55. Dalili ya swalah na zakaah na na tafsiri ya Tawhiyd

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya swalah na zakaah na tafsiri ya Tawhiyd, ni maneno Yake (Ta´ala):

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini, wenye kupondoka kwenye haki na kuiacha batili, na wasimamishe swalah na watoe zakah – na hiyo ndiyo dini iliyosimama imara.” (al-Bayyinah 98 : 05)

MAELEZO

Dalili ya swalah na zakaah – Bi maana dalili ya kwamba swalah na Zakaah ni katika dini ni maneno Yake (Ta´ala):

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini, wenye kupondoka kwenye haki na kuiacha batili, na wasimamishe swalah na watoe zakah – na hiyo ndiyo dini iliyosimama imara.”

Aayah hii imeenea na imekusanya aina zote za  ´ibaadah. Hivyo ni lazima kwa mtu amwabudu Allaah (´Azza wa Jall) kwa kumtakasia ´ibaadah na kufuata Shari´ah Yake.

Swalah na zakaah – Kusimamisha swalah na kutoa zakaah ni katika ´ibaadah, lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ametaja mawili hayo kutokana na ule umuhimu wake mkubwa. Swalah ni ´ibaadah ya kimwili, wakati zakaah ni ´ibaadah ya kimali. Vimetajwa sambamba katika Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jall).

Na hiyo ndio – Bi maana kumwabudu Allaah pekee, hali ya kumtakasia Yeye dini, kusimamisha swalah na kutoa zakaah.

Dini iliyosimama imara – Hiyo ndio dini iliyosimama barabara, kwa sababu ndio dini ya Allaah (´Azza wa Jall) na dini ya Allaah ni yenye kunyooka. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Kwamba hii ni njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate njia za vichochoro nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo alivyokuusieni kwayo mpate kumcha.” (al-An´aam 06 : 153)

Kama ambavo Aayah hii tukufu imetaja ´ibaadah na swalah na zakaah, vivyo hivyo imetaja ukweli wa Tawhiyd, nako ni kumwabudu Allaah kwa kumtakasia ´ibaadah Allaah (´Azza wa Jalla) pekee na kujiweka mbali na shirki. Yule asiyemwabudu Allaah kwa kumtakasia Yeye dini hazingatiwi kuwa ni mpwekeshaji. Yule mwenye kumfanyia ´ibaadah mwengine asiyekuwa Allaah, basi hazingatiwi pia kuwa ni mpwekeshaji.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 76-77
  • Imechapishwa: 31/05/2020