61. Mlango kuhusu picha


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (Ta´ala) amesema: “Ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule ambaye anajaribu kuumba mfano wa viumbe Wangu? Hebu waumbe mdudu chungu, waumbe punje ya nafaka au waumbe chembe ya shayiri.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

2- Wamepokea vilevile kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu watakaokuwa na adhabu kali siku ya Qiyaamah ni wale wanaomuiga Allaah katika uumbaji Wake.”[2]

3- Wamepokea pia kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesimulia ya kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Kila mtengeneza picha atakuwa Motoni. Ataifanya kila picha aliyoitengeneza kuwa na nafsi ambapo ataadhibiwa kwayo Motoni.”[3]

Wamepokea tena ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayetengeneza picha duniani atakalifishwa kuipulizia roho, jambo ambalo hatoweza.”[4]

Muslim amepokea kutoka kwa Abul-Hayyaaj ambaye ameeleza kwamba ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) alimwambia:

“Hivi nisikutume juu ya kazi aliyonituma kwayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Usiache picha hata moja isipokuwa umeiharibu wala kaburi lililoinuka isipokuwa umelisawazisha.”[5]

MAELEZO

Alichokusudia mwandishi kwa kuweka mlango huu ni kwamba picha ni miongoni mwa madhambi makubwa yanayoitia dosari Tawhiyd na yanaweza kumsababishia yule mfanyaji kupata ghadhabu za Allaah na kutumbukia Motoni na imani kupungua na kudhoofika. Watengeneza picha ni wale wanaoigiza uumbaji wa Allaah kwa njia ya kutengeneza picha za wanyama sawa kwa kutumia mkono au kwa kutumia nyenzo nyingine yoyote.

1- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (Ta´ala) amesema: “Ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule ambaye anajaribu kuumba mfano wa viumbe Wangu? Hebu waumbe mdudu chungu, waumbe punje ya nafaka au waumbe chembe ya shayiri.”

Swali hili limeulizwa kwa njia ya makanusho. Kwa msemo mwingine ni kwamba hakuna ambaye ni dhalimu zaidi kuliko huyu mtengeneza mapicha. Makusudio ya Hadiyth ni kutahadharisha kutokamana na kitendo hichi. Usulubu kama huu umekuja sehemu nyingi katika Qur-aan ikiwa ni pamoja na maneno Yake (Ta´ala):

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أَوْ كَذَّبَ بِآيَاتِهِ ۗ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الظَّالِمُونَ

“Ni nani mdhalimu zaidi kuliko yule aliyemzulia Allaah uongo au anayekadhibisha alama Zake? Hakika madhalimu hawatofaulu.” (al-An´aam 06:21)

Allaah amesema:

“… kuliko yule ambaye anajaribu kuumba mfano wa viumbe Wangu?”

Bi maana anatengeneza picha kama picha Yangu. Kama kweli wana uwezo wa kufanya hivo, basi:

“Hebu waumbe mdudu chungu … “

Waache waumbe mdudu chungu akiwa na sifa zake za kawaida kama vile usikizi, kutembea na nyenginezo. Pamoja na kipimo chake ni kiumbe wa ajabu mno:

“… waumbe punje ya nafaka.”

Waache waumbe punje ya nafaka au shayiri ikiwa na sifa zake za kawaida kama kumea, kuwanufaisha watu na nyenginezo. Ni vipi wataweza kuumba kiumbe kilicho na uhai ikiwa hawawezi kuumba kiumbe kisichokuwa na uhai na kumea?

3- Wamepokea pia kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesimulia ya kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Kila mtengeneza picha atakuwa Motoni. Ataifanya kila picha aliyoitengeneza kuwa na nafsi ambapo ataadhibiwa kwayo Motoni.”

