Kucheza shere na dini ni kuritadi kutoka katika Uislamu na kutoka nje ya dini kikamilifu. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?”  Msitoe udhuru; mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.”[1]

Aayah hii inafahamisha kwamba kucheza shere na Allaah ni kufuru, kucheza shere na Mtume ni kufuru na kwamba kucheza shere na Aayah za Allaah ni kufuru. Mwenye kucheza shere na moja katika vitu hivi basi ni mwenye kucheza shere na vyote. Yaliyowatokea wanafiki hawa ni kwamba walicheza shere na Mtume na Maswahabah zake. Ndipo ikateremka Aayah hii. Kwa hivyo kucheza shere na mambo haya ni vitu vyenye kwenda sambamba. Wale wanaoidogesha Tawhiyd ya Allaah (Ta´ala) na wakati huohuo wanaadhimisha kuombwa asiyekuwa Yeye katika wafu na pindi wanapoamrishwa Tawhiyd na wakakatazwa shirki wanalidogesha jambo hilo, kama alivosema (Ta´ala):

وَإِذَا رَأَوْكَ إِن يَتَّخِذُونَكَ إِلَّا هُزُوًا أَهَـٰذَا الَّذِي بَعَثَ اللَّـهُ رَسُولًا إِن كَادَ لَيُضِلُّنَا عَنْ آلِهَتِنَا لَوْلَا أَن صَبَرْنَا عَلَيْهَا

“Wanapokuona hawakuchukulii vyengine isipokuwa mzaha [huku wakisema]: “Je, ndiye huyu ambaye Allaah amemtuma kuwa Mtume?” Kwa hakika amekaribia kutupoteza na waungu wetu, ingelikuwa hatukuwa na uvulimivu kuwaabudu.”[2]

Wakamfanyia mzaha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipowakataza shirki. Bado washirikina ni wenye kuendelea kuwakejeli Mitume na wanawasifu upumbavu, upotevu na wendawazimu pindi wanapowalingania katika Tawhiyd kutokana na yale yanayopatikana ndani ya nafsi zao katika kuiadhimisha shirki. Vivyo hivyo utawaona walivyo wale wenye kufanana na wao. Pindi wanapomuona anayelingania katika Tawhiyd basi wanamfanyia mzaha kutokana na ile shirki waliyomo. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَتَّخِذُ مِن دُونِ اللّهِ أَندَاداً يُحِبُّونَهُمْ كَحُبِّ اللّهِ

”Wapo katika watu ambao wanafanya badala ya Allaah washirika [na] wanawapenda kama mapenzi [yapasavyo] ya kumpenda Allaah.”[3]

Mwenye kumpenda kiumbe mfano wa vile anavompenda Allaah ni mshirikina. Ni lazima watu watofautishe kati ya kupenda kwa ajili ya Allaah na kupenda pamoja na Allaah. Hawa ambao wameyafanya makaburi masanamu utawaona wanafanya mzaha na mambo ambayo yanahusiana na kumpwekesha na kumwabudu Allaah, wanawaadhimisha wale waliojifanyia waombezi badala ya Allaah, baadhi yao wanaapa kiapo cha uongo kwa kutumia jina la Allaah na hawathubutu kuapa kiapo cha uongo kwa kutumia jina la Shaykh wao. Makundi mengi yaliyotapakaa utamuona mmoja wao kumtaka uokozi Shaykh wake – ima kwenye kaburi lake au mbali na kaburi lake – anaona kuwa ni jambo lenye kumnufaisha zaidi kuliko kumuomba Allaah msikitini katika nyakati za alfajiri na anamchezea shere yule mwenye kwenda kinyume na mwenendo wake kuielekea Tawhiyd. Wengi wao wanaiharibu misikiti na wanaimarisha sehemu wanapojengea makaburi. Je, hii ina maana gani kama sio kumdharau Allaah, Aayah Zake na Mitume Yake na kuiadhimisha kwao shirki[4]? Haya yanatokea mara nyingi sana hii leo kwa watu wa makaburi.

[1] 09:65-66

[2] 25:41-42

[3] 02:165

[4] Majmuu´-ul-Fataawaa (15/48-49).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 117-118
  • Imechapishwa: 24/03/2020