Kwa hiyo ndoa ina manufaa mengi. Moja katika manufaa makubwa ni kwamba inamlinda mtu kutokamana na uzinzi na uchache wa kutazama mambo ya haramu.

Miongoni mwake ni kupata kizazi na kuhifadhi nasabu.

Miongoni mwake wanandoa kupata utulivu na kutulizana kwa nafsi.

Miongoni mwake ni wanandoa kusaidiana kutengeneza familia njema ambayo ni moja ya matofali ya jamii ya Kiislamu.

Miongoni mwake mume kusimamia malezi ya mwanamke na kumuhifadhi. Mwanamke kusimamia kazi za nyumbani na kutekeleza kazi yake ya kikweli katika maisha yake. Mambo si kama wanavodai maadui wa mwanamke na maadui wa jamii eti kwamba mwanamke ni mshirika wa mwanaume katika kufanya kazi nje ya nyumbani. Matokeo yake wakamtoa nje ya nyumba yake na wakamwondoa nje ya kazi yake ambayo ndio ya kikweli na wakampa kazi za mtu mwingine na kumpokonya kazi zake na kumpa mwengine. Natija yake mpangilio wa familia ukaharibika na kukatokea kati ya wanandoa kufahamiana vibaya, mambo ambayo mara nyingi yamepelekea mume na mke kuachana au kubaki juu ya majanga na usumbufu.

Shaykh wetu Muhammad al-Aamiyn ash-Shanqiytwiy (Rahimahu Allaah) amesema katika “Adhwaa´-ul-Bayaan”:

“Tambua – Allaah aniwafikishe mimi na wewe katika anayoyapenda na kuyaridhia – ya kwamba fikira hizi za kimakosa, ambazo ni duni na zinazopingana na hisia, akili, Wahy wa kimbingu na Shari´ah ya Muumbaji kumfanya sawa mume na mke katika hukumu na nyanja zote. Ndani yake kuna ufisadi na kuuharibu mpangilio wa jamii ya kibinadamu, jambo ambalo halifichikani kwa yeyote isipokuwa tu yule ambaye Allaah amempofoa macho yake. Hayo ni kwa sababu Allaah (´Azza wa Jall) amemjaalia mwanamke na sifa ambazo ni maalum kwake na zenye kufaa kwa sampuli ya ushirikiano katika kuijenga jamii ya mwanadamu, isilahi ambayo haimfai isipokuwa yeye mwanamke; kama mfano wa kushika mimba, kuzaa, kunyonyesha, kuwalea watoto, kuihudumia nyumba, kusimamia kazi zake kama za kupika, kukanda unga, kufagia na mengineyo. Huduma hizi anazozifanya kwa ajili ya jamii ya kiutu ziko ndani ya nyumba yake katika sitara, ulinzi, heshima, kulinda utukufu na ubora wake; [huduma hizi] hazipungui na huduma za mwanaume za kutafuta riziki. Ndipo wakadai wale wajinga wapumbavu katika makafiri na wenye kuwafuata kichwa mchunga kwamba mwanamke ana haki katika kuhudumia nje ya nyumba kama alizonazo mwanaume. Pamoja na kwamba katika kipindi cha ujauzito wake, kunyonyesha kwake na damu yake ya uzazi hawezi kufanya kazi yoyote ambayo ni nzito, kama jambo linavyoshuhudiwa. Hivyo, mwanamke yeye akitoka na mume ndiye akabaki anahudumia nyumba, basi mambo yote huharibika katika kuhifadhi watoto wachanga, kuwanyonyesha wale ambao bado wananyonya na kumwandalia mume chakula na kinywaji anapotoka kazini. Akimwajiri mtu kwa ajili ya kukaa mahali pake basi mtu huyo pia ataharibu nyumba hiyo uharibifu ambao yule mwanamke ametoka nje kwa ajili ya kukimbia. Natija inarudi katika jukumu lake mwanamke. Ingawa kwamba kutoka mwanamke na kufanya kwake kazi kunapoteza muruwa na dini yake.”[1]

Kwa hiyo basi, enyi kina dada wa Kiislamu, mcheni Allaah. Msihadaike na madai haya ya uongo. Uhakika wa hali ya wale wanawake waliohadaika nayo ni ushahidi tosha juu ya kuharibika na kupotea kwao. Uzowefu ni dalili bora kabisa.

[1] (03/422).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 100-102
  • Imechapishwa: 18/11/2019