55. Baadhi ya fadhila za Muhaajiruun na Answaar


Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

23- Vilevile na Wanusuraji wake na Wahajiri wa miji yao

     kwa unusuraji wao wameokolewa na Moto

MAELEZO

Muhaajiruun na Answaar vilevile wana fadhila kubwa. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ

“Na wale waliotangulia awali katika Muhaajiruun na Answaar… ” (09:100)

Muhaajiruun ni wale waliohama kutoka Makkah kwenda al-Madiynah. Walihama wakaiacha miji yao kwa ajili ya kuunusuru Uislamu.

Answaar ni wale waliomnusuru Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakawasaidia ndugu zao katika mji wa kuhamia. Haya yametajwa katika Suurah “al-Hashr”:

لِلْفُقَرَاءِ الْمُهَاجِرِينَ الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَأَمْوَالِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا وَيَنصُرُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ

“Mafuqara Muhaajiruun ambao wametolewa kutoka majumbani mwao na  [zikataifishwa] mali zao wanatafuta fadhila na radhi kutoka kwa Allaah na wanamnusuru Allaah na Mtume Wake – hao ndio wakweli.” (59:08)

Halafu akasema kuhusu Answaar:

وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِّمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“Na wale waliokuwa na makazi na wakawa na imani kabla yao wanawapenda wale waliohajiri kwao na wala hawapati kuhisi uzito wowote vifuani mwao kwa yale waliyopewa [Muhaajiruun] na wanawapendelea kuliko nafsi zao japokuwa wao wenyewe wako na njaa. Na yeyote anayeepushwa na ubakhili na tamaa ya uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.” (59:09)

kwa unusuraji wao wameokolewa na Moto – Allaah amewaokoa na Moto kwa kusuhubiana kwao na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).