahabah wako. Kwani hakika mtapotaka kuvunja mikataba yenu na mikataba ya Maswahabah wenu ni jambo jepesi kuliko kuvunja mkataba wa Allaah na mkataba Mtume Wake. Utapowazingira watu waliomo ngomeni na wakakutaka uwateremshe katika hukumu ya Allaah, usiwateremshe katika hukumu ya Allaah. Lakini badala yake wateremshe kwa hukumu yako. Kwani hakika hujui utapatia kwao hukumu ya Allaah au hapana.”

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mlinganie katika Uislamu.”

Kabla ya kila kitu walinganie kwanza katika shahaadah mbili. Kama ambavyo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyomwamrisha Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh) wakati alipomtuma Yemen. Wakikubali shahaadah mbili na wakaitamka, ndipo uwafunze faradhi zengine.

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… uwateremshe katika hukumu ya Allaah.”

Katika maamrisho na makatazo.

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… waombeni kodi.”

Bi maana pale watapokataa kuingia katika Uislamu na wakakataa kuhama. Haya yanahusiana na mayahudi, manaswara na majusi. Allaah (Ta´ala) amesema:

قَاتِلُوا الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَلَا بِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَلَا يُحَرِّمُونَ مَا حَرَّمَ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَلَا يَدِينُونَ دِينَ الْحَقِّ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حَتَّىٰ يُعْطُوا الْجِزْيَةَ عَن يَدٍ وَهُمْ صَاغِرُونَ

“Pambaneni na wale wasiomwamini Allaah na wala siku ya Mwisho na wala hawaharamishi aliyoyaharamisha Allaah na Mtume Wake na wala hawaiamini na kuifuata dini ya haki katika wale waliopewa Kitabu – [pambaneni nao] mpaka watoe kodi kwa khiyari wakiwa ni wenye kudhalilika.” (at-Tawbah 09:29)

Sunnah imetaja watu ambao wanatakiwa kutoa kodi kwa kutokufungamanisha na Qur-aan  imetaja kwa kufungamanisha mayahudi na manaswara. Sunnah imewafanya majusi wawe na hukumu hiyohiyo inapokuja katika kodi na si katika vichinjwa na wanawake.

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… muombeni Allaah msaada na piganeni nao.”

Hii ni dalili inayoonyesha kuwa ni wajibu kumtaka msaada Allaah. Muumini anatakiwa kumtaka msaada Allaah wakati wa kupambana na maadui Wake na wala asitegemee nguvu zake mwenyewe.

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Utapowazingira watu waliomo ngomeni… “

Mayahudi na manaswara walikuwa mara nyingi wakiwa katika ngome. Hawakuwa pamoja na mabedui huko jangwani.

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… wakakutaka ufunge nao mkataba wa Allaah na mkataba wa Mtume Wake… “

Ni wajibu kwa waislamu kutovunja ahadi na mkataba. Vilevile wasifunge ahadi kwa jina la Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu ni sahali kuvunja ahadi kwa majina yao kuliko kwa jina la Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata kama matendo yote mawili hayafai, lakini baadhi ya shari na madhambi ni makubwa kuliko mengine.

Vivyo hivyo wasikubali kuhukumiwa kwa mujibu wa hukumu ya Allaah wakiomba hilo. Badala yake anatakiwa kuwahukumu kwa mujibu wa hukumu ya wafuasi wake. Ni sawa akasema kuwa atafanya kila aliwezalo kuhukumu kwa mujibu wa Shari´ah inavosema, lakini asisemi ni kwa mujibu wa hukumu ya Allaah kwa sababu anaweza kukosea. Awawekee ijitahidi zake kwa mujibu wa vile Shari´ah inavosema. Kwa sababu akikosea anakuwa amemsemea uongo Allaah. Kitendo hichi ni kwa sababu ya usalama na ni kwa sababu ya adabu ya Kishari´ah katika kufunga mikataba na ahadi na kumhukumu adui kwa njia inayomridhisha Allaah (Ta´ala).

[1] Muslim (1731).

[2] al-Bukhaariy (1735).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 175-177
  • Imechapishwa: 14/11/2018