6. Matahadharisho ya kukaa na Ahl-ul-Bid´ah


Miongoni mwa misingi ya Sunnah ni:

“… kuepuka kukaa na Ahl-ul-Ahwaa´…”

Kwa sababu kukaa na Ahl-ul-Ahwaa´ mara nyingi kunasababisha kupinda kwa moyo. Watu wengi hudanganyika na elimu na upeo wa akili alionayo ambapo wanachanganyika na Ahl-ul-Bid´ah. Hapo ndipo Allaah huwaacha wakajimalizia nayo wenyewe ambapo hutumbukia katika upotevu. Huu ndio uhakika wa mambo. Imaam Ibn Battwah (Rahimahu Allaah) ameashiria hilo pindi aliposema:

“Tunawajua watu waliokuwa wakiwatukana na kuwalaani Ahl-ul-Bid´ah. Halafu pale walipoanza kukaa na kutangamana nao wakawa kama wao.”

Huu ndio uhakika wa mambo katika kila wakati na kila mahali. Kuna baadhi ya watu wakubwa walijidanganya wao wenyewe na hapo wakawa wametumbukia katika Bid´ah. Sitaki kuwataja. Wanafunzi wanajua ni kina nani. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“… kuepuka kukaa na Ahl-ul-Ahwaa´…”

Dalili ya hilo:

وَإِذَا رَأَيْتَ الَّذِينَ يَخُوضُونَ فِي آيَاتِنَا فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ

“Unapowaona wale wanaoziingilia Aayah Zetu, basi jitenge nao mpaka waingie kwenye mazungumzo mengineyo.”[1]

Usikae nao. Watu hawa wanakiingilia Kitabu cha Allaah na wanazungumza juu ya Allaah pasi na elimu. Bid´ah imejengwa juu watu wanazungumza kuhusu dini na Kitabu cha Allaah pasi na elimu na wananasibisha batili hii na Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndio maana ni wajibu kujitenga nao mbali. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kama tulivosema:

“Mkiwaona wale wenye kufuata Aayah zisizokuwa wazi, basi mjue kuwa hao ndio wale ambao Allaah amewaleza. Hivyo tahadharini nao.”

“Katika zama za mwisho kutakuja watu na mambo ambao hamyajui nyinyi wala baba zenu. Ninakutahadharisheni nao.”[2]

Hii ni dalili nyingine yenye kutahadharisha kukaa na Ahl-ul-Bid´ah.

Ikiwa una elimu na unaweza kubainisha mambo, walinganie katika haki wajinga na wale waliodanganyika na uwawekee mambo wazi. Ama kukaa nao kwa njia ya kupakana mafuta, urafiki, mapenzi na kuchanganyika nao, hili ni kosa lenye kupelekea katika upotevu. Inatakiwa kwa yule mwenye busara kuepuka mambo kama hayo. Maswahabah walitahadharisha mambo hayo. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) na maimamu wa waliokuja baada ya Maswahabah kama Ayyuub as-Sikhtiyaaniy na Ibn Siriyn (Rahimahumu Allaah). Walikuwa hawawasikilizi watu wa Bid´ah hata kama atataka kumsomea Hadiyth au Aayah moja. Walipoulizwa ni kwa sababu gani wakasema kuwa wanaogopa kufikwa na fitina isiyoponeka. Hakuna kitu kilicho sawa na usalama. Mtu asijiweke mwenyewe katika fitina na khaswa ikiwa anajijua mwenyewe kuwa ni mdhaifu.

[1] 06:68

[2] Muslim (6).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 368-369
  • Imechapishwa: 09/04/2017