3 – Kuhusu mwanamke mtumzima ambaye kishaolewa haozeshwi isipokuwa kwa idhini yake. Idhini yake ni kule kuzungumza tofauti na bikira ambaye idhini yake ni kule kunyamaza.

Mtunzi wa “al-Mughniy” amesema:

“Kuhusu mtumzima hatujui tofauti kati ya wanachuoni kwamba idhini yake ni kutamka kutoa khabari. Jengine ni kwa sababu kutamka ndio kunaashiria kilichomo moyoni na ndio kinachozingatiwa katika kila pahali ambapo kunazingatiwa idhini.”[1]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Haitakikani kwa yeyote kumuozesha mwanamke isipokuwa kwa idhini yake, kama alivyoamrisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akichukia kitendo hicho basi hatolazimishwa kuolewa isipokuwa msichana mdogo ambaye ni bikira. Baba yake anaweza kumuozesha na yeye hana idhini. Kuhusu mtumzima ambaye kishabaleghe haijuzu kumuozesha pasi na idhini yake; si kwa baba wala mwengine kwa maafikiano ya waislamu. Kadhalika bikira ambaye kishabaleghe haifai kwa mwengine mbali na baba na babu kumuozesha bila idhini yake kwa maafikiano ya waislamu. Ama baba na babu wanatakiwa kwanza kumtaka idhini. Wanachuoni wakatofautiana juu ya kumtaka idhini kama ni wajibu au imependekezwa tu; maoni sahihi zaidi ni kwamba ni wajibu. Ni wajibu kwa msimamizi wa mwanamke kumcha Allaah juu ya yule anayemuozesha naye na amtazame yule mume kama ni mwema au si mwema. Kwani anamuozesha kwa manufaa yake mwanamke na si kwa manufaa yake yeye.”[2]

[1] (06/493).

[2] (32/39-40).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 104-105
  • Imechapishwa: 19/11/2019