Wanachuoni wote wamekubaliana juu ya kwamba kutengeneza picha za viumbe vyenye roho kwa njia ya masanamu vinyago ni katika madhambi makubwa. Ikiwa sio kwa njia ya masanamu vinyago, kama vile kuchora kuta, vibao na nguo, baadhi ya wanafunzi wa Maswahabah wamejuzisha hilo. Hata hivyo wale maimamu wane na wanachuoni wengi wamekubaliana juu kwamba picha hizo pia zimeharamishwa na kwamba zina hukumu moja kama vile picha zenye kivuli. Maoni haya ndio sahihi zaidi kwa sababu Hadiyth ni zenye kuenea na zimekusanya zile picha za masanamu vinyago na zisizokuwa hivo na zimejumuisha pia zile picha za kisasa na nyenginezo. Miongoni mwa dalili zinazofahamisha kuwa hukumu ni yenye kuenea ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku moja wakati alipokuja kwa ´Aaishah na akaona picha kwenye pazia zake alighadhibika. Akasema:

“Hakika watu wa picha hizi ni wenye kuadhibiwa siku ya Qiyaamah na wataambiwa: “Vipeni uhai vile mlivyoviumba!”[6]

Katika pazia hakuna masanamu vinyago.

Picha za kisasa zina hukumu moja. Dalili ya hilo ni yale yaliyotokea ile siku ya ufunguzi wa mji wa Makkah ambapo Usamaah (Radhiya Allaahu ´anh) alimletea maji Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akayafutia mapicha kutoka kwenye Ka´bah. Ni wajibu kutahadhari na hilo. Muislamu anatakiwa kujiepusha na madhambi haya. Ni wajibu kuziondosha na kuziharibu.

Muslim amepokea kutoka kwa Abul-Hayyaaj ambaye ameeleza kwamba ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) alimwambia:

“Hivi nisikutume juu ya kazi aliyonituma kwayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Usiache picha hata moja isipokuwa umeiharibu wala kaburi lililoinuka isipokuwa umelisawazisha.”

Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikataza kuyajengea makaburi kwa sababu ni jambo linalopelekea katika shirki. Kadhalika picha zinapelekea katika shirki. Kwa ajili hii shirki ilitokea wakati wa Nuuh (´alayhis-Salaam) kwa sababu ya mapicha.

Kuhusu yale mahitajio ya watu ya picha hii leo, zinatakiwa kutumiwa wakati wa kutenzwa nguvu tu na wakati wa haja. Kwa njia hiyo mtu anayafanya hali ya kuwa si mwenye kupenda kwake mwenyewe. Mfano wa picha hizo ni kama zile zinazotumiwa katika vyeti vya vitambulisho.

Picha zinawazuia Malaika kuingia katika nyumba, kama ilivyofahamisha hivo Haidyth Swahiyh[7]. Kunavuliwa katika hayo zile picha zenye kutwezwa. Picha kama hizi haifai kuzitengeneza, japokuwa ni zenye kutwezwa, lakini haziwazuii Malaika kuingia katika nyumba. Mfano wa picha hizo ni zile zinazokuwa katika magodoro. Kadhalika mbwa ya ulinzi na mbwa ya kuelekeza njia haziwazuii Malaika kuingia katika nyumba kwa sababu zimeruhusiwa. Kwa hiyo mtu akinunua godoro lililo na picha na akalilalia, haina neno kwa sababu ni lenye kutwezwa na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Uharamu ni wenye kuhusu pia zile picha za wale wapambanaji wa kiafghanistani. Jihaad inakuwa pasi na picha. Wala haitakikani kuwachukua video camera.

Kuwaning´iniza wanyama juu ni jambo halitakikani. Huku ni kuharibu mali bila faida yoyote. Baadhi wanaweza vilevile kutumia hoja kwamba mnyama ni picha pia. Kuna khatari vilevile baadhi wakaanza kuitakidi imani mbovu juu ya mnyama huo na kwamba anawazuia majini na mfano wa hayo.

Makatazo katika Hadiyth ni yenye kujumuisha vilevile picha kwa madhumuni ya mafunzo na mengineyo.

[1] al-Bukhaariy (5953) na (7559) na Muslim (2111).

[2] al-Bukhaariy (5954) na Muslim (2107).

[3] Muslim (2110).

[4] al-Bukhaariy (5963) na Muslim (2110).

[5] Muslim (969).

[6] al-Bukhaariy (2105) na Muslim (2107).

[7] al-Bukhaariy (3322) na Muslim (2106).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 168-170
  • Imechapishwa: 14/11/2018