Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

… Malaika Wake…

MAELEZO

Malaika ni viumbe visivyoonekana wanaomuabudu Allaah (Ta´ala). Hawana kitu chochote katika uola wala uungu. Allaah (Ta´ala) amewaumba kwa nuru. Akawapa unyenyekevu mkamilifu juu ya maamrisho Yake pamoja na nguvu za kuyatekeleza. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَنْ عِندَهُ لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ وَلَا يَسْتَحْسِرُونَ يُسَبِّحُونَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لَا يَفْتُرُونَ

“Na wale walio Kwake hawatakabari na ‘ibaadah Yake na wala hawachoki. Wanasabihi usiku na mchana, wala hawazembei.” (al-Anbiyaa´ 21 : 19-20)

Wako idadi kubwa na hakuna anayeijua isipokuwa Allaah (Ta´ala) peke yake.  Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kutoka katika Hadiyth ya Anas (Radhiya Allaahu ´anh) kuhusiana na kisa cha Mi´raaj:

“Nyumba iliyojaa ilinyanyuliwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndani yake kila siku wanaswali Malaika 70.000. Pindi wanapotoka, hawarudi tena.”[1]

Kuamini Malaika kunakusanya mambo manne:

1- Kuamini uwepo wao.

2- Kuamini wale tunaowajua kwa majina yao. Kwa mfano wa Jibriyl. Ama wale tusiowajua majina yao, tunatakiwa kuwaamini kwa njia ya jumla.

3- Kuamini sifa zao tunazozijua. Kwa mfano sifa ya Jibriyl. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza ya kwamba amemuona katika umbile lake la kihakika na alikuwa na mbawa mia sita zinazofunika upeo wa macho.

Kutokana na amri ya Allaah Malaika anaweza kujigeuza katika umbile la mtu. Mfano wa hilo ni pale ambapo alimtuma (Ta´ala) Jibriyl kwa Maryam katika umbile la mtu mkamilifu. Mfano mwingine ni pale alipoenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali ya kuwa alikuwa amekaa na Maswahabah zake. Alikuja katika umbile la mtu ambaye alikuwa amevaa mavazi meupe mno na nywele nyeusi mno. Hakuna kilichokuwa kinaashiria kuwa alikuwa ni msafiri na hakuna yeyote katika Maswahabah aliyekuwa akimjua. Akakaa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akaweka magoti yake karibu na magoti yake na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake. Halafu akamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Uislamu, Imani na Ihsaan, Qiyaamah na alama zake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamjibu na kisha akaondoka zake. Baada ya hapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Ilikuwa ni Jibriyl amewajia ili akufunzeni dini yenu.”[2]

Imepokelewa na Muslim.

Kadhalika inahusiana na Malaika ambao walitumwa na Allaah (Ta´ala) kwa Ibraahiym na Luutw. Wao pia walikuwa katika umbile la wanamme.

4- Kaumini kazi zao tunazozijua. Kazi hizi wanazifanya kwa maamrisho ya Allaah (Ta´ala). Mfano wa hayo ni kwamba wanamsibihi na wanamwabudu usiku na mchana pasi na uvivu wala kuchoka. Baadhi yao wana kazi maalum.

Kazi ya Jibriyl mwaminifu ni kufikisha Wahy wa Allaah (Ta´ala) kwa Manabii na Mitume.

Kazi ya Mikaaiyl amewakilishwa kwa ajili ya mvua na mazao.

Kazi ya Israafiyl amewakilishwa kupuliza parapanda wakati Qiyaamah kitaposimama na kufufuliwa.

Kazi ya Malaika wa mauti amewakilishwa kutoa roho wakati wa kufa.

Kazi ya Maalik amewakilishwa kuchunga Moto.

Kuna Malaika pia ambao wamewakilishwa kuwahudumia watoto waliomo tumboni mwa mama zao. Kipomoko kinapofikisha miezi minne tumboni mwa mama yake, basi Allaah hukitumia Malaika na kumuamrisha kuandika riziki yake, muda wake wa kuishi, matendo yake na kama atakuwa mwovu au mwema.

Kuna Malaika ambao kazi yao wamewakilishwa kuyadhibiti na kuyaandika matendo ya wanadamu. Ni Malaika wawili; mmoja yuko kuliani na mwingine kushotoni.

Kuna Malaika ambao kazi yao wamewakilishwa kumhoji yule maiti. Pindi anapowekwa maiti kwenye kaburi lake, basi anajiwa na Malaika wawili na kumuuliza kuhusu Mola Wake, dini yake na Mtume wake.

Kuwaamini Malaika kunazalisha matunda yafuatayo:

1- Ujuzi juu ya ukubwa wa Allaah (Ta´ala), nguvu Zake na ufalme Wake. Ukubwa wa viumbe unaashiria ukubwa wa Muumba.

