52. Qur-aan ni maneno ya Allaah


Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Qur-aan ni manneo ya Allaah. Haikuumbwa ili imalizike wala sio sifa ya kiumbe ili itokomee.

MAELEZO

Miongoni mwa yale wanayoamini Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kwamba Qur-aan ni maneno ya Allaah iliyoteremshwa na haikuumbwa. Kwake ndiko imeanza na Kwake ndiko itarejea. Qur-aan tukufu ni sehemu katika maneno ya Allaah na maneno ya Allaah hayamaliziki. Ni maneno ya Allaah ambayo kwayo anawaendesha viumbe Wake kwa maamrisho na makatazo. Hayana mwanzo wala mwisho. Maneno aina yake ni ya kale milele (قديمة النوع), na yanazuka kutegemea na matukio (حادثة الآحاد). Hiyo ina maana kwamba Anazungumza (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa akitakacho, pale anapotaka na kwa namna anayotaka daima na siku zote. Maneno Yake (Subhaanahu wa Ta´ala) ni sifa Yake ya kimatendo ambayo anasifiwa kwayo pale anapotaka. Miongoni mwa maneno Yake ni pamoja na maneno yanayozuka kutegemea na matukio, ikiwemo Qur-aan na vitabu vyenginevyo vilivyoteremshwa kwa Mitume. Allaah alizungumza kwa Tawraat, Injiyl, Qur-aan na vitabu vyenginevyo vilivyoteremshwa. Anamzungumzisha amtakaye miongoni mwa waja Wake kwa namna anayotaka. Ni lazima kuamini jambo hilo. Qur-aan ni maneno ya Allaah inapokuja kimatamshi na kimaana.

Jahmiyyah wanamkanushia Allaah maneno kama ambavo wanamkanushia sifa nyenginezo zote. Wanasema kuwa maneno Yake yameumbwa na kwamba Allaah ameyaumba ima katika Ubao uliohifadhiwa au ndani ya Jibriyl, Muhammad, Muusa na ´Iysaa. Kwa msemo mwingine wanaona kuwa ni katika jumla ya viumbe. ´Aqiydah hii ni batili. Maneno ya Allaah ni sifa miongoni mwa sifa Zake za kimatendo na hayakuumbwa na wala hayafanani na maneno ya viumbe.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 42
  • Imechapishwa: 02/08/2021