6. Hakuna manasibisho yasiyokuwa ya Kiislamu

Allaah (Ta´ala) amesema:

هُوَ سَمَّاكُمُ الْمُسْلِمِينَ مِن قَبْلُ وَفِي هَـٰذَا

“Yeye Ndiye hapo kabla [katika Vitabu vya awali] na katika [Kitabu] hiki aliyekuiteni “waislamu”.” (22:78)

al-Haarith al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninakuamrisheni mambo matano ambayo Allaah ameniamrisha kwayo; usikivu, utiifu, Jihaad, Hijrah na mkusanyiko. Hakika yule mwenye kuacha mkusanyiko kiasi cha shibri basi amevua kamba ya Uislamu kutoka shingoni mwake isipokuwa ikiwa kama atajirudi. Mwenye kuita wito wa kipindi cha kikafiri ataadhibiwa Motoni.” Mtu mmoja akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hata kama ataswali na kufunga?” Akajibu: “Hata kama ataswali na kufunga. Enyi waja wa Allaah! Iteni kwa wito wa Allaah; Yeye ndiye kakwiteni “waislamu” na “waumini”.”[1]

Ameipokea Ahmad na at-Tirmidhiy ambaye amesema:

“Hadiyth ni Hasan na Swahiyh.”

Kumepokelewa [Hadiyth] Swahiyh ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kuacha mkusanyiko kiasi cha shibri na akafa, amekufa kifo cha kipindi cha kikafiri.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema pia:

“Mnaita wito wa kipindi cha kikafiri ilihali niko kati yenu?”

Abul-´Abbaas amesema:

“Kila jina lenye kwenda kinyume na Uislamu na Qur-aan katika manasibisho ya ukoo, miji, makabila, madhehebu au mifumo ni katika sifa za kipindi cha kikafiri. Pindi mtu wa Muhaajiruun alipozozana na mtu wa Answaar na kila mmoja akawaita watu wake, ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Mnaita wito wa kipindi cha kikafiri ilihali niko kati yenu?”

Akaghadhibika sana kutokana na hilo.”[2]

[1] Ahmad (4/130), at-Tirmidhiy (2863), Ibn Hibbaan (14/125), Ibn Khuzaymah (3/195) na wengineo.

[2] as-Siyaasah ash-Shar´iyyah (1/82).

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwl-ul-Islaam, uk. 19-22
  • Imechapishwa: 23/10/2016