3- Mawili hayo ni kudai kujua elimu ya mambo yaliyofichikana na kuyajua mambo yaliyofichikana. Kama mfano wa kuelezea yatayotokea ardhini, yatapotokea na ni wapi kipo kitu kilichopotea. Hayo ni kwa njia ya kuwatumia mashaytwaan ambao wanaiba usikizi kutoka mbinguni. Amesema (Ta´ala):

هَلْ أُنَبِّئُكُمْ عَلَىٰ مَن تَنَزَّلُ الشَّيَاطِينُ تَنَزَّلُ عَلَىٰ كُلِّ أَفَّاكٍ أَثِيمٍ يُلْقُونَ السَّمْعَ وَأَكْثَرُهُمْ كَاذِبُونَ

“Je, nikujulisheni wanaowateremkia mashaytwaan? Wanateremka juu ya kila mzushi mwenye kutenda dhambi. Wanaotega sikio na wengi wao ni waongo.”[1]

Hayo yanatendeka kwa mashaytwaan kuiba neno kutoka katika maneno ya Malaika na akayafikisha sikioni mwa kuhani. Baada ya hapo kuhani huyo hudanganya kwa neno hilo uongo mia moja. Matokeo yake watu humsadikisha kwa sababu ya lile neno moja alilosikia kutoka mbinguni.

Allaah (´Azza wa Jall) pekee ndiye kapwekeka na elimu ya mambo yaliyofichikana. Kwa hivyo yule mwenye kudai kushirikiana naye kwenye chochote katika mambo hayo, kwa kuhani au mwengine, au akamsadikisha mwenye kudai hivo, basi huyo amemjaalia Allaah mshirika katika sifa ambazo ni Zake pekee. Ukuhani hausalimiki kutokamana na shirki. Kwa sababu inahusiana na kujikurubisha kwa mashaytwaan kwa wayapendayo. Kwa upande wa kudai kushirikiana na Allaah katika elimu Yake mtu anakuwa ameshirikisha katika uola. Kwa upande wa kujikurubisha kwa asiyekuwa Allaah kwa kitu katika ´ibaadah mtu anakuwa ameshirikisha katika ´ibaadah. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kumwendea kuhani akamsadikisha ayasemayo, basi ameyakufuru yaliyoteremshwa kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[2]

[1] 26:221-223

[2] Ahmad (10170), Abu Daawuud (394), at-Tirmidhiy (135) na  Ibn Maajah (639).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 105-107
  • Imechapishwa: 23/03/2020