57. Mwenye busara na upole na kutofanya haraka

1 – Ni wajibu kwa mwenye busara kufanya upole katika mambo yote na kuacha kuwa na haraka. Allaah (´Azza wa Jall) anapenda kufanya upole katika mambo yote. Yule anayenyimwa upole basi amenyimwa kheri. Ambaye amepewa upole basi amepewa kheri. Mtu anakaribia kutofikia ndoto yake asipolazimiana na upole na kuepuka kuwa na haraka.

2 – Mwenye busara anakuwa mpole na mkati na kati. Kupindukia mipaka ni kasoro. Kuzembea ni kushindwa. Yale yasiyorekebishwa kwa kufanya upole basi hayarekebishwi kwa kufanya ukali. Hakuna dalili ya ustadi kama upole. Hakuna msaidizi mwenye nguvu kama busara. Upole unapelekea kuwa mwangalifu. Ndani ya uangalifu kuna usalama. Kuacha upole kunapelekea katika upumbavu. Ndani ya upumbavu kuna maangamivu.

3 – Mpole anakaribia kutotanguliwa. Mtu mwenye haraka anakaribia kutowahi. Anayenyamaza anakaribia kutojuta. Anayezungumza anakaribia kutosalimika. Mtu mwenye haraka huzungumza kabla ya kujua, hujibu kabla ya kufahamu, anasifu kabla ya kujaribu, anasimanga baada ya kwamba ameshasifu, huamua kabla ya kufikiria na huenda kabla ya kuamua. Papara imeambatana na majuto. Usalama umejitenga kutokamana na jambo hilo. Waarabu walikuwa wakiita haraka “Mama wa majuto”.

4 – Majuto ni yenye kutunza haraka. Hakuna yeyote aliyefanya haraka isipokuwa alijuta na kusemwa vibaya. Kuchukua hatua ya kufanya kitendo baada ya kuzingatia  ni thabiti zaidi kuliko kukisimamisha baada ya kuanza kukifanya. Haraka kamwe si yenye kusemwa vizuri.

5 – Sababu ya mafanikio ni kuacha uzembe. Dawa ya kunyimwa ni uvivu. Uvivu ni adui wa muruwa na adhabu kwa kijana. Uzembe na kushindwa kunapelekea katika maangamivu. Uzembe wakati wa fursa nzuri ni kosa kubwa. Haraka kabla ya kuweza ni kosa kama vivyo hivyo. Mwenye busara ni yule aliyeepuka haraka. Mkosefu ni yule aliyekosea kutokana na kuzembea. Mwenye haraka daima hukosea. Mwenye kuhakikisha daima hupatia.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 215-218
  • Imechapishwa: 25/08/2021