2- Kumshukuru Allaah (Ta´ala) kwa kumtunza mwanadamu kwa kule kumuwakilishia yeye Malaika hawa ambao wanamuhifadhi, kuyaandika matendo yao na mengineyo katika manufaa yao.

3- Mapenzi kuwapenda Malaika kwa ile ´ibaadah wanayomfanyia Allaah (Ta´ala).

Watu wapotevu wamekanusha Malaika kuwa na miili. Badala yake wanasema kuwa wao ni ibara ya nguvu ilio nyuma ya wema uliojificha kwa viumbe. Nadharia hii inakadhibisha Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya waislamu. Allaah (Ta´ala) amesema:

الْحَمْدُ لِلَّـهِ فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ جَاعِلِ الْمَلَائِكَةِ رُسُلًا أُولِي أَجْنِحَةٍ مَّثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ

“Sifa zote njema ni za Allaah Muumbaji wa mbingu na ardhi, Mwenye kuwafanya Malaika kuwa ni wajumbe wenye mbawa mbilimbili na tatutatu na nnenne.” (Faatwir 35 : 01)

وَلَوْ تَرَىٰ إِذْ يَتَوَفَّى الَّذِينَ كَفَرُوا ۙ الْمَلَائِكَةُ يَضْرِبُونَ وُجُوهَهُمْ وَأَدْبَارَهُمْ وَذُوقُوا عَذَابَ الْحَرِيقِ

“Na lau mgeliona pale Malaika wanapowafisha wale waliokufuru wanawapiga nyuso zao na migongo yao na [wanawaambia]: “Onjeni adhabu iunguzayo.” (al-Anfaal 08 : 50)

وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الظَّالِمُونَ فِي غَمَرَاتِ الْمَوْتِ وَالْمَلَائِكَةُ بَاسِطُو أَيْدِيهِمْ أَخْرِجُوا أَنفُسَكُمُ

“Na lau ungeliwaona madhalimu pale wakiwa katika mahangaiko ya mauti na Malaika wamenyosha mikono yao [wakiwaambia]: “Zitoeni nafsi zenu!” (al-An´aam 06 : 93)

حَتَّىٰ إِذَا فُزِّعَ عَن قُلُوبِهِمْ قَالُوا مَاذَا قَالَ رَبُّكُمْ ۖ قَالُوا الْحَقَّ ۖ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ

”Mpaka itakapoondolewa fazaiko nyoyoni mwao [baada ya kuzimia]; watasema [wakiulizana]: “Amesema nini Mola wenu?” – waseme: “Ya haki; Naye yujuu, Mkubwa kabisa.” (Sabaa´ 34:23)

وَالْمَلَائِكَةُ يَدْخُلُونَ عَلَيْهِم مِّن كُلِّ بَابٍ سَلَامٌ عَلَيْكُم بِمَا صَبَرْتُمْ ۚ فَنِعْمَ عُقْبَى الدَّارِ

“Na Malaika wanawaingilia katika kila milango  [na huku wakisema]: “Amani iwe juu yenu kwa yale mliyosubiri. Basi uzuri ulioje hatima nzuri ya makazi!” (ar-Ra´d 13 : 23-24)

Katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wakati Allaah anapompenda mja, basi humwita Jibriyl: “Hakika Allaah anampenda mtu fulani; hivyo na wewe mpende.” Jibriyl akaanza kumpenda na halafu akanadi kwa watu wa mbinguni: “Allaah anampenda mtu fulani; hivyo nanyi mpendeni.” Basi hupendwa na watu wa mbinguni na halafu baada ya hapo akawa ni mwenye kukubalika katika ardhi.”[3]

Vilevile imepokelewa kutoka kwake aliyesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Inapokuwa siku ya ijumaa basi katika kila mlango wa msikiti kunakuwa Malaika wanaoandika wale wahudhuriaji. Imamu akishaketi chini, basi wanafunga madaftari yao na kusikiliza ukumbusho.”[4]

Maandiko haya yanasema wazi kabisa kwamba Malaika wana viwiliwili vya kikweli na sio ibara ya nguvu fulani, kama wanavyosema baadhi ya wapotevu. Haya ndiyo yanayosemwa na maandiko na maafikiano ya waislamu.

[1] al-Bukhaariy (3207), Muslim (259) na an-Nasaa’iy (447).

[2] Muslim (08).

[3] al-Bukhaariy (3209), Muslim (2637), at-Tirmidhiy (3372), Maalik (1778) na Ahmad (2/267).

[4] al-Bukhaariy (3211), Muslim (850), an-Nasaa´iy (1384), Ibn Maajah (1092), ad-Daarimiy (1544) na Ahmad (2/239).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 90-94
  • Imechapishwa: 01/06/2020